Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge kuhusu Mapendekezo ya Kuridhia Itifaki ya Biashara ya Huduma ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ya Mwaka 2012

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge kuhusu Mapendekezo ya Kuridhia Itifaki ya Biashara ya Huduma ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ya Mwaka 2012

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kutoa mchango wangu katika Azimio hili ambalo liko mbele ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nampongeza sana Waziri mwenye dhamana ya Viwanda na Biashara kwa kuleta Itifaki hii. Kipekee nawapongeza Kamati kwa namna ambavyo wamechakata na kutoa maoni ambayo na sisi tunaweza kupata mwanga wa kuweza kushauri katika kuridhia Itifaki ya Biashara ya Huduma ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika ya Mwaka 2012.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina wasiwasi kidogo kwa nini Itifaki hii imechelewa, lakini sio jambo geni kwa Tanzania, mara nyingi mambo mengi huwa tunachelewa, ila sasa kwa sababu sasa hivi dunia inakwenda kasi, ni vizuri tukipata fursa nzuri kama hizi, tukajitahidi kwenda nazo kwa haraka zaidi. Ninachotaka kusema ni kwamba sisi kabla ya mwaka 2000 Sera yetu ya Mambo ya Nje ilikuwa ni ukombozi wa Bara la Afrika na tulijikita zaidi Kusini mwa Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, karibu nchi zote hizi ambazo tunazozizungumzia, ukiacha zile ambazo zimepata uhuru kabla yetu au karibu na sisi, nyingine zote tumeshiriki kwa jasho na damu kusaidia kuzikomboa. Jambo hili lilikuwa na maana sana kwamba baada ya ukombozi ule wa kupata uhuru, basi wakishakuwa huru ni lazima tutengeneze utengemano kama huu wa kufanya biashara, kwa hiyo kwa hatua hiyo naipongeza Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningetaka niliseme ni kwamba, Sera yetu ya Mambo ya Nje wakati huo ilikuwa ni ya ukombozi, kwa hiyo ni vizuri tukaipitia upya Sera yetu ya Mambo ya Nje ya sasa ya Economic Diplomacy yaani Diplomasia ya Uchumi kwa sababu bado kuna maeneo mengi ya kiuchumi ambayo hatujayatumia vizuri kama Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi nchi tunazozizungumzia hapa ukiacha nchi mbili kwa maana ya Afrika Kusini na Angola, hizi nyingine zote GDP per capita tunawazidi, kwa maana sisi uchumi wetu uko juu zaidi. Sasa kwa jiografia ilivyo na utamaduni ulivyo ni kwamba nchi hizi karibu sehemu kubwa hata kabla ya kuridhia hii Itifaki tunazihudumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya mambo ambayo yametajwa kwenye Itifaki kwa mfano huduma za kifedha, zipo nchi kama DR Congo tayari kuna huduma za kifedha kwenye hizo nchi, kwa maana mikataba ya nchi na nchi, tayari kuna Benki ya CRDB ina-operate pale Lubumbashi. Ukienda Comoro tayari kuna Benki ya Exim nadhani na CRDB pia wana-operate pale Comoro. Kwa hiyo, utaona kwamba zile bilateral treaties tayari zinafanya kazi nje ya Itifaki hii kwa maana ya nchi na nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija katika mawanda mazima ya mawasiliano, kwenye mawasiliano tunazungumzia suala zima la uchukuzi na suala zima la logistics. Hii inafanyika, hata kwa kampuni moja moja lakini pia kwa nchi kwa maana kwamba tunaposafirisha bidhaa kutoka katika bandari zetu kwenda katika Nchi hizi za SADC bado kuna eneo ambalo tayari tunafanya. Kwa hiyo Itifaki hii iende ikaboreshe na kutengeneza mnyororo mzima wa kuthaminisha Itifaki hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo ambalo hatukufanya vizuri na ambalo tunataka Itifaki hii ambayo tunairidhia baada ya miaka 11, twende tukaisimamie ni suala zima la elimu. Kama ambavyo nimetangulia kusema kwenye utangulizi ni kwamba kwa kuwa tumeshiriki katika ukombozi wa hizi nchi maana yake tumezisaidia kwa namna moja ama nyingine hasa katika eneo la ulinzi na usalama (peace keeping). Ukifika huko mara nyingi askari polisi na jeshi kwa ujumla wake wamepewa mafunzo na Watanzania na ndiyo maana ukifika kwenye nchi hizo ukikutana na maaskari wanajua vizuri hata Kiswahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la elimu tunatakiwa tuingie hapo kupeleka huduma. Kwa mfano, huduma za