Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Tecla Mohamedi Ungele

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Namshukuru Mungu kwa nafasi hii na pumzi ya uhai. Natoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi anayofanya ya ujenzi na huduma zingine katika jamii yetu na hasa Mkoa wa Lindi. Pongezi nyingi pia zimuendee Mheshimiwa Wizara, Mheshimiwa Naibu Mawaziri na watendaji wote wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kazi kubwa wanazofanya nzuri kona zote za nchi hii ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na sisi Wanalindi tunapongeza na tunamshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi inayofanyika ya ujenzi wa barabara kutoka Nanganga kwenda Ruangwa na hatimaye itaenda mpaka Nachingwea; kwa kweli tunashukuru sana. Tunaona sasa hivi nuru ipo ya Mkoa wa Lindi kuunganisha kwenda Mkoa wa Mtwara kwa lami, tunashukuru sana, ilikuwa adha ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na tunaona ukurasa wa 11 katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri tunaona kuna huu utaratibu wa EPC + Financing, tumeona utaratibu wa Barabara ya Masasi – Nachingwea kwenda Liwale unaenda kufanyika, zile kilometa 175 tunaenda kuziona kwa kutumia lami. Ahsante sana tunashukuru sana Wananachingwea, Wanaruangwa, Wanaliwale, Wanamasasi na Mkoa wa Lindi kwa ujumla. Barabara hii ilikuwa kweye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 ukurasa wa 75. Sasa Wanalindi wanashukuru inaenda kutekelezwa, ushauri wangu katika ujenzi wa barabara hii, wakandarasi watakapofika kwa utayari wa kujenga barabara ile, ninaomba, kwa kuwa Nachingwea ni katikati, ni center, basi watakapokuja na mitambo yao waielekeze mingine ielekee barabara ya kwenda Masasi. Ifanye kazi kuelekea Masasi na mitambo mingine ielekee Liwale, ifanye kazi kuelekea Liwale ili kazi hii ifanyike kwa wakati mmoja. Watafurahi sana watu wale, wananchi wa Nachingwea na kwingineko kote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hilo pia kwa habari ya viwanja vya ndege. Tunaona Uwanja wa Ndege Nachingwea na Uwanja wa Ndege wa Lindi, imeelekezwa sana, tunaendelea kuomba sana, tunaomba viwanja vile viwekwe lami ili viwanja vile vitumike wakati wote wa masika na wakati wa kiangazi. Kwa sababu sasa hivi Lindi kunakuja LNG, lakini pia Nachingwea viwanja vile vinatumika pia kusafirisha hata viongozi wa kitaifa. Tukiacha hata uchumi unaoenda kuongezeka kwenye maeneo yetu, tunaomba Waziri muangalie sana Viwanja wa Nachingwea na Lindi kwa upande wa lami. Lakini pia Mbunge wa Nachingwea alishasema wale waliopisha maeneo yao kwa ajili ya upanuzi wa viwanja vile basi walipwe fidia yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakumbushia Barabara ya Kibiti – Lindi ina lami tayari lakini kuna maeneo Mheshimiwa Waziri korofi. Kwa mfano kuna mahali panaitwa Muhoro, wameweka pale viraka viraka ambavyo ni shida, ajali zinatokea mara kwa mara, lakini kuna maeneo kutoka Somanga kuja Nangurukuru napo kuna changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaona kuna eneo linaitwa Kiranjeranje, lakini pia kuna eneo kuanzia pale Kirangara kwenda karibu na Mchinga kwenye ile njia panda ya kwenda Moka, nako pale barabara imeonyesha kuzama kuzama na kuinuka, kuzama na kuinuka. Kama driver akiwa ni mgeni maeneo yale au ameenda kwa speed pale kuna kutokea ajali mara kwa mara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tusingependa wananchi wapate ajali, tusingependa watu wawe navilema vya kudumu na tusingependa vifo vitokee. Tunaomba marekebisho hayo yafanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kutuangalia Wananachingwea, kutuangalia Wanalindi, sasa hivi tunaenda kufunguka kuwa na mawasiliano na mikoa mingine kupitia lami. Hicho ni kilio cha muda mrefu, kulikuwa na vumbi, kulikuwa na hofu, kulikuwa na mahangaiko. Ukishafika Masasi ukiwa kwenye basi utasikia wanasema, enhee, sasa tunaenda Tanganyika, tunaenda kutanganyika sasa. Kwani hakuna viongozi? Haya nayasema kwa sababu anayesifia mvua imemnyeshea. Nimeshasafiri kwenye mabasi hayo mara kwa mara, nafahamu hali ilivyokuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli sasa hivi sisi Wanalindi tunasema tuna imani na barabara hizi kwamba zinaenda kujengwa. Tuna imani kabisa kwa sababu hata vitabu vinasema kwenye Waebrania 11:1: “Imani ni kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo, bayana ya mambo yasiyoonekana.”

Mheshimiwa Spika, sisi Wanalindi tuna imani sasa hivi kama ile barabara ya lami kutoka Masasi - Nachingwea – Liwale tumeipokea hivi tayari ni kama vile tunapita. Tunaamini hilo Mheshimiwa Waziri ataenda kutekeleza, barabara itajengwa na Wanalindi watafarijika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)