Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Shabani Hamisi Taletale

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza ningependa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa mema yake anayofanyia Nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, nipende kumpongeza Mheshimiwa Waziri kaka yangu pamoja na jopo lake. Huyu Waziri ana kitu ndani yake, atafika mbali. Naona kabisa wakati tunapambana na Barabara yetu ya Bigwa – Kisaki, nilimsumbua akaniita nyumbani kwake, lakini pia akaniita ofisini na jopo la wataalam 20. Nikashangaa mimi mtoto wa Kiluguru hawa wataalam 20 nitaongea nao nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wale wataalam wakaniambia tunakuhakikishia hii barabara tutaipata, njia ni kupata fedha, bado naendelea kusema Mheshimiwa Waziri ana kitu ndani yake, atafika mbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri alisema nitaongea na mama yako na leo nathubutu kusema katika ule Mkoa wa Morogoro katika Wabunge wanaopendwa na Mama Samia, mimi ni number one. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kupata Barabara ya Bigwa – Kisaki, kilometa 73 ambayo haijawahi kutokea, mimi number one. Wamepita Wabunge kibao huko nyuma na wananchi wangu wameniambia usipotuletea Barabara ya Bigwa – Kisaki hurudi hapa. Wameona matangazo ya Mheshimiwa Waziri pale kwamba Juni tunakwenda kusaini ile barabara na mimi nauona mlango wangu wa kubaki Kusini Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kuipongeza hii Wizara na niendelee tena kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutupa Barabara yetu ya Ubena – Zomozi ya kilometa 11. Hii Barabara ya Bigwa – Kisaki inakwenda kufungua mipaka na tunakwenda kukutana na mtani wangu kule Mchengerwa. Nimwombe Mheshimiwa Waziri tumeona matangazo ya Juni, 2023. Naomba specific date kwamba naomba tarehe na mimi nikamuwekee mziki mnene pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikuhakikishie hiyo tarehe ambayo tunakwenda kusaini ule mkataba, nataka Taifa lijue Mama Samia ameweka alama, ameweka mguu mzito pale Kusini Mashariki na sisi tunakwenda kuonekana, tunakwenda kutoka kwenye matatizo. Ile Barabara, leo hii Dar es Salaam wanakula matunda yanatoka Morogoro Vijijini, Iringa wanakula matunda yanatoka Morogoro Vijijini. Hata hapa Dodoma wanakula matunda yanatoka Morogoro Vijijini. Ukizungumzia Bigwa – Kisaki leo hii unazungumzia wauza juice wengi wa pale Dar es Salaam. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, hii Juni, 2023 tunaomba tujue specific date ili na nimwandalie muziki mnene asubuhi pale na kuandaa watu wampokee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikuhakikishie, hii Wizara ina watu ambao naendelea kuwaambia watafika mbali. Kaka yangu Kadogosa ana kitu ndani yake, atafika mbali. Mkurugenzi wa Shirika la Ndege, ndugu yangu ana kitu ndani yake, atafika mbali; lakini mtu mzito kabisa kaka yangu, bosi wa TBA, huyu ana kitu hasa ndani yake, atafika mbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, sina mbambamba nyingi. Namkaribisha Mheshimiwa Waziri Kusini Mashariki, tuzindue barabara yetu, tusaini mkataba wetu. Ahsante sana. (Makofi)