Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, nami ninakushukuru sana kwa kunipa wasaa huu katika kuchangia hoja iliyo mbele yetu, kwanza nianze kuunga mkono hoja hii.

Mheshimiwa Spika, ninamshukuru sana Mungu wa Mbingu na Dunia aliyetufanya leo tujadili hoja hii muhimu ndani ya Bunge lako Tukufu. Shukrani zangu za kipekee ziende kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ameendelea kuniamini kuwa Msaidizi wake katika nafasi hii ya Naibu Waziri sekta ya Uchukuzi kwa kipindi kingine tena. Shukrani zingine ziende kwa Mheshimiwa Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, zaidi Waziri wetu Profesa Mbarawa ambaye amekuwa Mwalimu mwema, ametufundisha na anatusimamia vema sisi Wasaidizi wake katika nafasi hii.

Mheshimiwa Spika, zaidi pia Waheshimiwa Wabunge niwapongeze wote kwa namna ambavyo mmechangia hotuba hii ya bajeti ya Wizara yetu ya Ujenzi na Uchukuzi pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu pamoja na wote ambao wengine wamechangia kwa njia ya maandishi lakini wengi mmeongea. Pia familia yangu mama, watoto pamoja na familia kwa ujumla na wananchi wangu wa Jimbo la Busokelo ambao wameniamini kwa kipindi hiki cha pili awamu ya pili kama Mbunge wao na Mwakilishi wa Jimbo la Busokelo.

Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze katika hoja za Waheshimiwa Wabunge. Waheshimiwa Wabunge naungana nanyi kwa michango yenu yote ambao wamechangia katika Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi. Nakumbuka Bunge kama hili la mwaka jana na mwaka huu ni tofauti sana, kwa kweli tunawashukuru sana na nitaanza kujielekeza katika ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR.

Mheshimiwa Spika, tunampongeza Mheshimiwa Rais tangu amepata nafasi ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu amesimamia vyema sana miradi yetu hii ya SGR. Wakati anaingia madarakani katika lot ya kwanza ilikuwa asilimia 83.55, hivi sasa ni asilimia zaidi ya 98.1. Lot Namba Mbili kwa maana ya kutoka Morogoro hadi Makutupora ilikuwa asilimia 57.57 sasa ni zaidi ya asilimia 93.4. Kwa kweli kazi imefanyika na kilometa zilizokuwepo zilikuwa ni 722 na sasa ni zaidi ya kilometa 1280 ambazo Mheshimiwa Rais katika awamu yake amesaini na thamani ya miradi yenye takribani zaidi ya trilioni 23.3 katika reli hii ya SGR. Kwa kweli tuna kila sababu ya kumshukuru na kumpongeza na vipande vinne vimesainiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutoa ufafanuzi kulikuwa kuna hoja za ni lini hasa SGR itaanza kufanyakazi. Reli hii ya kisasa kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro yenye kilometa 300, mara nyingi tumekuwa tukijibu swali hapa Bungeni, lakini nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba mabehewa yamekwishaingia baadhi lakini mengine mabehewa ya ghorofa kutoka Ujerumani yanaingia nchini ifikapo tarehe Mbili Juni na tunategemea kupata vichwa vya treni mwezi wa Julai. Kwa hiyo, mara tu baada ya vichwa vya treni kufika tunategemea huduma zitaanza kutolewa.

Mheshimiwa Spika, kipande hiki cha Dar es Salaam – Morogoro chenye kilometa 300 tunategemea kukamilika kwa kadri mkataba wetu ulivyo ni mwezi Septemba 2023. Kipande cha Morogoro - Makutupora tunategemea kukamilika Januari 2024 kwa sasa ni asilimia 93.83 ya mradi yenye kilometa 422.

Mheshimiwa Spika, kipande cha Makutupora - Tabora kinategemea kikamilike mwezi Desemba 2026 kwa sasa ina asilimia Saba yenye kilometa 368. Kipande cha Tabora- Isaka chenye kilometa 165 kwa sasa iko asilimia 2.39. kipande cha Isaka – Mwanza asilimia 31. 07 yenye kilometa 341. Kipande cha Tabora - Kigoma ambapo hivi sasa Mkandarasi yuko site na yupo kujenga camp.

Mheshimiwa Spika, kazi hii ya SGR imefanywa na wazawa wa kitanzania, Ma-Engineer wa Kitanzania ndiyo wame-design. Kupitia wataalam wetu na niwapongeze sana viongozi wote nikianza na Mkurugenzi Mtendaji wa TRC pamoja na Mainjinia wote walioshiriki katika design and building ya mradi huu ni mradi mkubwa kimkakati kwa hiyo tunategemea hata wenzetu wa ile reli ya kutoka Uvinza - Musongati mpaka Gitega yenye kilometa 317 hivi sasa mazungumzo yanaendelea Benki ya African Development imeonesha nia ya kufadhili mradi huu. Kwa hiyo, itakuwa kuna connection sasa kati ya reli na wa kwenda Kigoma pamoja na hii ambayo inaenda mpaka Burundi ambako kuna tani zaidi ya milioni 150 za nickel na ambazo tunategemea zisafirishwe kupitia SGR yetu. Takribani kwa mwaka tunakusudia, kwamba reli hii minimum itaweza kubeba tani milioni 17 kwa mwaka lakini maximum zaidi ya tani milioni 25. Kwa hiyo, niwapongeze wote wanaoshiriki katika ujenzi huu.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ninalotaka nizungumzie zaidi ni suala hili la Reli ya Kusini. Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia hapa Reli ya Kusini kwamba ni mkombozi na kweli nasi Wizara tumeliona hili. Reli ya Kusini kutoka Mbamba bay mpaka Mtwara. Tunatambua kwamba mizigo ama makaa ya mawe yanayosafirishwa na mizigo kutoka makaa ya mawe mpaka bandarini yanaharibu sana barabara zetu. Kwa maana hiyo Serikali imefanya nini?

