Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Antipas Zeno Mgungusi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Malinyi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi kuwa mtu wa nne kuchangia jioni ya leo kwenye Wizara hii ambayo nina interest nayo kubwa sana kama mtu wa Malinyi na bonde la Kilombero hasa kutokana na changamoto ya Barabara. Nina masuala kadhaa hapa ya kuchangia yale ya jimboni kwa maana ya barabara yetu ya kwenda Songea kuunganisha Mkoa wa Morogoro na Ruvuma na pia kuna kipande cha kuunganisha Wilaya ya Malinyi na Kilombero kwa maana ya Mlimba kupitia kivuko. Vile vile kwa masuala ya kitaifa, kuna hili sakata la bandari ambalo linasemwa semwa, nami nitasema kidogo. Pia kuna suala la uchumi wa masaa 24, kwa maana ya kutamani kuona usafiri wa mabasi yanakesha hapa nchini na mwisho, kuhusu mabasi madogo (Costa Mini Buses) kutoa huduma kubwa kabisa kama mabasi makubwa.

Mheshimiwa Spika, nitoe shukrani zangu kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maana ametuheshimisha watu wa Malinyi na watu wa bonde la Kilombero wote. Imekuwa historia tangu dunia imeumbwa, sisi hatukuwahi kuwa na lami. Leo hii ukijadili Wilaya ya Malinyi, ni mara tano, yaani uchukue Mkoa wa Dar es Salaam wote uuzidishe mara tano au mara sita ndiyo unakutana na Malinyi moja na hatuna lami hata kilometa mbili. Kwa hiyo, hata watoto wanaozaliwa kule, lami ni mpaka uende Morogoro Mjini.

Mheshimiwa Spika, kwenye Kampeni tumesema sana tutakwenda kufanya jambo la lami kuunganisha Morogoro na Ruvuma kwa maana ya kupita Ifakara, Malinyi na kutokea Namtumbo kule, watu wanasema hii siasa ni uongo uongo, miaka yote mbona inasemwa? Litawezekanaje jambo hili? Hata mimi nilikuwa nazungumza, kwenye kampeni tumeahidi na nimeendelea kuwaambia Wana-Malinyi tutafanya, huku kimoyomoyo kidogo moyo unadunda, unaogopa, unasema hawa jamaa (Serikali) watasaidia kweli? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Rais amekwenda kunitoa hofu, amekwenda akuwafurahisha Wana-Malinyi, tunakwenda kusaini mkataba mwezi ujao kwa huu mtindo wa EPC+ F kwa maana ya kuunganisha Mkoa wa Morogoro na Ruvuma, Malinyi inakwenda kuwa na lami. Pia kipande cha kutoka Ifakara kwenda Ulanga - Mahenge inakwenda kuwa na lami, ni sehemu ya mradi huu mmoja. Kwa hiyo, namshukuru sana Mheshimiwa Rais na zaidi wasaidizi wake.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

TAARIFA

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nampa taarifa mzungumzaji, katika Mkoa wa Morogoro, kwa muda mrefu ilikuwa kilio cha Mkoa mzima wa Morogoro. Mkoa huu tangu tupate uhuru haukuunganishwa na Mkoa wa Ruvuma kama anavyosema mzungumzaji, siyo tu Mkoa tu wa Ruvuma, bali sasa historia inakwenda kuandikwa. Mlimba inakwenda pia kuunganishwa na Njombe. Kwa hiyo, Mkoa huu kwa mwaka huu wa fedha unakwenda kuunganishwa na Mikoa yote miwili, Ruvuma na Njombe kwa upande wa Mlimba na Malinyi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Kicheko/Makofi)

SPIKA: Waheshimiwa niwakumbushe tu kwamba muda wa taarifa ni muda wa anayekuwa anazungumza. Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa, lakini naomba unisaidie hata dakika moja ya nyongeza muda wangu ukiisha. (Kicheko)

SPIKA: Hapana. Muda huu ninaotumia sasa hivi ni wa kwangu, kwa hiyo huu unalindwa. Kwa sababu nikiwakumbusha kila wakati, mnaona kama kiti kinawabana. Kwa hiyo, taarifa muwe mnaambiana wenyewe huko. Mkishakubaliana ninyi, mimi sina hiana hapa mbele. Kanuni zinawaruhusu kabisa. Mheshimiwa Mgungusi.

