Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Abeid Ighondo Ramadhani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake kwa utendaji kazi mzuri, pia watendaji akiwamo Katibu Mkuu Balozi Aisha.

Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa naomba kuwasilisha kilio cha wananchi wa Jimbo la Singida Kaskazini kuhusu barabara ya kutoka Singida - Ilongero - Haydom. Barabara hii ni ahadi ya viongozi wote wa Kitaifa ambao hufika Ilongero kuanzia Hayati Mwalimu Julius Nyerere hadi Rais aliyepo madarakani alipokuwa Makamu wa Rais alifika Ilongero akaahidi kuhakikisha barabara hii inawekwa lami.

Mheshimiwa Spika, cha kusikitisha hata katika bajeti hii ya leo barabara hii haipo katika mpango. Ni miaka 60 ya Uhuru leo Wana-Singida Kaskazini wanalia, wanateseka, wanataabika, wanakarahika na mateso ya hii barabara.

Mheshimiwa Spika, naomba Waziri aipe kipaumbele barabara hii muhimu kwa uchumi wa Wana-Singida, ni roho ya uchumi wa Wana-Singida Kaskazini. Ni barabara ya msaada mno lakini imekuwa longolongo miaka nenda-rudi, na mimi Mbunge nimechoka matusi ya wananchi. Naomba lami katika hii barabara katika bajeti hii ya mwaka 2023/2024.

Mheshimiwa Spika, naomba tupate walau kilometa kumi za lami katika barabara hii hadi makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Singida katika Mji Mdogo wa Ilongero. Watumishi hivi sasa hawakai kwa kukimbia mateso ya barabara hii hususan wakati wa masika na rasta zinazokera na kuharibu magari ya watu.

Mheshimiwa Spika, siungi mkono hoja ya bajeti ya Wizara hii ya Ujenzi hadi nione fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii muhimu sana kwa maisha ya Wana-Singida Kaskazini. Nataka nione kilometa kumi hadi katika Mji wa Ilongero.