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweza kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, hivi sasa tunatafuta fedha kwa njia ya ubia ili reli hii ianze pia kufanya kazi kama ambavyo reli ya kati tunayoijenga.

Mheshimiwa Spika, pia kulikuwa kuna hoja za ni lini hasa wakati mwingine behewa zile zilizokuja baadhi ya Wabunge walikuwa wanasema siyo yenyewe. Sasa nataka niwahakikishie kwamba kuna set za treni za kisasa EMU maana yake Electrical Multiple Unit kwa lugha nyingine tunasema treni zilizochongoka vichwa vyake navyo vitawasili hapa nchini ifikapo Machi, 2023.

Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie Watanzania wenzangu kwamba reli hii inakwenda vizuri na tuko vizuri kwamba itakamilika kwa wakati kama ambavyo nimeeleza.

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ilikuwa ni reli ya TAZARA. TAZARA ni muunganiko kati ya Tanzania na Zambia. Tarehe 14 Machi Waheshimiwa Mawaziri wetu kupitia Baraza la Mawaziri walifanya kikao. Changamoto kubwa reli hii ilikuwa ni suala la sheria iliyopo na wenzetu waliomba tuwape nafasi kwa sababu ni Serikali mpya, kwa hiyo wana-review sheria zote za nchi yao ikiwemo na hii ya TAZARA. Hatukuishia hapo tu baada ya kuona wenzetu wana-review hiyo sheria na sisi tayari tulishaanza maandalizi na tulisha-review lakini hatuwezi kufanya maamuzi lazima tuwashirikishe kama ambavyo mkataba wetu ulivyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nini ambacho kipo sasa hivi? Ni kwamba reli ya TAZARA tumeunda timu tatu, timu ya Mawaziri wa Tanzania na Zambia, timu ya Makatibu Wakuu pamoja na Watendaji Wakuu. Timu hizi kazi yao kubwa ni kuratibu zoezi hili la transition period kwa sababu tayari kuna wawekezaji ambao wameonesha nia kuishirikisha sekta binafsi ikiwemo wenzetu wa China kwamba wanaweza kuwekeza katika reli hii ya TAZARA.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ninalotaka nizungumzie zaidi ni suala zima la meli za Ziwa Tanganyika. Waheshimiwa Wabunge wa Mikoa yote hususan Mikoa ya Kigoma, Rukwa pamoja na Katavi na asubuhi hapa nimejibu swali kuhusiana na suala la Meli za Ziwa Tanganyika. Tumepokea ushauri wenu kwamba, badala ya kuwa na meli moja kubwa ambayo inabeba watu 600 na tani 400 tunategemea tufanye vile ambavyo mmeshauri. Ina-make sense kwamba tukiwa na meli mbili ambazo zinaweza zikawa zinapishana na kwa kuwa bado tuko katika kipindi cha majadiliano, ushauri wenu umepokelewa na Serikali tutaufanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine kuna meli zingine ambazo tunaendelea kuzikarabati, kwa mfano meli ya MV Liemba pamoja na MV Mwongozo. Mv Liemba tunasaini makataba mwezi ujao wa Sita na MV Mwongozo tayari Mkandarasi Mshauri ameshapatikana ambaye ni TMA, kwa hiyo nao wanaanza kazi rasmi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo limezungumzwa sana hapa ni suala la viwanja vya ndege nchini. Baadhi ya Wabunge wamechangia suala la kwamba ndege zetu nchini ikifika saa kumi na mbili wakati huo huo zinakwenda kulala na binadamu tunakwenda kulala. Sasa nini kifanyike? Ni kuweka taa katika viwanja vyetu vyote nchini ili ndege zifanye kazi masaa 24.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia jambo hilo katika bajeti ijayo 2022/2023 viwanja vifuatavyo vinakwenda kufungiwa taa. Kiwanja cha Arusha, Iringa, Msalato, Kigoma, Sumbawanga, Shinyanga, Lake Manyara, Tanga, Lindi. Kwa sababu kwa sasa, viwanja ambavyo vina taa ni vichache sana, kiwanja cha JNIA, kiwanja cha KIA, kiwanja cha Zanzibar, Mwanza, Tabora, Songwe, Songea na Mtwara. Kwa hiyo, maombi yenu na namna ambavyo mmechangia bajeti hii mjue kwamba, katika mipango yetu na kwa kuwa baadhi ya viwanja tayari tumeshasaini ni miongoni mwa maeneo ambayo tunakwenda kuweka taa katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna changamoto ya kiwanja cha Bukoba. Kiwanja cha Bukoba tumekipangia fedha kwa ajili ya kujenga control tower kwa maana ya kuongozea ndege pamoja na mifumo ya kuongozea ndege inayoitwa Instrument Landing System na hii mifumo itafungwa maeneo yote.

Mheshimiwa Spika, tuwaombe Waheshimiwa Wabunge watupitishie bajeti yetu ili haya yote ambayo ninayasema hapa yaweze kutekelezeka. Kulikuwa pia kuna jambo la miradi ya kimkakati ambayo Mheshimiwa Waziri wangu atakwenda kuizungumzia. Kwa hiyo, katika haya kulikuwa kuna jambo pia la umiliki wa ndege ambayo pia Mheshimiwa Waziri wangu ataenda kuzungumzia hususan kati ya ATCL pamoja na TGFA.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nikushukuru sana kwa muda huu, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa namna ya kipekee ambavyo wameweza kuchangia bajeti yetu na naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)