Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Agnes Mathew Marwa

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuongea katika Wizara hii. Kwanza nimpongeze sana Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anazozifanya. Mama alituambia hakuna kitakacholala na kweli tunaona hakuna kinacholala kila kitu kinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, na Wizara nzima kwa ujumla kwa kazi nzuri wnayoifanya. Sisi wananchama au watu wako tunasema piga kazi, chapa kazi, mama amekuamini na Watanzania tunakuamini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi niende moja kwa moja kwa kusema namshukuru Mheshimiwa Rais kwa miradi mingi mizuri aliyoileta Mkoa wa Mara, lakini pesa nyingi tulizozipata Mkoa wa Mara kwa ajili ya maendeleo ya Mkoa wetu. Kipekee zaidi niombe kiwanja cha ndege cha Musoma kinachoendelea kujengwa.

Mheshimiwa Spika, ni kweli Mheshimiwa Rais ametoa pesa nyingi, lakini hadi sasa kinachoendelea ni kwamba mpaka dakika hii kuna watu ambao bado wanadai fidia zao. Basi nikuombe Mheshimiwa Waziri ujitahidi watu hawa wapate fidia zao ili na wao wafanye mambo yao mengine kwa sababu mpaka sasa mambo yao mengi yamesimama. Kwa hiyo, uchumi kidogo unakuwa unasuasua.

Mheshimiwa Spika, lakini mimi niombe pia kutokana na hali halisi ya Mkoa wa Mara ndio Mkoa uliomtoa Mwasisi wa Taifa hili Mwalimu Julius Kambarage Nyerere basi ni mkoa ambao pia unapaswa kupata upendeleo.

Mheshimiwa Spika, kuna barabara hii inayotoka Majita - Musoma – Busekela ambayo imekwishajengwa kilometa tano tu na bado kilometa 87. Kilometa hizi zilizobaki ni nyingi sana na ukizingatia tangu Uhuru wa Taifa hili Wilaya ya Musoma Vijijini walikuwa hawajawahi kuiona lami. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, mimi nikuombe sana utuangalie kipekee Mkoa wa Mara na barabara hii ya Majita. Pia ukizingatia mimi mtoto wa Chifu Hangaya naishi huko Majita, kwa hiyo, inakuwa ni ngumu kidogo kwenda mpaka kule kwa sababu inakuwa ni ngumu kufika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kipkee nimpongeze Meneja Waheshimiwa Wabunge, TANROADS Mkoa wa Mara kwa kazi nzuri anayoifanya. Kwa kweli ni mchapakazi, anafanya kazi vizuri na mimi mwenyewe ni shahidi. Kuna daraja ambalo lilikuwa limeharibika muda si mrefu sana ambalo linaunganisha Musoma mpaka Mwanza, Daraja la Nyamika A pale Sabasaba. Mimi nilipita pale usiku nikamshuhudia Meneja amesimama wakati kazi zikiwa zinaendelea. Basi tukiwapata viongozi wa hivi basi naamini Taifa letu litaendelea mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kipekee mimi pia niongelee kuhusu uwekezaji; uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam ni muhimu sana kwa Taifa la Tanzania, lakini pia utaongeza ajira kwa Watanzania na kuongeza kipato katika Taifa hili. Ninamuamini sana Mheshimiwa Rais kwa kazi anazozifanya na ndio maana anakwenda kutafuta mahusiano nchi za nje kila kukicha. Mama halali asubuhi, mchana na usiku, anafanya kazi twenty-four-seven, yeye halali wala hapumziki kwa ajili yetu, anakwenda kututafutia wawekezaji. Naamini kabisa mama hawezi kwenda kututupa shimoni, mama ni mlezi, kwa hiyo, uwekezaji huu wa bandari mimi nina amini kabisa ni uwekezaji salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi niwaombe tu hata wale waliokuwa Mawaziri kipindi hicho wanapobeza inakuwa sio jambo zuri, hata wao wakati huo walipokuwa Mawaziri na wao walikuwa wanafanya kazi kwa kipindi hicho. Kwa hiyo, kwa kipindi hiki wawaache Mawaziri walioko madarakani wafanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili suala linatukera sana, unamkuta mtu alikuwa Waziri kipindi chake na yeye mwenyewe wakati akiwa Waziri hakufanya vizuri, lakini sasa hivi kwa sababu sio Waziri anaona wenzake wanafanya kazi anawazongazonga. Hawa ni wateule wa Mheshimiwa Rais, wawaache wafanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi binafsi kama Mbunge kilichoniuma sana, kuna Mbunge mwenzetu huku ndani ambaye kipindi hicjho alikuwa Waziri, muda wote kazi kusema sema wenzake. Mara Mwigulu ajiuzulu, Mwigulu ana makosa gani amemfanyia nini; lakini Wizara hii sio ya Mwigulu. Kwa hiyo, ni kitendo ambacho kinatuudhi sana mtu kwenda kwenye mitandao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini mimi niseme tu tunamtia moyo Mheshimiwa Waziri Mbarawa, afanye kazi uwekezaji huu ni mzuri sana. Hata sisi tulikwenda kujifunza katika Bandari hii ya Jebel Ali ambayo ni katika hii Kampuni ya DP World. Hii kampuni sisi kama Wabunge tuliangalia vitu vingi, tuliona kwa kweli ufanyaji kazi wao ni mzuri, wana vifaa vya kisasa na wako vizuri kabisa, lakini kama Wabunge tumejiridhisha. Mimi nilimuuliza Mheshimiwa Waziri, inakuwaje katika uwekezaji huu mbona Watanzania wanalalamika? Mheshimiwa Waziri, akatuelewesha kwamba Watanzania wataendelea kufanya kazi kama kawaida na wawekezaji wataendelea kuwkeza, lakini wameweka mikataba mizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais, hawezi kututupa shimoni. Mimi niwaombe ndugu zangu tumwamini Mheshimiwa Rais, kwa manufaa ya bandari yetu imesuasua kwa muda mrefu. Tukipata wawekezaji wazuri, lakini tukaweka mikataba mizuri inayotusaidia sisi ama kutu-support sisi kama Watanzania, mimi ninaamini kabisa ndio mikataba tunayoihitaji na ndizo kazi ambazo tunazihitaji sisi zifanywe na Mawaziri za kutafuta wawekezaji wazuri. Kwa hiyo, ndugu zangu Watanzania kuweni na imani na Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa sababu yeye ni mama, yeye ni mzazi, tena mkae mkijua na mnajua mimi naamini kwamba mwanamke ni mwaminifu kuliko mtu yeyote duniani kwa sababu yeye ni mzazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)