Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge Kuhusu Mapendekezo ya Kurejea Katiba ya Tume ya Usafiri wa Anga ya Afrika ya Mwaka 2009

Hon. Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge Kuhusu Mapendekezo ya Kurejea Katiba ya Tume ya Usafiri wa Anga ya Afrika ya Mwaka 2009

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ili niweze kuchangia kuhusu kuridhia Azimio hili la AFCAC. Naungana na Mheshimiwa Waziri pamoja na Kamati kwa namna ambavyo wameweza kuwasilisha jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili lina faida kubwa sana kwa nchi yetu, mpaka sasa tumechelewa. Kama ambavyo amesema Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake kwamba nchi zaidi ya 15 zimekwisharidhia, lakini sisi kama nchi bado hatujaridhia. Kuna faida kubwa sana kwa Taifa letu. Waheshimiwa Wabunge wengi hapa wameelezea faida ambazo zinatokana na kuridhiwa kwa itifaki hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba Waheshimiwa Wabunge waweze kuridhia jambo hili. Faida zake zimeelezwa kinagaubaga ikiwemo suala la kukuza lugha yetu ya Kiswahili, katika Katiba limeelezewa vizuri kabisa. Ukiisoma Katiba yetu kuanzia Article 24 imeeleza lugha itakayotumika ni pamoja na Kiswahili. Kwa hiyo, tutakuwa na sifa muhimu kwa ajili ya kueneza lugha yetu ya Kiswahili kwa Bara zima la Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni pamoja na soko shindani. Mheshimiwa Stella Fiyao amesema hapa, kwamba tujipange kama Serikali. Nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba kama Serikali tumejipanga vizuri kwa ajili ya kushindana na ndio maana na sisi kama nchi tunahitaji kuridhia ili tuendane na ulimwengu wa kileo. Kama tuliridhia mwaka 1969 na Katiba mpya ya 2009 tulisaini tangu mwaka 2010. Tulikuwa hatujaridhia kwa kipindi chote hicho tukisubiri wenzetu waweze kuridhia. Sasa nchi zaidi ya 15 zimeshasaini, maana yake sasa hivi sisi tuko nje ya mfumo ama hatuko ndani ya itifaki hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge na Watanzania wote kwamba kama Serikali tumejipanga vizuri katika soko hili shindani na hata ndege ambazo Mheshimiwa Rais amekuwa akitoa fedha kwa ajili ya kununua haziwezi kufanya kazi Tanzania peke yake. Tunahitaji kwenda kwenye mabara mengine, ili tukienda huko watalii waweze kuja lakini pia tufanye biashara na mataifa mengine. Hatuwezi kufanya hivyo kama jambo hili tutakuwa hatujaliridhia.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho lakini sio kwa umuhimu, Mheshimiwa Dkt. Chamuriho pia alizungumza suala la ni namna gani tumejipanga kutokana na mkataba ambao ulisainiwa kule Senegal Yamoussoukro. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumejipanga kwa namna hii; kwanza, kuna mikataba kati ya nchi na nchi lakini pili kuna mikataba kati ya bara na bara. Kwa namna sisi tunavyofanya mpaka sasa tutatumia mkataba unaoitwa BASA yaani Bilateral Air Services Agreement. Hata sasa tunafanya hili, kwa hiyo tusiwe na mashaka kwamba pengine tukiridhia makampuni makubwa kama Emirates yanaweza kuja ndani ya nchi, halafu yakaanza kufanya shunting za ndege kwa mfano kutoka Dar es Salaam kwenda mikoani, hilo halitakuwa hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana.