Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Elibariki Emmanuel Kingu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa unyenyekevu kabisa naomba nichukue nafasi hii kukushukuru sana kwa heshima kubwa uliyonipa ya kuweza kutoa mchango wangu katika Wizara hii nyeti kabisa ambayo inahusiana kabisa na kuchochea maendeleo ya Taifa letu. Nakwenda kuzungumza maeneo mawili matatu kwa kifupi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nitumie nafasi hii kama wengine walivyofanya kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Profesa Mbarawa na wasaidizi wake wawili Manaibu Waziri pamoja na Makatibu Wakuu wanaoongoza Wizara hii kwa ufanisi mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Singida, nimuombe Mheshimiwa Profesa Mbarawa, tunatambua kazi kubwa sana wanayoifanya Mheshimiwa Profesa na Wizara yake katika ujenzi wa kufungua barabara za kiuchumi. Barabara ya Tanga inayotokea Kiteto kuja kutokea Kondoa kwenda mpaka Singida, tunampongeza sana Mheshimiwa Profesa Mbarawa na Wizara yake. Sasa nimwombe, ili tuwasaidie wananchi wa Mkoa wa Tabora na Singida, wananchi wanapotoka Tabora wanazunguka Nzega, Igunga, Arusha, wanakwenda Same, wanakwenda Tanga, hiyo barabara ni ndefu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nampa Mheshimiwa Profesa alternative ya barabara. Hii ambayo ameifungua kutoka Tanga kuja mpaka Singida, aje jimboni kwangu kuna barabara inatoka kwangu inakwenda Mtunduru, inakwenda Igombwe, inakwenda Iyumbu, inakwenda mpaka Tabora, hapa atakuwa amekata zaidi ya kilometa 200 za watu kuzunguka kufika Tanga. Sasa namwomba kaka yangu Waziri na Wizara yake, afanye feasibility study, afungue barabara hii na kuna shughuli nyingi za kiuchumi zinakwenda kufanyika pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo naomba niwasemee watu wa Kusini. Inawezekana kabisa watu wa Kusini wametumia muda mwingi sana kujisemea wakaonekana huenda wanazungumza sababu wao wanatoka Kusini. Sasa huenda leo mimi Mbunge wa Singida Magharibi nikizungumza kwa maslahi ya Taifa na nchi, huenda naweza ninaweza nikaeleweka na kuleta tija kwa maslahi ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma statistics hapa, feasibility study inaonesha sasa hivi ndani ya miezi 14 zimesafirishwa tani za makaa ya mawe milioni 2.3. Ukienda kwenye statistics unahitaji kama lori moja litakuwa linafanya kazi ya kusafirisha haya makaa ya mawe, unahitaji malori 2,000 kuweza kuya-tap makaa ya mawe kule yanakozalishwa kuyafikisha kwenye bandari tayari kwa kusafirishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nchi, kupanga ni kuchagua. Hivi kweli barabara zetu zinaweza zika-afford malori 2,000 kupita barabarani na kuangalia gharama kubwa ambayo Serikali inaingia katika kujenga barabara? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa niaba ya watu wa Kusini. Leo nazungumza kama Mbunge wa Singida Magharibi, mimi sitoki Kusini, lakini nazungumza jambo hili kwa sababu limebeba maslahi mapana ya Taifa hili, limebeba maslahi ya kiuchumi ya Taifa hili. Mheshimiwa Profesa Mbarawa feasibility study iliyofanywa mwaka 2016 chini ya RAHCO inaonesha namna gani potential ya kiuchumi ya ile corridor ya Mtwara tunayoizungumza jamani. Kuna potential za kiuchumi kule, kuna potential za utalii, kuna potential za kilimo, kuna potential za investment nyingi zimewekwa kule. Naomba nitoe ushauri, wamwache Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aandike kitabu chake mwenyewe, wamwache mama Samia atengeneze legacy yake mwenyewe kwenye uongozi, wamwache mama yetu aruhusu mifumo ya uwekezaji. Tukajenge reli ya corridor ya Mtwara tuweze ku-tap coal inayozalishwa kule na kuileta katika Bandari ya Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikwambie, tukiwa kama Wabunge, tukiacha kuangalia ukanda tukaweka maslahi ya nchi mbele, Taifa hili litapiga hatua. Nataka nikwambie wapo wawekezaji wako tayari kufanya investment za build, operate na ku-transfer, wamejaa Mheshimiwa Profesa Mbarawa, lakini PPP pia zinafanya kazi. Kama Serikali hawana finance, watafute private sector wakawekeze, hawa watu wa Mtwara wakiwekeza haitakuwa kwa faida yao, itakuwa ni kwa faida pana ya maslahi ya hili Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Profesa Mbarawa chondechonde, kama kuna vitu atakuwa amemsaidia Rais wetu kuacha legacy ni kumruhusu Rais wetu wa Awamu ya Sita ajenge reli ya corridor ya watu wa Mtwara kwa lengo la ku- tap resources zilizoko kule kwa maslahi mapana ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, hili la bandari sikuwa na nia hata ya kulichangia sana kwa sababu, jamani kwa dunia ya sasa hivi Waheshimiwa Wabunge, hivi kweli kwa dunia ya sasa hivi tunaweza tukawa na hofu ya kubinafsisha mwendeshaji wa Bandari hii ya Dar-es-Salaam, kweli? (Makofi)

MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kingu kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Maimuna Pathan.

