Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha mchango wangu kwa njia ya maandishi.

Mheshimiwa Spika, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema. Nampongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi iliyotukuka ya kuliongoza Taifa letu. Nakupongeza wewe binafsi, Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na wasaidizi wao na timu nzima ya Wizara.

Mheshimiwa Spika, nachangia maeneo matatu nikianza na ujenzi wa barabara ya Muhutwe - Kamachumu - Buganguzi - Kishanda - Nshamba - Muleba (Mujungi Road); barabara hii ina urefu wa kilometa 54. Barabara hii ilianza kujengwa kidogo kidogo tangu Serikali ya Awamu ya Nne, mpaka jana unasoma bajeti yako ya mwaka wa fedha 2023/2024, barabara hii imejengwa kwa kiwango cha lami kilometa 38 tu. Kwa taarifa kilometa 3.8 ziko kwenye maandalizi ya ujenzi kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, sehemu ya barabara iliyobaki ni kilometa 12 tu ili barabara hii ikamilike. Barabara hii imejengwa kwa muda mrefu. Nimeangalia kwa makini bajeti yako ambayo naichangia, barabara hii imetengewa kiasi kidogo cha pesa ambazo zitajenga labda kilometa moja tu. Naomba sana, barabara hii ni muhimu sana, nakuomba uongeze bajeti angalau kilometa saba ili bajeti ya mwaka ujao tumalizie ujenzi wa barabara hii. Namuomba sana Mheshimiwa Waziri tumalizie ujenzi wa barabara hii kabla ya uchaguzi wa mwaka 2025.

Mheshimiwa Spika, pili ni ujenzi wa uwanja wa ndege wa Omukajunguti; uwanja wa ndege wa Bukoba sio salama kwa kuruka na kutua ndege zetu za ATCL na Precision Air. Ndege hizi zinahitaji kutua kwenye uwanja wa ndege wenye njia ya kuruka na kutua ndege urefu kilometa mbili. Uwanja wa ndege wa Bukoba una njia ya kuruka na kutua ndege wenye urefu wa kilometa 1.5. Kwa bahati mbaya uwanja huu hauwezi kupanuliwa kutokana na jiografia ya eneo letu. Kwa sababu hiyo, nakuomba ujenzi wa uwanja wa ndege wa Omukajunguti ufanyike kipindi hiki.