Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Tauhida Cassian Gallos Nyimbo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Mawaziri wake kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kujenga Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina mambo mawili ambayo naweza kuyachangia kwa siku ya leo. Ninampongeza Waziri pamoja na wafanyakazi wote kwa kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Spika, suala la bandari ni suala ambalo kila ninaposimama huwa nawasemea wanawake wa Tanzania. Kwangu kumekuwa na kero kubwa na bado haijapatiwa ufumbuzi. Baada ya kuwa kila nikisimama nikiwa miongoni mwa wanaolalamika na suala la bandari na mimi nikiwa miongoni mwao, sasa nimetoka kwenye kulalamika nimeamua kwa maksudi kwenda kuangalia hasa tatizo lililoko huko bandarini ni nini.

Mheshimiwa Spika, kwa kufahamu kwa undani kabisa bandari kila siku tumekuwa tukitupia lawama kwa Waziri, lakini kuna matatizo ambayo yanasababishwa pia kutoka kwenye Wizara nyingine. Kero kubwa iliyopo ndani ya bandari inasababishwa na TRA. Pia wanaosababisha kero wapo Askari Polisi na Bandari wenyewe.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeamua kwa maksudi kwenda kujua haya matatizo tunayolalamikia kila siku bandari yanasababishwa na nini? Tulikuwa mwanzoni hatufahamu tunayemlalamikia hasa ni nani, lakini nimuombe Waziri mzigo mkubwa bandari unaubeba wewe na unaubeba wewe kwa sababu wewe ndiyo kioo cha bandari, wewe ndiyo mhusika wa bandari, lakini una watu kiungo ambao wanafanya kazi na wewe.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri nitumie fursa hii sasa kukushauri upate fursa ya kukutana na Mawaziri wenzio wanaohusika na masuala ya kodi, Mheshimiwa Waziri wa Fedha lazima ukae naye upate muafaka wa kwenye suala la bandari kodi zinazotozwa kwa wanawake wajasiriamali wadogo wadogo.

Mheshimiwa Spika, haiingii akilini kila tunaposimama hapa tunapigia kelele wanawake wafanyabiashara ndogo ndogo. Kwa nini tunazungumza wakati huu wa bandari, kwa sababu shida anayoipata mwanamke wa Kitanzania awe anatoka Zanzibar au Bara anaipatia bandarini anapopita na mzigo wake mdogo. Tukuombe ukae na Waziri mwenzio muone mnatatuaje matatizo yaliyopo katika maeneo ya bandari.

Mheshimiwa Spika, pale kuna Askari pia, lakini anapofika pale anakuwepo ndani ya bandari, ninadhani lazima mpate muda wa kufanya kazi kwa pamoja, Mawaziri wapo ambao mnaweza mkakaa mkazungumza na mkatatua changamoto zinazokuwepo pale.

Mheshimiwa Spika, pale ndani ya bandari napazungumza kuna mambo mengi na kuna watu wengi. Tumekuwa muda mwingi tukishauri lakini tunalalamika. Niseme kwamba kuna mazuri yanayofanyika pale ndani ya bandari. Kuna watu wanatoa huduma vizuri, Waziri tunachukua fursa za kukushauri yale mazuri yaendelee, lakini maeneo ambayo yanahitaji maboresho tukuombe Mheshimiwa Waziri utusaidie kuweza kufanya maboresho ili wanawake na vijana wa Tanzania waweze kufanya mahitaji yao kwa wepesi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nazungumzia bandari kwa sababu kuna mambo mengi yanayoendelea pale, siamini kama yote yanaweza kumfikia, lakini kwa sisi ambao tunaitumia bandari, Mheshimiwa Waziri kilio hiki kwangu kimekuwa cha muda mrefu. Ninaelewa kama siyo la kwako, lakini usipokaa na wahusika matatizo haya hayawezi kuondoka. Tunaomba utusaidie ili matatizo yanayosonga pale bandarini yaondoke.

