Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge kuhusu Mapendekezo ya Kuridhia Itifaki ya Biashara ya Huduma ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ya Mwaka 2012

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge kuhusu Mapendekezo ya Kuridhia Itifaki ya Biashara ya Huduma ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ya Mwaka 2012

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Napenda kuipongeza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kutuletea kuridhia Itifaki hii ya SADC. Nawapongeza wote wa hapo Wizarani kwa juhudi zao mbalimbali za kuhakikisha nchi yetu inakwenda kunufaika na fursa mbalimbali zilizopo katika SADC na sehemu nyingine katika dunia yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na mapendekezo ya Kamati kwa kuishauri Serikali. Kati ya nchi tano ambazo hazijaridhia Azimio hili na Tanzania imo, leo hii tunakwenda kuridhia Azimio hili kwa manufaa ya nchi yetu, manufaa ya Watanzania na manufaa ya wafanyabiashara wetu wanaotoa huduma mbalimbali katika nchi. Tutanufaika na fursa mbalimbali zikiwemo biashara za huduma kama vile elimu, afya, usafirishaji na mambo mengine yanayohusu kutoa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumzwa hapa suala la kwamba tutapata fursa ya kukitumia na kukieneza Kiswahili katika ukanda huu wa SADC. Ushauri wangu kwa Serikali, tuitumie vema fursa hii ya uwekezeaji kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na vijana wetu ambao tayari ni weledi wa Lugha ya Kiswahili. Tuhakikishe Tanzania tunaendelea kukihakikisha Kiswahili ni cha Tanzania kuepusha soko hili likatekwa na nchi nyingine wakajifanya wao ndiyo wakuu wa Kiswahili. Nashauri tuendelee kuhamasisha vijana wetu kutumia fursa hii ya ajira kwa soko la kueneza Kiswahili kwa fani mbalimbali ualimu, ukalimani, uhadhiri na mambo mengine ya kuandika vitabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakwenda kunufaika pia na fursa nyingine kwa upande wa mazingira, tutanufaika pia kwa fursa za watoa huduma ikiwemo mawasiliano elimu na afya. Naishauri Serikali tuweke mazingira mazuri kwa watoa huduma wetu tulionao na Serikali kuanzisha kitengo maalum ndani ya Wizara cha kuibua fursa ambazo watakwenda kuwekeza katika hizo nchi nyingine za SADC. Kwa sababu, isiwe wao wanakuja kwetu tu kutumia fursa zetu lakini sisi hatupati kwenda. Ni vyema sasa tukawasaidia wafanyabiashara wetu hawa wa huduma namna ya fursa zilizokuwemo kwenye nchi za wenzetu za SADC ili tuwe tunabadilishana uzoefu na maarifa wao wanakuja na sisi tunakwenda. Tukifanya hivyo na sisi tutajitangaza zaidi kwa fursa mbalimbali za uwekezaji katika nchi nyingine za SADC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusaidie kuwawezesha kimitaji wafanyabiashara wetu watoa huduma, kwa sababu bado kuna hili tatizo la mitaji ya kutosha. Tuwasaidie namna ya kupata mitaji katika benki ili na wao waingie kwenye huu ushindani kwenye kuwekeza katika nchi mbalimbali za SADC ili tupate hayo manufaa na sisi ya kuingia kwenye SADC. Tukifanya hivyo wafanyabiashara wetu watoa huduma watakuwa na wao na ujasiri watakuwa na uelewa na weledi wa kuwekeza na watatoka uoga kwa sababu wakati mwingine ni hofu tu lakini tukiwatoa hofu tukawapa elimu na tukawapa maarifa ya kuingia, wataweza kuingia kwenye ushindani huu wa soko la kutoa huduma mbalimbali katika nchi za SADC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Bunge likubali kuridhia Azimio hili ili tuendane na wakati tusiwe tumeachwa nyuma twende sambamba na hali ya mabadiliko ya dunia ya sasa ili kuibua fursa za uwekezaji kwa wananchi wa Tanzania fursa za ajira, fursa za masomo na fursa nyingine za kuinua uchumi wa nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)