Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge kuhusu Mapendekezo ya Kuridhia Itifaki ya Biashara ya Huduma ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ya Mwaka 2012

Hon. Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge kuhusu Mapendekezo ya Kuridhia Itifaki ya Biashara ya Huduma ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ya Mwaka 2012

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kutoa machache kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri katika kuridhia itifaki ya biashara ya huduma ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ya mwaka 2012.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuendelea kutupa uzima na hadi leo kutufikisha hapa kujadili itifaki hii muhimu. Lakini pili nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini kuendelea kutumikia nchi yangu katika nafasi ya Naibu Waziri katika Wizara ya Viwanda na Biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuruni nanyi pia Viongozi wetu wa Bunge, wewe Mwenyekiti lakini Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wote ambao mmeendelea kutuongoza vizuri hapa Bungeni lakini pia ushirikiano mkubwa mnaopata kutoka kwa Wabunge wenzetu katika kujadili masuala mbalimbali ambayo ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, itifaki ya biashara ya huduma ni mwongozo unaotoa wajibu wa kila nchi mwananchama wa SADC namna ya kushughulikia sekta ya huduma katika nchi yake na hii ni matokeo kama ambavyo Mheshimiwa Waziri amesema ni matokeo ya utekelezaji wa itifaki ya biashara ya mwaka 1996 ambayo nayo iliendelea kujadiliwa na utekelezaji wake ukaanza Januari mwaka 2000. Nasema hili kwa sababu kumekuwa na hoja ya kwamba labda sisi tumechelewa sana kuridhia itifaki hii ya huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutia saini itifaki hii mwaka 2012 pale Maputo Msumbiji kulikuwa na muda wa majadiliano katika nchi zote ambayo majadiliano hayo yalikamilika mwaka 2019. Kwa hiyo, katika muda huo ilikuwa kila nchi inafanya majadiliano ili kuona namna gani wataweza kunufaika au kushiriki katika itifaki hii ya huduma ya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nchi zile kumi na moja ambazo zimeiridhia ni kwamba ni baada ya hapo. Kwa hiyo, ni takribani kuanzia mwaka 2022 takribani mwaka mmoja ndiyo utekelezaji hasa wa hii itifaki umeanza. Kwa hiyo, Watanzania, Waheshimiwa Wabunge hatujachewelewa ni muda muafaka lakini pia kuchelewa huko kwa mwaka mmoja ni muda mzuri ambao na sisi tumejitafakari kuona namna gani tunaweza kushiriki kikamilifu katika itifaki hii ya huduma au biashara za huduma katika Jumuiya ya SADC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na hoja nyingi sana ambazo zimetolewa hapa lakini muhimu kwanza nikuona namna gani tunaboresha sera zetu, sheria na kanuni lakini na mipango mbalimbali ambayo itawezesha sisi kama nchi kuweza kunufaika baada ya kuridhia itifaki hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi ni hoja muhimu na sisi tumeishaanza kufanya hivyo pamoja na mambo mengine sera zetu zinauhushwa na ziko katika ngazi mbalimbali baada ya muda siyo mrefu italetwa hapa Bungeni ili nazo ziweze kupitishwa naamini hiyo itasaidia kuhakikisha tunapoanza baada ya kuridhia, naamini baada ya kuridhia itifaki hii zitatuwezesha kutekeleza vizuri maazimio ambayo yatakuwa yamepitishwa katika azimio hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na hoja muhimu sana ambayo sisi kama Serikali kuona namna gani tunawezesha sekta binafsi ili iweze kuwa shindani tuandae baada ya kuridhia itifaki ya biashara za bidhaa protocol on trade ya 2000. Sasa wafanyabiashara na wafanyabiashara na bidhaa mbalimbali lakini changamoto imekuwa katika sasa huduma kwamba sasa huduma kwamba mtu anaweza akawa anatoka na bidhaa zake hapa kupeleka Afrika Kusini lakini sasa hauwezi kusafirisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo tunayofanya sasa huduma hizi zilizopo ni baina ya nchi na nchi bilateral kama ni benki kati ya Tanzania na Burundi au DRC mfano hiyo lakini hizi ni bilateral agreement kati ya nchi na nchi au makampuni ama makampuni katika kufanyia biashara. Sasa tunataka tuseme katika Jumuiya tuweze kufanya makubaliano namna ya kushiriki katika huduma za biashara. Kwa hiyo, Serikali tunaona ni muhimu sana ndiyo maana nimeleta hapa turidhie ili tuweze kuwahusisha wafanyabiashara wetu waweze kufanya biashara zao vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi haja kubwa, hoja kubwa ambayo imeelezwa ni namna ambavyo sisi kama nchi kama Serikali tunaendelea kutoa elimu kwa wadau mbalimbali ili kuweza kushiriki fursa zinazotokana na Jumuiya zetu zilizopo ikiwemo hii ya SADC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tunaendelea kufanya hivyo na tunaendelea kutoa elimu kwa wadau wote ikiwemo wafanyabiashara, sekta binafsi lakini pia kwa wananchi kwa ujumla ili wajue nini tunafanya kama Serikali ili kuhakikisha tunainua uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu tuweze kuridhia itifaki hii ambayo ni muhimu sana kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu kama walivyosema Waheshimiwa Wabunge sisi siyo kisiwa kwa hiyo hatuwezi kujetenga kusema tutashindwa, tutakaa peke yetu wakati wenzetu wanakwenda katika kuridhia itifaki hii na tayari nchi kumi na moja zisharidhia. Kwa hiyo, ni sisi ni muda muafaka baada ya kutathimini na kutafakari kwa kina tunaamini sasa ni muda muafaka kuridhia tuweze kuendelea na sisi kufaidika na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, ahsante sana, nakushukuru. (Makofi)