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwenye jambo hilo hilo, tunafahamu, nadhani mmekuwa mkiona hata kwenye taarifa ya Habari kila masika watu wa Malinyi tumekuwa tukilia mabasi yanakwama, Malinyi hapaingiliki wala hapatokeki. Hata juzi imetokea hivyo, lakini kwa mara ya kwanza kabisa hili jambo naamini linakwenda kuisha.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, kipindi hiki wakati tunasubiri hili jambo litokee barabara ianze kujengwa mwaka huu, basi ukarabati ambao unaenda kufanyika na watu wa TANROAD ufanyike kwa ubora ambao unapaswa. Sehemu kubwa ya maeneo ya barabara ambapo tunakwama ni matope ambayo wakandarasi huwa wanaleta wakati wa kiangazi, wanakarabati barabara inaonekana safi, ikija mvua tunapata shida kubwa. Kwa hiyo, niseme tu Mheshimiwa Waziri wasiliana na watu wako wa TANROAD, ingawaje wananipa ushirikiano mkubwa sana, wakandarasi awamu hii wasilete tope, wakati wa kiangazi kukarabati vije vifusi vya changarawe au mawe.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, ilikuwa ahadi yetu ya Chama cha Mapinduzi, naimi kama Mgombea wao wa Ubunge kuunganisha Wilaya ya Ulanga na Wilaya ya Malinyi kupitia kivuko pale Kikove kwa maana ya Kijiji cha Lupunga na Ngalimila kule Mlimba. Kwa mara ya kwanza mwaka huu inapaswa twende kuunganika, tutakuwa na kivuko. Ile pantoni itakuwa pale inaunganisha watu wa Malinyi, maana yake hata watu wa Njombe watakuwa wanapita pale kwa mwaka huu. Jambo hili linaonekana kama ni ndoto, lakini linaenda kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ila changamoto ni kwamba Mkandarasi ambaye yuko site hebu saidia kumkimbiza kimbiza. Mimi sitaki kugombana na wewe, ni mtu mzuri, umenipa ushirikiano mkubwa, nachoka kufuatilia mkandarasi mmoja mmoja. Kwa hiyo, naomba hili jambo ulichukue waweze kuharakisha kuhakikisha kwamba lile gati linakamilika kwa wakati tuweze kupitisha watu wa Malinyi na Mlimba kuungana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye masuala ya Kitaifa, kuna suala hili la bandari ambalo linazungumzwa; maboresho au kubinafsisha ile shughuli ya operation, menejimenti. Mimi binafsi kama mpenda maendeleo, naunga mkono jambo lifanyike kwa sababu kadhaa kubwa. Naamini ni vema mtumishi wa Umma ukawa mbunifu, ukabuni vitu vya kufanya kuhakikisha kwamba huduma zinakwenda vizuri na mapato yanaongezeka kuliko kutofanya lolote kabisa. Kwa hiyo, kubaki kama tulivyo kama bandari siyo jambo ninalotamani kuliona au kurudi nyuma tulikotoka, siyo jambo ninalotamani kuliona. Natamani tusogee, lakini ninaamini kwenye majaribio ya nia njema inaweza kutokea tukakosea mbeleni, bora likazungumzika tukifanya makosa mbeleni kuliko kutofanya mabadiliko kabisa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kimsingi nawatia moyo wale wanaofanya, watu wa Wizara endeleeni kusaidia. Matamanio yangu ni kwamba, hata TANESCO na taasisi nyingine za maji, sijui RUWASA na kadhalika ikibidi kupata private sector siku za mbeleni ikitufikirisha tufanye. Tunafahamu utendaji wa Serikali kidogo sehemu kubwa watumishi hawako serious sana, lakini private sector naamini inaweza ikafanya vizuri. Kwa hiyo, jambo hili naliunga mkono ila tu zile hofu za watu zijibiwe. Wengine wanasema kuna masuala ya usalama, wengine mapato yatakuwaje? Ajira za ndugu zetu zitakuwaje? Wale wanaohusika na Wizara wazijibu kuwatoa watu hofu, lakini ni jambo jema, mimi naunga mkono liendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu uchumi wa masaa 24, mnafahamu dunia nzima tunazunguka, watu wanakesha, mabasi yanakesha, sisi kwa nini tulale? Mnaona yale magari madogo ya IT yanaenda nje ya nchi, mnaona magari ya magazeti yanagombaniwa Dar es Salaam kila mahali kusafirisha watu usiku, kwa nini? Uhitaji ni mkubwa sana kusafiri usiku. Kwa nini sisi tulale? Wenzetu wa LATRA tunagombana nao, lakini najua wao wanasimamia sheria au maelekezo ya wakubwa kwa maana ya Wizara. Wizara ikiwaambia vinginevyo, watatekeleza kama wanavyoambiwa, hawawezi kujiamulia wenyewe. Naomba niishawaishi Wizara turidhie.

