Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge Kuhusu Mapendekezo ya Kurejea Katiba ya Tume ya Usafiri wa Anga ya Afrika ya Mwaka 2009

Hon. Eng. Dr. Leonard Madaraka Chamuriho

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge Kuhusu Mapendekezo ya Kurejea Katiba ya Tume ya Usafiri wa Anga ya Afrika ya Mwaka 2009

MHE. ENG. DKT. LEONARD M. CHAMURIHO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniruhusu kuwa mchangiaji wa kwanza kwenye suala hili. Huu mkataba ni mzuri kwa AU kwa maudhui yake na utakwenda kutoa fursa nyingi kama ambavyo imetamkwa kuhusu faida zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna masuala ambayo yamo ndani ya hii itifaki ya kuridhia ambayo hayakuelezwa sawasawa, ambazo ni changamoto tunazoweza kuzipata katika kutekeleza hiki kitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nitajikita kwenye Mkataba wa Yamoussoukro ambao umeongelewa katika itifaki hii, ambao maudhui yake ni kufungua usafiri wa anga kwa Afrika nzima. Huko nyuma tuliona kwamba hili ni jambo jema lakini kwa mataifa ambayo yana mashirika ya ndege machanga inakuwa ni changamoto kidogo na ni hatari.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii Yamoussoukro Decision kama ambavyo imeonekana kwenye hii itifaki, tulikubaliana mwaka 1999 lakini bado sisi tulikuwa hatujaridhia kuitekeleza. Tulisaini lakini hatujaridhia kwa sababu ya athari zake ambazo tuliziona kule nyuma, ilikuwa ni kwamba, tunapokuwa na shirika dogo linaloanza tukifungua anga moja kwa moja, mashirika makubwa yatatumeza na tutashindwa kukua kwa haraka. Tulikuwa tunaona kwamba tungepata muda fulani ili tuweze kukua ili tuweze kuingia katika ushindani huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika maelezo yaliyotolewa sikupata hiyo comfort kwamba kuna muda fulani ambao tutajizatiti katika kujenga uwezo wa shirika letu la ndege ili tusimezwe na mashirika makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa Yamoussoukro Decision, una maana kwamba mashirika ya nje kwa mfano yanaweza yakapita ndani yakachukua abiria katika vituo vyetu vya ndani. Hiyo inafaa kwa nchi ambayo haina shirika la ndege, lakini kama una shirika lako la ndege inakuwa ni changamoto kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukienda katika kifungu cha tatu ambacho ni objectives, yaani malengo. Nikiangalia kifungu cha 3 (b) nikisoma kama kilivyoandikwa ni “Facilitating, coordinating and ensuring their successful implementation of Yamoussoukro Decision by supervising and managing African liberalise Air Transport Industry”. Hapa ndipo penye changamoto. Tukishachukua tungeambiwa vizuri kwamba tumejipangaje katika kulinda shirika letu la ndege lisimezwe wakati linakua.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, nikiangalia Article No. 4 (j) ambayo inasema, katika kazi mojawapo nikisoma hapa kama ilivyoandikwa ni “Pursuant to provision of the Article 9 of the Yamoussoukro Decision to discharge the duty of the executing agency of air transport in Africa”. Kwa hiyo bado tunasukuma kwamba, kama lengo litakuwa ni kusukuma utekelezaji wa hii Yamoussoukro Decision.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nikiangalia Article 11 (i) function of the plenary nayenyewe inaonesha kwamba itahakikisha utekelezaji wa hiyo Yamoussoukro Decision. Pia nikiangalia Article 18 ambayo inaongelea vikwazo ambavyo unaweza kufanyiwa. Kuna vikwazo ambavyo tunaweza tukawekewa kama tutashindwa utekelezaji wa hiyo kitu. Kwahiyo, ina maana kama tukishakubaliana na ile halafu tukasema anga linafunguliwa, huwezi kulizuia shirika la ndege la nchi nyingine, kwa mfano kupita Dar es Salaam likachukua abiria likawateremsha KIA au Mwanza na ambapo hiyo ilikuwa ni majukumu ya mashirika yetu ya ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tungepata maelezo mafupi tujue kwamba katika kuridhia hii, je, ulinzi wa shirika letu dogo ambalo linakua litakuwaje na tumechukulia vipi? Kwa hali ilivyo na bado tunakua; nilikuwa nashauri kwamba, tuweke muda wa kuruhusu shirika letu kukua kabla ya kuingia katika huu mradi ambao utahusisha ku-liberalise Air Transport Industry kwani katika ukuaji huo tunaweza tukamezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.