Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge kuhusu Mapendekezo ya Kuridhia Itifaki ya Biashara ya Huduma ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ya Mwaka 2012

Hon. Francis Isack Mtinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge kuhusu Mapendekezo ya Kuridhia Itifaki ya Biashara ya Huduma ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ya Mwaka 2012

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia itifaki hii ya huduma za kibiashara ya nchi za SADC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuwapongeza sana Wabunge wenzetu ambao wameendelea kuaminiwa na Mheshimiwa Rais ya kuwapa kazi ya kumsaidia katika kuiongoza na kuiendesha nchi yake lakini pia niwape pongezi wale ambao wanaingia kwa mara ya kwanza na hususani Mwenyekiti wetu wa Kamati yetu Mheshimiwa Kihenzile Mwenyekiti wetu hodari sana kwakupata nafasi naamini yale ambayo alikuwa anayafanya mazuri sana kwenye Kamati yetu sasa anaenda kuyaonyesha kwenye Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niendelee kumpongeza sana Rais wangu kwa jinsi ambavyo anaendelea kuupiga mwingi na nchi yetu inaendelea kunufaika sana na mambo mengi ambayo Rais wetu anayafuatilia. Jimbo langu leo linaogelea mambo mengi sana ya kimaendeleo kwa sababu ya kazi nzuri anayoipiga Rais wetu. Naamini hata hao wachache ambao wamehamishwa hamishwa wataendelea kuyafanya hayo mambo ya kumsaidia Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naunga mkono kwamba itifaki hii niombe Bunge liipitishe pamoja na kuchelewa kwa muda mrefu sana. Ni kweli miaka mingi imepita takribani kumi na moja tangu isainiwe mtu yeyote anaweza akawa na hofu kidogo kwanini imechelewa? lakini waswahili wanasema chelewa ufike. Tumechelewa lakini sasa tunafika ni jambo la msingi sana kulifanya kwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu niiombe Serikali sisi kama Bunge tunaridhia sasa lakini wao ndiyo watekelezaji wa hizi itifaki ambazo tunaridhia kwa maana ya kwamba wanakwenda sasa kufanya mikataba mbali mbali bilateral kati ya sekta zinazohusika katika utendendaji wa hizi itifakia ambazo tunazipitisha. Kwa hivyo ningewaomba sana Serikali washirikishe sana sekta binafsi kwa karibu sana katika utekelezaji wa hizi itifaki kwasababu wao ndiyo walaji wakubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano tukichukulia tu suala la mabenki wafanyabiashara wetu wamekuwa na tabu sana wanapofanyabiashara katika nchi hizi na hasa ukizingia hata sasa kwa mfano tatizo la dola naamini kama nchi hizi zote za SADC mabenki yetu yatakua katika nchi hizo, ufanyaji wa biashara utakuwa mwepesi sana. Mtu anaweza akaenda hata nchi nyingine akatumia local currency yetu kwa kujua benki yetu iko kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana Serikali iziwezeshe benki zetu lakini pia izishirikishe na kuzishauri na kua karibu nao katika kuwahamasisha kuanzisha mabenki katika nchi takribani zote tu za itifaki hii nchi za SADC ili hili suala la biashara liwe jepesi sana. Mfanyabiashara akienda nchi ya SADC yeyote akaikuta benki yake ya NMB au CRDB iko kule hata ile imani tu ya ufanyaji wa biashara anakuwanayo lakini pia usaidizi wa karibu wakupata hata anapopata tatizo lolote la kifedha au la kibiashara inakuwa rahisi sana. Kwasababu unahisi kama benki yako ndiyo kama uko kwenye nchi yako tu kwa sababu benki yako unayoijua na unayoiamini iko kule. Lakini vilevile benki yetu itaendelea kufanya biashara katika maeneo yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningeomba sana Serikali iangalie kwa karibu sana jambo hili la kushirikisha mabenki kuhakikisha na kuyawezesha na kuyashauri kwa vyovyote inavyowezena ili kuweza kufungua katika hizi nchi za SADC na tuweze kulifaidi vizuri soko hili. Kwa sababu biashara ni fedha, usipokuwa na fedha hamna biashara ambayo utaweza kuifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kuishauri Serikali katika suala la huduma ya afya niwaombe Serikali itimize ndoto ya Rais Jakaya Kikwete ya kuifanya Hospitali ya Benjamini Mkapa kuwa kituo cha kimataifa cha afya pamoja na utafiti. Nahakika kabisa kama tutafanya mambo ambayo yalikusudiwa pale huduma, vifaa na madaktari tunao wengi, madaktari wetu mabingwa wako katika nchi za watu wanatibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi ninahakika kama tukiwezesha hospitali hii kuwa kituo cha utafiti kikubwa na tiba basi Tanzania ndiyo itakuwa India ya hizi nchi zote za SADC na hivyo tutakuwa sasa tunatengeneza utalii, utalii wa kihuduma, utalii wa kimatibabu na hivyo kufanya nchi yetu kupata fedha nyingi za kigeni lakini vilevile kuwa tumeitendea haki itifaki hii katika sekta hii ya huduma ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali hebu hili iliangalie kwa makini tayari kuna kitu kikubwa pale kimeanza ni kiasi cha kuongeza nguvu tu na tutasababisha nchi zote hizi zikaitegemea nchi yetu. Tiba ni vifaa na madaktari na naamini nchi yetu tuna uwezo mkubwa sana kama tumeweza kujenga mabwawa ya matrilioni, tumeweza kuweka hizi standard gauge za matrilioni hatuwezi kushindwa ku-invest kwenye afya hapa Benjamini Mkapa na hizi nchi zote zikatutegemea wakaachana na habari ya kwenda India, India yao ikawa hapa Dodoma hapa Tanzania na hivyo kuweza kufanya hii huduma tukatumia vizuri hili soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa pia kuangalia Serikali iwezeshe hizi biashara zetu ndogo ndogo kufanyika kwa urahisi Wafanyabiashara wetu wamekuwa wakiteseka sana. Unakuta mtu anaenda kwenye mpaka anabidhaa anaambiwa hii bidhaa hairuhusiwi kuingia huku, kwa mfano kuna nchi zinakataa nyama yetu wakati zipo nchi za jirani zinanua mifugo yetu, zinakwenda zinachinja huko zinapata nyama zinapeleka kwenye hizo nchi ambazo zinakataa, zinasingizia kwamba sisi hatuchanji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, unaona kuna vihujuma vidogo vidogo ambavyo vinafanyika. Sasa itifaki kama hizi ebu ziwe mwarubaini sasa wa kutibu hizi hujuma ndogo ndogo na Serikali iangalie kabisa kama tuna mahusiano ya kupeana huduma, huduma ziko za aina nyingi sasa huduma siyo tuhujumiane pia. Kwa hiyo, ningependa Serikali iwe makini sana kuhakikisha wafanyabiashara wetu hawateseki na wanafaidi hili soko kubwa kwa kuepukana na hizi hujuma ndogo ndogo ambazo zinafanyika katika biashara zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuangalie sheria zetu, sheria zetu zingine zinatushika miguu sisi wenyewe, ningeomba Serikali ebu iangalie kwa makini sheria ambazo zimepitwa na wakati kuna mambo mengine tunajishika miguu wenyewe. Unakuta mtu anataka kupeleka nyama mahala anafika boarder au anafika bandarini anambiwa hebu lete cheti cha mionzi, wakati hata hiyo nchi inayopelekewa hizo nyama hata habari ya mionzi hawana, hawajui chochote kuhusu mionzi tunashikana miguu wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hebu tuangalie na vitu ambavyo sisi wenyewe vinafanya wafanyabiashara wetu wanashindwa kufanya biashara na hizi nchi na hivyo kufaidi hili soko kwa kuangalia zile sheria zilizopitwa na wakati turekebishe tufanye mambo ya biashara yawe rahisi katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine amelisema mama wa afya ya akili hapa Mheshimiwa Jesca suala la watu kufahamu kupata elimu juu ya hizi itifaki. Niiombe Serikali ni kweli inapoleta suala la itifaki Bungeni ni suala la Kibunge lakini niiombe Serikali iwe na mtindo wa kuwaanda wananchi kwamba sasa tunapeleka itifaki fulani Bungeni, itafaki inayowahusu ninyi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu bungeni ndiyo mahali pekee ambako tunaweza kumuita mwananchi, tunaweza kumwita mdau tukaja tukamsikiliza anasema nini kuhusu itifaki tunayotaka kuipitisha. Kwa hiyo, niiombe Serikali ijenge tabia ya kuwahabarisha wananchi, kuwahabarisha wadau kwamba tunapeleka itifaki fulani Bunge inayohusu jambo fulani kule ndiyo mahala ambako mnaweza kwenda kusema. Kwa hiyo, jamii na wadau wanakuwa na habari kwamba kuna itifaki inakwenda bungeni inakwenda kujadiliwa inayotuhusu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Bunge tunapowaita sasa wadau njooni mseme kuhusu itifaki wanakuwa wanauelewa. Kwa hiyo, tunapata input za watumiaji wa hiyo itifaki kwa hiyo, linakuwa ni jambo letu wote tunapolipitisha sasa tunapokuwa hawana habari halafu tunapitisha jambo Bunge tukitangaza sisi Bunge tuna taratibu zetu za kutangaza watu waje. Kwamba njooni msikilize lakini jinsi watanzania wetu tulivyo watu wengine magazeti hawasomi, mitandao hawapitii. Sasa kama Serikali haijawahabarisha vizuri tunapotangaza wadau waje hawawezi kuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe mfano sisi kwenye kamati yetu kuhusu jambo hili tumeaihirisha mara mbili tunataka wadau waje tuwasikilize kwa sababu tu watu wengine hawana information. Kwa hiyo, niiombe Serikali katika itifaki mbalimbali mnapotaka kuzileta Bungeni jengeni tabia ya kuwahabarisha wadau, habarisha wananchi kwamba tunapeleka itifaki Bungeni kule ndiyo mahala mnaweza kwenda kutoa input zetu ili tukipitisha linakuwa ni jambo letu na siyo la kutukana Bunge la kulaani Bunge kwa jambo ambalo sisi tumepitisha kwa nia njema, kwa nia ya kuwasaidia wao lakini kwa sababu hawakuwa na habari wanaona kama vile wamesalitiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali ijenge hii tabia ili twende kwa pamoja na wadau wawe wanafaidi hizi itifaki kwa sababu wanakuwa wanazielewa zimepita kwa nini na kwa manufaa gani na hivyo kuzitumia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nihitimishe tu kwakusema niliombe Bunge lipitishe hii itifaki kwa sababu ina nia njema lakini twende kwa pamoja na sisi Wabunge katika maeneo yetu tuendelee kuwahabarisha wafanyabiashara na watu wengine wafaidi hizi itifaki ambazo tunazitumia. Kwa sababu nchi yetu ni nchi kubwa yenye kila namna yenye neema na tukiyatumia vizuri itifaki hizi tutaendeleza maisha ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naunga mkono hoja, ahsante sana.