Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuwa mchangiaji wa kwanza jioni ya leo.

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba leo nimesimama, sitakuwa na mambo mengi zaidi ya kutoa shukrani zangu za dhatii kwa niaba ya wananchi wa Rorya, kwanza kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pili, kwa Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii pamoja na Manaibu wake wawili, hasa Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Engineer Kasekenya. Pia nitoe shukrani zangu za dhati kabisa kwa Watendaji kwa maana ya Makatibu Wakuu wa Wizara hii hasa Dada yangu Ndugu Aisha, pia nitoe pongezi za dhati kabisa kwa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara.

Mheshimiwa Spika, nimeanza kutoa pongezi hizo kwa kipekee kabisa kwa niaba ya wananchi wa Rorya kwa Serikali hii ya Mama Samia kuridhia maombi zaidi ya miaka 40 ya barabara ambayo tumekuwa tukiiomba muda mrefu hapa ya lami kutoka Mika – Utegi – Shirati mpaka Mpakani mwa Kenya Kirongwe kuingizwa kwenye mpango wa bajeti kwa ajili ya ujenzi wa lami.

Mheshimiwa Spika, naomba niwashukuru wananchi wangu na kwa kuwa wananisikia na waliniambia nifikishe salamu na pongezi hizi na shukrani za dhati kabisa kwa sababu barabara hii siyo tu kwamba ni barabara ambayo inatuimarisha usalama kati ya nchi na nchi, lakini ni barabara ambayo ikijengwa kwa kiwango cha lami inakwenda kuinua uchumi wa Halmashauri yenyewe, uchumi wa Mkoa wa Mara, lakini uchumi wa Serikali kwa ujumla kwa sababu inakwenda kugusa nchi mbili.

Mheshimiwa Spika, mbali ya hivyo, hii ni barabara ambayo kimsingi tumeiomba kwa muda mrefu sana. Ilani ya Chama cha Mapinduzi toka mwaka 2010 ilikuwa inasemwa barabara hii itaingizwa kwenye mpango wa utekelezaji lakini ilikuwa haifanyiki, toka 2005, 2010 mpaka leo kwa Awamu hii ya Sita angalau imeweza kuingia kwenye mapendekezo ya ujenzi wa lami.

Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla kwa maana ya Wizara hii, niombe sasa kwa kuwa tayari imekwishaingia kwenye mpango wa utekelezaji wa lami, iweze kutengewa fedha, kwanza itangazwe lakini itengewe fedha ambazo itaweza kujengwa kwa kilometa zote 56. Ninaamini wananchi wamefarijika sana na ndiyo furaha yao kubwa.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili nataka tu nimkumbushe Mheshimiwa Waziri, kama nilivyosema leo mimi sina mambo mengi kwenye Wizara hii, kwa furaha tulizonazo sisi tunaamini kabisa kwamba wananchi wote katika Wizara hii wamefarijika sana. Natamani nimkumbushe Mheshimiwa Waziri juu ya Kivuko cha MV Musoma. Kwa kuwa kivuko hiki kilikwenda kwenye matengenezo, mara nyingi Mheshimiwa Waziri nimekuwa nikikuuliza ndani hapa, kwenye majibu ya nyongeza umekuwa ukitoa ahadi kwamba angalau kile kivuko, mwanzoni ulisema tarehe 30 Aprili kitarejea na kitaanza kutoa huduma.

Mheshimiwa Spika, siyo hivyo tu, Kiongozi kwa maana ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama, Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi Taifa, naye alipokuwa katika eneo lile alikupigia simu ukaahidi kile kivuko kitarudi kabla ya tarehe 05 Aprili. Leo ni tarehe
23 Mei, Mheshimiwa Waziri ninatamani wakati unafanya majumuisho, wale wananchi wanaotumia kivuko kile wangetamani wapate kauli yako, ni lini kile kivuko kinarudi kwa ajili ya kutoa huduma kwa kuwa kile kivuko kilichopo ni kidogo na siyo salama kwa maisha yao.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ambalo ninatamani pia nikukumbushe ni juu ya bandari ya Musoma. Nimeona kwenye hotuba yako Mheshimiwa Waziri, zipo bandari kadhaa ambazo zinakwenda kufanyiwa matengenezo, bandari za Mwanza na maeneo mengine, lakini sijaiona bandari ya Musoma ikitajwa.

