Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon Ally Juma Makoa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kondoa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi. Awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna alilvyoonesha mafanikio makubwa sana kwenye Wizara mbalimbali hususan hii Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa miradi mikubwa ya reli, barabara, bandari, ununuzi wa ndege na miradi mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nitoe shukrani zangu kwa Wizara inayoongozwa na Mheshimiwa Mbarawa pamoja na Naibu Mawaziri wawili, Katibu Mkuu na Watendaji wote niwapongeze kwa juhudi kubwa za kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kutekeleza majukumu haya ya kuitengeneza Tanzania katika ubora wa viwango. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina mambo machache, kwanza nishukuru Wizara kupitia Mheshimiwa Mbarawa kwa kukubali kuingiza ile Barabara ya kutoka Dalai – Mondo kwenda Bicha ambayo ndiyo iliyokuwa imetajwa kwenye Ilani na baadaye kidogo kukawa na sintofahamu, lakini baada ya kutusikiliza ameamua kuirudisha, namshukuru sana, hii kilometa 35, sasa ni habari njema kwa Wakazi wa Kondoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nishukuru pia Serikali kwa kukubali baada ya miaka miwili sasa imekubali kutupelekea fedha kwa ajili ya kipande kidogo kile cha kilometa 0.8 kutoka NMB mpaka National Milling. Nimeona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwamba kipande hicho wamekiingiza, nawashukuru sana Wizara ya Ujenzi kwa kutupa faraja na matumaini. Ikumbukwe kwamba hii ni bajeti ya tatu, bajeti zote mbili hatukupata bahati ya kutengewa fedha na ndiyo kipindi hiki tumetengewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa nina concern ndogo kwamba barabara hii ipo kati kati ya mji, lakini inapoanzia pale Magereza mita 100 kuna mto mkubwa ambao masika yote huwa hapapitiki. Nawakumbusha Wizara pale kunatakiwa lijengwe daraja. Kwa hiyo wafahamu hilo kwamba barabara yao hii inayoingia mjini katikati kuna daraja ambalo linatakiwa lijengwe la TANROADS. Daraja lililopo ni dogo sana ambalo linamilikiwa na TARURA na limekuwa likileta athari kubwa kwa wananchi na limekuwa likisababisha ajali kutokana na udogo na daraja lenyewe ni la muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, wiki mbili zilizopita niliuliza swali juu ya barabara hii na majibu ya Serikali yalikuja kwamba tutatengewa kilometa tatu za lami mjini ikiwepo kipande hiki cha kilometa 0.8, lakini kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri sijaona kama hizo kilometa tatu zimeinishwa pale. Kwa hiyo nimuombe Mheshimiwa Waziri kama kulikuwa na kausahaulifu kidogo nikumbushe tu, majibu ya Serikali wiki mbili zilizopita tuliambiwa tutapewa kilometa tatu ambayo kilometa hizi 2.2 ambazo zitakuwa zinatokea TANESCO kuelekea Daraja la Munguri B. Kwa hiyo niombe waingize hiyo kwenye bajeti ili iwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, leo hoja kubwa iliyopo katika Jimbo la Kondoa Mjini ni lile Daraja la Munguri B. Tunaishukuru Serikali ilitutengea shilingi milioni 600 katika bajeti hii tuliyonayo na katika bajeti hii tumeona kuna shilingi milioni 150. Tunaishukuru sana Serikali, lakini Mheshimiwa Mbarawa akumbuke, aliposimama Mheshimiwa Rais pale Bicha, hoja aliyomuuliza ni juu ya daraja hili na akalitolea maelezo. Kwa kweli ujenzi wa daraja hili ni muhimu sana kutokana na uchumi wetu ambao watu wengi wanalima eneo la pili la Mto Bubu, lakini pia tumefungua utalii kwenye Pori letu la Swagaswaga.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunaomba daraja hili walitilie mkazo at least ukifika mwezi wa sita itangazwe tender kama zilivyotangazwa za madaraja mengine ya Mkoa wa Dodoma. Kwa hiyo hili naomba Waziri alichukulie maanani kwa sababu hakuna hoja kubwa zaidi ambayo Mheshimiwa Rais anaweza akauliza sasa hivi katika Jimbo la Kondoa Mjini zaidi ya daraja hili.

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho, TANROADS walipita Barabara ya kutoka Dodoma kwenda Babati ilipita ikamega eneo la Shule ya Msingi Nkuku na kukawa na mazungumzo ya kulipa fidia ili ile shule tuiondoe pale tuipeleke sehemu nyingine. Niombe Wizara kwenye bajeti hii watutengee fedha ili tuiondoe ile Shule ya Nkuku tujenge shule nyingine ya msingi kwa ajili ya kunusuru madhara ambayo yanaweza yakajitokeza kwa sababu ile shule sasa hivi iko barabarani sana. Kwa kweli Wizara ya TAMISEMI wametuletea shilingi milioni 370 za ujenzi wa shule ya msingi mpya. Kwa hiyo nadhani ni kiwango hicho hicho ambacho TANROADS wanapaswa watutengee kwa ajili ya kunusuru maisha ya watoto ambapo shule ile iko barabarani.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema haya nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi na naunga mkono hoja. (Makofi)