Mheshimiwa Spika, kuna wanawake wajawazito wanapita bandarini, kuna akina mama wanaougua wanapita bandarini, bado kwenye mifumo ya maeneo hayo Mheshimiwa Waziri hapajakaa vizuri, ninadhani hapajakaa vizuri wewe umeshikilia bandari lakini kuna wengine wanakuja kutoa huduma ndani ya bandari. Hawa watu kila mmoja anafikiria huduma ya mwenzie wakati hajulikani mhusika hasa nani. Tunakuomba Mheshimiwa Waziri ikiwezekana tutengenezee utaratibu kuona tunapata njia ya kupita akina mama wajawazito, watu wenye mahitaji maalum vilevile wale ambao wanakuwepo pale wagonjwa.

Kuna muda tunawashukuru wafanyakazi wanaotoa huduma kwa VIP, huwa wanalazimika kuisaidia jamii japo najua hii kazi wanayoifanya siyo yao. Kwa hiyo, huwa wanasaidia kwenye maeneo ya wagonjwa wajawazito. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, pamoja na kazi nyingi na kubwa unazozifanya na sisi tukizishuhudia kwa macho yetu, bado kilio cha bandari na kero za bandari hazijaondoka moja kwa moja. Tunakuomba Mheshimiwa Waziri, fanya ziara maeneo yale na kuweka mikakati ya makusudi kuweza kulisaidia Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nije kwenye hoja yangu ya pili ambayo ni suala la uwekezaji ndani ya bandari. Mwenyezi Mungu alivyotujalia, kila mmoja amemuumba na karama yake, kila mmoja amemuumba na majaliwa yake. Namwomba Mheshimiwa Waziri, hili jambo analotaka kwenda kulifanya la uwekezaji ndani ya bandari, niseme kweli, kwa namna nilivyojiridhisha, naomba niseme kwamba tunamridhia aende akaendelee nalo kwa utekelezaji. Huwa mgumu sana wa kukubali kitu haraka haraka, lakini kwenye eneo hili nimejiridhisha vya kutosha, uzalendo na utu uliokuwanao, hao wawekezaji wanakuja kuifungua Tanzania, usiache kuweka mbele uzalendo na ubinadamu na utu.

Mheshimiwa Spika, nimejiridhisha kwa kuuliza maswali, nimejiridhisha kwa hoja ambazo zimekuwa zikinisumbua. Nilikuwa najiuliza, tukienda kuwekeza: Je, wazawa wetu wataondolewa? Waziri ameniridhisha kwa majibu kwa kuniambia hapana, wataendelea na kama kuna watu watakuja kufanya kazi wageni ni kwa muda. Kwa suala hili Mheshimiwa Waziri sina namna, lazima niungane nawe kusema bandari sasa ifunguke. Mheshimiwa Waziri, anayesifia mvua maana yake imemnyeshea, tunaelewa na kufahamu matatizo makubwa yaliyokuweko ndani ya bandari yetu. Hatuwezi kung’ang’ania vitu ambavyo hatuna uwezo wa kuvifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme kwamba bandari itakapoenda kufunguka, Tanzania itafungua milango yake zaidi. Bandari itakapofunguka, itaenda kufungua njia na itaongeza ajira. Nimemwuliza Mheshimiwa Waziri kuhusu mapato yetu kama Watanzania, kodi itakuwaje? Jibu lake ni kwamba kodi itaongezeka.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. TAUHIDA C. GALLOS: …Niwe na ugumu gani wa kusema Waziri endelea na suala zima la uwekezaji wa bandari? Mheshimiwa Waziri…

SPIKA: Mheshimiwa kengele ilishagonga, nilikuwa nataka umalizie hoja yako. Sekunde thelathini malizia sentensi.

MHE. TAUHIDA C. GALLOS: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ninaunga mkono hoja, lakini niungane na Mheshimiwa Waziri kwenye suala la uwekezaji wa bandari, ni jambo jema. Mheshimiwa Waziri tanguliza uzalendo mbele, tanguliza ubinadamu mbele.

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)