elimu ya uhandisi, bado tuna wahandisi wengi hapa ndani ya nchi na hakuna ajira, ni lazima tutengeneze mkakati wa kuhakikisha tunasukuma watu wetu wa kada hiyo kwenda kufanya kazi katika nchi hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la afya, Wahadhiri wa vyuo tunatakiwa tuwapeleke huko kwa sababu sisi tuna idadi kubwa na wenzetu hawa baadhi ya nchi bado hazijajitosheleza, ni lazima tutumie fursa hiyo kupeleka watu wetu kutoa huduma hiyo ya elimu katika hizi nchi. Kwa sababu za kidiplomasia nashindwa kuzitaja, lakini tumefanya utafiti wa kina zipo nchi bado zinahitaji huduma ya Madaktari, zipo nchi zinazohitaji huduma ya Wahandisi na zipo nchi zinahitaji huduma ya Manesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo Watanzania wamethubutu wenyewe kwenda kwenye hizo nchi, lakini Tanzania haiwatambui, kwa maana Balozi zetu zilizopo kule haziwatambui kwa sababu wameenda wenyewe. Kwa hiyo, tunachotaka kumshauri Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana, aitumie vizuri Wizara ya Mambo ya Nje tuhakikishe kwamba Mabalozi wetu kwenye diplomasia ya uchumi kwa Nchi za SADC tuna-capitalize kwenye hili eneo la kuweza kusaidia Watanzania ambao wamesoma na ndani ya nchi tumeshindwa kuwaajiri, lakini kuna fursa hiyo nje ya Tanzania, basi waipate kupitia eneo hili la SADC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo liko kwenye Ibara ya 16 ni suala zima la afya. Afya hapa imetajwa kwa ujumla na nimeshataja katika maeneo hayo ya kitaaluma, lakini kwenye logistic chain ya usambazaji wa madawa, hapa nataka niweke wazi kwamba hata MSD waliwahi kupata zabuni ya kusambaza dawa katika nchi zote za SADC wakati huo zikiwa 13 na sasa zimefika 16.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana kwamba tunaweza tukahakikisha pia tunaishirikisha vema Wizara ya Afya kupitia MSD kwenda kutumia fursa hiyo ya kusambaza madawa katika hizo nchi. Imeonekana kwamba usambazaji wa dawa unaofanywa na MSD ndani ya Tanzania ni usambazaji wa kiwango cha kimataifa, hivyo wenzetu hawa wamevutiwa. Kwa hiyo, tutumie fursa hiyo ya kwenda kutengeneza logistic ya kwenda kusambaza dawa katika SADC, lakini wakati huo huo tukiitumia kama advantage ya kuhakikisha kwamba tunafungua viwanda vingi vya madawa katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dawa nyingi ambazo tunazisambaza katika nchi yetu hazizalishwi Tanzania. Source kubwa ya madawa yetu yanatoka Ujerumani na India. Kwa hiyo, maana yake kama SADC watamchukua MSD kwenda kusambaza madawa katika nchi zao inawezakana kabisa kwamba na dawa ambazo zitapita Tanzania au zitazalishwa Tanzania soko letu litakuwa kubwa zaidi. Tukiwekeza katika viwanda vya madawa maana yake dawa zetu zitakuwa ni sehemu ya kwenda kusambazwa katika Nchi za SADC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningetaka kushauri ni suala zima la ukuzaji wa Lugha ya Kiswahili. Hapa napo ni lazima tuwe na mkakati madhubuti. Kiswahili hiki tunachozungumza leo sio cha kwenda kufundishia. Ni lazima tujipange upya, BAKITA na Wizara inayohusika tuanze kuandaa wataalam, Linguists ambao watakwenda kufundisha hicho Kiswahili katika nchi ambazo tunakusudia. Haitawezekana kumfundisha Kiswahili kama hujui lugha yake. Zipo nchi zinazungumza Kireno, zipo nchi zinazungumza Kifaransa na zipo nchi zinazungumza Kiingereza. Kwa hiyo, ni lazima tuwaandae watu wetu watakaokwenda kufundisha Kiswahili wawe wanazijua hizo lugha ili waweze kurahisisha uwasilishaji na mawasiliano kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho lakini sio kwa umuhimu nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, lakini tunataka kuona mabadiliko makubwa katika eneo hili la SADC kwa sababu kwa jiografia ya nchi yetu ndiyo eneo kubwa zaidi ambalo linaingiza pato kubwa baada ya India. Sehemu nyingine ambayo tuna soko kubwa la watu hawa zaidi ya milioni 360 ni ukanda wa SADC. Kwa bahati nzuri ni kwamba ukanda huu unatutegemea zaidi sisi, kwa hiyo sisi katika Itifaki hii maana yake tunakwenda kupiga comparative advantage ya uwepo wetu katika SADC. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo, nakushukuru sana kwa nafasi, naunga mkono Itifaki hii. (Makofi)