Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Nashon William Bidyanguze

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Nami naomba niungane na Wabunge wenzangu kumpongeza Rais wetu, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoendelea kufanya katika Taifa letu. Pia naomba nimpongeze Waziri, amesoma bajeti yake vizuri, pia wanaomsaidia kwa maana ya Naibu Mawaziri, wanachapa kazi vizuri. Nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niende moja kwa moja kwenye eneo moja la Bandari ya Lagosa na Sibwesa. Mheshimiwa Waziri, hizi bandari zilitengewa fedha na zilishajengwa kwa kiasi kikubwa tu, bado kidogo kumalizia. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, peleka fedha katika eneo la Lagosa na Sibwesa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mbaya zaidi, pamoja na kwamba tunahitaji bandari hizi zianze kufanya kazi pamoja na kwamba meli hazijakamilika, lakini wananchi wa maeneo yale, wanawadai wakandarasi fedha nyingi sana. Yaani watu wamefilisika, watu waliamini kwamba watalipwa lakini baada ya Serikali kusitisha kupeleka fedha pale kwenye zile bandari, wananchi wanapata shida sana. Nakumbuka juzi kwenye semina niliwahi kuongea jambo hili na majibu niliyopata ni kwamba fedha tayari Mkandarasi wa Lagosa ameshapata na kwa hilo naomba nikushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo naomba nilete shukurani ni kwenye daraja la Malagarasi Chini. Ni kweli fedha ilikwenda kwa ajili ya upembuzi yakinifu na kwa sasa hivi taarifa ya Serikali ni kwamba mwezi Novemba Mkandarasi yule atamaliza kazi. Naomba sana amalize kazi mapema iwezekanavyo ili tuanze kuweka mchakato wa kuona namna ya kwenda kujenga hilo daraja kwa sababu ni kiunganishi kikubwa.

Mheshimiwa Spika, sisi Mkoa wa Kigoma tuko pembezoni na ile barabara ni kubwa ambayo inaweza kututoa kwenye Mkoa mwingine wa Katavi na Mkoa wa Sumbawanga pia. Sasa unaweza kuona kabisa kwamba barabara ile ni muhimu sana na hasa hilo daraja. Viel vile, kwenye barabara hiyo hiyo ambayo ni barabara ya Nsimbo – Kalya, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri, inaendelea kutengewa fedha mara kwa mara, na inasimamiwa vizuri sana na Meneja wa TANROAD ambaye anaendelea kuisimamia na kwa kweli inapitika. Nashukuru sana kwa jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia kwenye barabara ya Kalya - Sibwesa, Mheshimiwa Waziri barabara ya Kalya - Sibwesa ni barabara ambayo inakwenda bandarini kwenye hiyo bandari ambayo nimesema ya Sibwesa. Naomba sana, uliweka fedha kwa ajili ya kuifungua na mimi kwenye Mfuko wa Jimbo ile milioni 500 aliyotupatia Mheshimiwa Rais, nikaweka pale, TARURA wakaenda pale kujenga madaraja pamoja na fedha za TANROADS, barabara ile imekwishafunguka, lakini bahati mbaya bado haijakamilika. Naomba sana unapoendelea kujenga na kukamilisha bandari hiyo ya Sibwesa na hii barabara ni vizuri uiwekee fedha ili iweze kukamilika.

Mheshimiwa Spika, lakini pia iko barabara hii kubwa ambayo inotoka Tabora. Sisi kipande cha Mpeta – Uvinza ni kilometa 51. Naishukuru Serikali, Mheshimiwa Waziri uliweka fedha na mkandarasi yuko kazini lakini anasuasua, tatizo ni nini? Mheshimiwa Waziri hebu nenda uone inawezekana vifaa ni vichache, lakini inawezekana fedha pia hapati vizuri. Naomba sana kwenye jambo hili kwa sababu kwenye kipindi hiki cha mvua wananchi wamepata shida sana. Kwa sababu diversion anazotengeneza haziko imara, magari yalikuwa yanakwama sana, nakuomba sana na bado wana umbali mrefu sana, kwa kweli jambo hili naomba nipongeze, lakini naomba nisistize kipande kile kiweze kutengenezwa kwa haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwa barabara ya Katavi – Uvinza – Kasulu, barabara hii sijasikia imezungumziwa kabisa. Hii yote ni kufungua Mkoa wa Kigoma. Naomba utakapokuja ku–wind up hili jambo kwa kweli ulizungumze kabisa. Hakuna haja ya mtu wa Kigoma kupita Tabora wakati anakwenda kwa Mheshimiwa Tulia pale Mbeya, njia yetu ndiyo hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia kwenye habari ya meli; nakushukuru umetoa habari nzuri hapa Bungeni kwamba kuanzia mwezi wa sita ambayo ni kesho kutwa tu, mkandarasi anaanza kukarabati Meli ya Mv Liemba. Huo ndio ukombozi wa sisi watu wa Kigoma, yaani Kigoma, Katavi na Sumbawanga ukweli ni kwamba ziwa lile limetufanya tuwe karibu na nchi tatu kwa maana ya Congo, Zambia na Burundi. Sasa nchi zile tunabaki tunaziangalia tu kwa sababu hatuna usafiri wa kwenda kule. Pia ninataka nikwambie Mheshimiwa Waziri, meli zile ndizo zimekuwa zinasababisha kupata uchumi kwenye Mkoa wa Kigoma na uchumi wa mtu mmoja mmoja kwa wananchi wetu wa Kigoma, kwa hiyo ni jambo la msingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia kwenye eneo lile la utengenezaji wa meli mpya na mimi niungane na wenzangu, meli kubwa sana nadhani itakuwa haiwezi kusaidia, kwa sababu mizigo sio mingi ni mizigo kidogo kidogo. Kwa hiyo, kwa meli ile ambayo inaweza kuwa na tani 2000 tukipata hata meli mbili za tani 1000 kila meli ni jambo jema sana. Itakuwa inakwenda-inarudi haraka haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nizungumzie kwenye uwanja wa ndege wa Kigoma; Mheshimiwa Mbarawa wewe ulikuja Kigoma, sisi Wabunge tulikuwepo, ulisaini mkataba mbele yetu tuliona, tulitaka tuone kazi inafanyika tusiishie kuona mkataba peke yake, wananchi wasije wakafika mahali wakachoka. Kwa kweli nataka nikwambie, Mheshimiwa Rais wetu wananchi wa Kigoma wanampenda sana na wanamwamini sana kama sisi Wabunge tunavyompenda na kama tunavyomwamini. Kwa kweli kwenye majimbo yetu hali ni nzuri na haijapata kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miradi ya maji, barabara za TARURA yaani huwezi kuamini mimi kule kwenye jimbo langu hata huko bondeni kwenye ziwa barabara zimefika, kitu ambacho kilikuwa hakijawahi kutokea wananchi wanashangaa. (Makofi)

Kwa hiyo, mimi nilikuwa naomba nikupongeze na niseme hayo machache lakini pia nikutie moyo, pambana na fanya kazi vikwazo ni vingi lakini mimi ninaamini Mheshimiwa Mbarawa utashinda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa Nashon wakati unataja zile barabara, ile ya kutoka Uvinza inayounganisha Katavi ndiyo hiyo umeitaja au hiyo haipo?

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, hiyo ni nyingine. Hiyo ya Katavi ni nyingine, hii nyingine inaitwa Simbo- Kalya.