Mheshimiwa Spika, umekuwa ukilisemea sana hili. Hili jambo ni la kwako, umelisema muda mrefu, na sasa mabasi nafikiri yanaanza kuanzia saa tisa usiku. Kama unakubali saa tisa mabasi yaanze, kwa nini yasianze saa saba? Kwa nini yasianze saa mbili usiku? Kuna shida gani? Madereva ni wale wale. Kwa hiyo, naomba sana hili jambo Waziri wakati ana-wind up alisemee, atoe maelekezo, kwa sababu hata zuio la kusafiri usiku halikuwa kisheria. Tumefanya tu mazoea. Sisi tangu tukiwa wadogo kuna mabasi yalishatekwa, wakasema tusisafiri usiku. Sasa kama tunaogopa kusafiri usiku kuogopa majambazi, maana yake tunawapa umaarufu majambazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna Polisi, majeshi na kila kitu, tunaogopa majambazi kusafiri usiku, kwa nini? Kwa hiyo, hatutakiwi kuwapa wahalifu umaarufu mwepesi. Serikali inaweza kufanya, tutoe tamko, watu wasafiri masaa 24. Hamna suala la kusikilizia kusema tuanze kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho, kuhusu mabasi madogo, kwa maana ya minibuses na Costa haziruhusiwi kupewa route rasmi kupeleka watu mikoani, lakini mabasi makubwa yanafanya. Mabasi makubwa hayana uwezo wa kumaliza watu wote. Nadhani mnafahamu barabarani, wote tunapenda kudandia magari ya kuunga. Kwa nini Costa hazipewi vibali au kufunguliwa zipate route kama mabasi makubwa? Wanafanya kama special hire; ukiwa na msiba unakodisha; ukiwa na shughuli za Kwaya, watu wanaenda wanakodisha. Kwa nini wasipewe route rasmi?

Mheshimiwa Spika, watu wakifariki, familiwa wanaruhusiwa kusafirisha msiba na kutumia Costa usiku, lakini mfanyabiashara akitumia Costa kupeleka hizo dawa ili watu wasife anaambiwa sheria hairuhusu, lakini wakifariki watu wake, anaruhusiwa kusafirisha. Haileti maana katika hali ya kawaida. Kwa hiyo, naomba kushawishi, naomba Bunge lako liridhie, kama Waziri akihitimisha lazima tusafiri masaa 24 na Costa ziweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, watu wa LATRA wanasema, sheria inataka basi angalau liwe na watu 40 ndiyo linaweza kusajiliwa kupewa route. Sasa mbona taxi ina watu wanne, lakini inasafirisha mtu Dar es Salaam mpaka Mwanza? Idadi ya watu inahusianaje? Hai-make sense. Kwa hiyo, naomba kuwafikirisha ndugu zangu, tusiwe na mawazo mgando, tubadilike. Basi linabeba watu 65 linapeleka Mwanza, taxi watu wanne inapeleka Mwanza, kwa nini coster yenye watu 29 au 39 haitakiwi kubeba mtu mpaka itimie 40? Mantiki ni nini kuhusu idadi ya watu? Suala security nafahamu tuna vyombo vyetu, vifanye kazi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la barabara kama siyo salama, TANROADS na mamlaka nyingine zifanye kazi zao. Sasa muda mwingine watu wa Serikali huwa wanaamua tu kuwaza kidogo halafu jambo tunalimeza wote, Mawaziri nao wanalichukua linakuwa jambo la kitaifa, lakini hai-make sense. Kwa hiyo, naomba nishawishi Bunge lako liridhie kama watu wa Serikali wataleta kama ni sheria, tuko ladhi kuunga mkono ibadilishwe lakini watu wakeshe barabarani. Tunalala ili itokee nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa leo, lakini nasisitiza kwamba namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa barabara yetu ya Malinyi kutokea Songea.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)