TAARIFA

MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. naomba kumpa Taarifa Mbunge anayeongea sasa hivi, Rais wetu wa kwanza, Mwalimu Nyerere, alikuwa hataki mambo ya ukabila, ukanda, wala udini. Kwa hiyo, nampa pongezi kubwa sana bado anamuenzi Rais wetu wa kwanza kwa kuondoa ukabila, udini na ukanda. Big up na huo ndio Ubunge tunaoutaka wa kitaifa. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kingu, Taarifa unaipokea?

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa hii kwa sababu imeni-recognize kwamba, ni Mbunge wa Kitaifa, nimeipokea kwa mikono miwili. Namshukuru sana Mheshimiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la bandari, jamani kwa wale tunaotembea duniani hebu tuwe na trust nak il ambacho mamlaka inafikiria kwa lengo la kuongeza revenue kwenye hii nchi. Hili la bandari, hivi kweli kuna mashaka kwamba, tukibinafsisha bandari yetu ile katika operation, si walikuwa wanafanya TICTS jamani, si walikuwa wanafanya TICTS juzi tu hapa, sasa kuna ubaya gani kampuni nyingine ikaja kuleta ufanisi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeambiwa, mimi natoa mfano, juzi kati niliingiza vitanda vya kusaidia akinamama jimboni kwangu, miaka miwili iliyopita. Ukiangalia gharama ya kukodi container moja mpaka hapa dola 4,000, lakini wenzetu wanalipa dola 1,600 au 1,800 jamani kuna shida gani kubinafsisha bandari, tija ipatikane, maendeleo ya nchi yapatikane? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengine jamani tuangalie maslahi ya nchi. Huyu Rais aliyeko madarakani hawezi kufanya jambo kwa maslahi ya familia yake na watoto wake. Chochote atakachokifanya mama yetu atafanya kwa ajili ya maslahi ya nchi na sisi Wabunge huwa tuko wazi hapa, mambo yakija ndivyo sivyo, hatuogopi kusema, tunasema wazi, lakini hili lina maslahi ya nchi. Rais wetu aungwe mkono, Bandari ya Dar-es-Salaam, tena nawaambia, nashangaa sana kwa sababu, Serikali sisi Wabunge kazi yetu ni kuwashauri, lakini nashangaa sana, hili jambo wanataka kulifanya kama vile mpaka sijui fulani aamue, hapana. Jambo linalohusiana na maslahi ya nchi na ndio maana tuna Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wafanye kazi wasiogope.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi matarajio yetu ni kuona bandari ile inapata ufanisi na mambo yanakuwa mazuri kwa maslahi ya Taifa hili. Wala wasisubiri eti kumuuliza na kuhoji mtu fulani aone nini kinafanyika. Ndio maana tuna Amiri Jeshi, yuko Kikatiba, yuko kisheria, hakuna mtu wa kuweza kuuliza kinachofanyika, zaidi tutahoji tunapoona kuna violation ya maslahi makubwa ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ambalo naomba nichangie, wengi wamezungumza kuhusiana na mambo mazima ya ujenzi wa SGR na mambo mengine. Nataka niseme kitu kimoja, lazima kwenye hili tuelewane, wakati mwingine tunaweza tukawa na hisia za kuhisiana tu ambazo zinaweza zisilisaidie hili Taifa. Niwaombe sana, Mheshimiwa Jerry Silaa leo amezungumza mchana na nimempa Taarifa, takwimu zinaonesha na kuna muda nilikosea nikatamka kwamba, engineering estimates nikazitaja kama BOQ.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa zinaonesha Tanzania ndio nchi ambayo kwa kutumia rasilimali zetu na mikopo tunayokopa tumeweza kujenga reli kwa bei nafuu sana ndugu zangu. Hii habari tunazungumza sijui ya mabehewa, sijui ya nini, hivi kweli leo kama nchi, tumepata mkandarasi anaambiwa na Serikali tunaomba utupe guarantee ya ubora wa mabehewa yako, anasema hapana najitoa, Serikali gani itakuwa tayari kumpa mtu huyo kazi? Haipo duniani. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Kingu, muda wako umekwisha.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi nikushukuru sana kaka yangu Mungu akubariki sana. Japokuwa Mheshimiwa Shigongo alikuwa anaomba niongezewe muda, lakini naomba kwa heshima yako nikae. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.