Mheshimiwa Spika, nilichangia mwaka jana kwenye hotuba ya bajeti ya Wizara yako na nikakuomba sana kwa unyenyekevu mkubwa, bandari ile sisi kwetu ndiyo kiungo muhimu cha kuinua uchumi wa Mkoa wa Mara. Nasi Mheshimiwa Waziri wewe ni shahidi, ile bandari imesahaulika kabisa. Kwa sasa ilivyo imechakaa na haifai. Ninaomba sana kwenye bajeti hii, pamoja na kwamba tayari mmetaja bajeti zingine, muone namna ya kuifufua ile bandari.

Mheshimiwa Spika, kwetu ile bandari ndiyo kiungo muhimu cha kuinua uchumi wa Mkoa ule wa Mara. Lakini sisi tunaitegemea ile bandari iweze kufanya kazi, kwa sababu tunayo bandari ya Sota eneo la Rorya ndiyo muunganiko wa bandari zote mbili. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri kwenye bajeti na utekelezaji kwenye hotuba yako umesema hapa tunajenga Reli ya SGR, matarajio yetu ni kwamba reli ya SGR baada ya kuwa inafika Mwanza, tunatamani kutokea Mwanza kwenda maeneo mengine kwa maana ya Nchi za Kenya na Uganda, waweze kutumia bandari ya Musoma, waweze kutumia bandari ya Sota kufika maeneo ya Kenya na Uganda. Sasa isipokuwa inawekwa kwenye bajeti kila mwaka inakuja haitengewi fedha na ilivyochakaa pale Mheshimiwa Waziri, haipendezi. Ninatamani sana na yenyewe muiweke kwenye vipaumbele Bandari ya Musoma Mjini na Bandari ya Sota. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho kama nilivyosema, ni juu ya jengo la abiria kwenye eneo la kivuko cha Musoma na upande wa Kinesi. Wananchi wale wakati wa mvua na wakati wa jua kali Mheshimiwa Waziri, hawana mahali pa kujikinga jua wala mvua wakiwa wanasubiri kivuko. Ninaomba pia, nimeona kwenye bajeti umelisemea, kivuko hiki kiharakishwe kwenye pande zote mbili, upande wa Kinesi na upande wa Musoma ili angalau kuweza kurudisha matumaini na kuweza kuwasaidia hawa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, nimeona hapa Barabara ya Kuruya – Makutano kwa maana ya Makutano – Komuge mpaka Kinesi mmeiweka kwenye utekelezaji kwa ajili ya kuandaa mpango kwa maana ya ufanisi. Ninaomba barabara hii pia kwa bajeti ya mwakani tuiwekee lami kwa sababu ni muhimu sana kiunganisho kati ya maeneo ya kivuko, maeneo ya Kinesi na upande wa Kuruya kuja maeneo ya Musoma mpaka Mwanza. Kwa kuwa mmetenga fedha za upembuzi yakinifu, ninaomba sana mwakani Mheshimiwa Waziri barabara hii pia uikumbuke.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema mimi kwenye Wizara hii sikuwa na neno kubwa zaidi ya kutoa shukrani kwa furaha kubwa ambazo wananchi wangu wamefarijika. Nitumie nafasi hii kukuomba sasa Mheshimiwa Waziri usiishie tu kuiweka kwenye bajeti, barabara hii ni muhimu sana kwa kiungo cha Mkoa mzima wa Mara iwekee fedha itangazwe ili ianze kujengwa kwa kiwango cha lami kwa maana ya kutoka Utegi – Shirati kwenda mpaka kule Sota na maeneo ya Kirongwe. Ninaamini kabisa itafungua uchumi wa hizi Nchi mbili kwa maana ya Kenya na Tanzania.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, ahsante sana. naunga mkono hoja. (Makofi)