Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Robert Chacha Maboto

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii mchana huu wa leo ili na mimi niweze kuchangia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Lakini pia nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya kwa ajili ya kupeleka fedha za maendeleo katika majimbo yetu ili kukamilisha miradi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niishukuru Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi inayoongozwa na Mheshimiwa Makame Mbarawa na Naibu wake kwa kazi kubwa ambayo wameendelea kuifanya, lakini pia kwa namna ambavyo wametekeleza mradi mkubwa wa barabara ya kiwango cha lami kutokea Jimbo la Mwibara, Jimbo la Bunda Mjini, na Jimbo la Bunda Vijijini. Barabara hii ilisumbua kwa muda mrefu lakini kwa sasa imeendelea kukamilishwa kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Wizara ni kuhakikisha kwamba barabara hii wakati inajengwa tuta lile lililowekwa kwenye barabara ile limekuwa juu sana kuliko makazi ya wananchi wetu. Niwaombe sana Wizara ikumbuke kuwawekea wananchi wetu barabara zile zinazoingia katika makazi yao ili ziweze kuendana na hali halisi ya barabara yenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine katika barabara hii. Wizara ituwekee taa za barabarani ambazo zitakuwa zinatokea kwenye maungano ya barabara pale kuelekea barabara ya Kibara na hii barabara inyokwenda Nyamuswa, watuwekee taa za barabarani. Lakini pia katika barabara hii tuna taa za upande mmoja kutokea Balili Kwenda Nyasura, ambako taa hizi zimewekwa upande mmoja na upande mwingine hakuna taa. Kuhusiana na jambo hili mimi nilishajaribu kuzungumza na Meneja wa TANROADS wa Mkoa, nikamuomba, kwamba, katika meneo mengine mengi ambayo mimi nayaona taa zote za barabarani zimewekwa kwa pande zote mbili, ni kwa nini, Bunda tu peke yake kuwe upande mmoja?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri atusaidie kwenye jambo hili ili liweze kuendana na hali halisi; ambapo taa zinawekwa katika maeneo yetu. Lakini jambo jingine, Mheshimiwa Waziri nikushukuru katika Jimbo letu la Bunda Mjini katika Bajeti tumepata taa za kuongozea magari kwenye makutano yale ya barabara ya Kisorya, Nyamuswa, Mwanza na Musoma; tumepata taa za kuongozea magari. Na jambo hili mimi nililisema nikasema kwenye eneo lile tukisema tuweke ule mzunguko eneo lile ni dogo kwa sababu litatulazimisha kwenda kubomoa makazi ya wananchi wetu. Naishukuru Wizara, na kwa sababu imekubaliana na hili jambo lile likifanyika naamini kwamba litaufanya Mji wetu wa Bunda uweze kukaa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia jambo jingine tunaishukuru Wizara kwa sababu wanatekeleza miradi mikubwa pale ya kujenga mizani katika Halmashauri yetu ya Mji wa Bunda Kata ya Balili na kata ya Buta. Sasa mizani hii ina muda mrefu. Niwaombe sana Wizara muhakikishe kwamba viongiozi wetu wa Mkoa wa TANROADS wanasimamia miradi hii ili iweze kukamilika vizuri, lakini mizani hii ikikamilika kwa wakati itatusaidia kulinda zile barabara zetu, hasa hii barabara mpya inayokwenda Kisorya na inayokwenda Nyamuswa, ya lami, mzani ule utatusaidia kulinda sana ule ulioko kule Buta; na hii barabara kuu ambayo inakwenda Mwanza na Musoma. Mizani hii ikamilika kwa wakati ili iweze kulinda barabara hizi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Mheshimiwa Waziri jambo jingine ni kuhusiana na Mfuko wa TARURA. Tuiombe Wizara iendelee kuwaongezea fedha watu hawa wa TARURA ili waendelee kutusaidia katika barabara zetu zile za mitaa ili zikamilike. Kazi imefanyika Mheshimiwa Waziri lazima tukuthibitishie hilo lakini bado tatizo lipo, kwa sababu barabara zile kwa muda mrefu zimekuwa hazifanyiwi matengenezo. Kwa kipindi hiki tumeona matenegenezo yanafanyika na wananchi wanaona hatua zinachukuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana tuendelee kuwapa TARURA nguvu kwa kuwapitishia bajeti ya kutosha ili kwamba weze kutusaidia kuhakikisha kwamba barabara hizi zinapitika kwa muda wote, na hasa kwa sababu mji wa Bunda ndio sura halisi ya Mkoa wa Mara. Utakapokaa vizuri mji wa Bunda ndiyo picha halisi ya Mkoa wa Mara, na kwa sababu pia tuko pembezoni mwa Mbuga ya Serengeti. Mtu yoyote mtalii anayekwenda Mbuga ya Serengeti lazima apite Bunda. Mtu yoyote anyetoka Mwanza nakwenda Silali Kenya lazima apite Bunda. Anaweza asipite mahali pengine popote lakini Bunda Mjini lazima apapite. Kwa hiyo ni vizuri Mheshimiwa Waziri jambo hili la taa za barabarani, taa za kuongoza magari zikawekwa katika Halmashauri ya Mji wa Bunda ili iweze kuleta mvuto mzuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri jambo jingine ni suala la Barabara ile ya Manyamanyama, Kabulabula, Muhoji, Masinono Kwenda Bugwema ambayo inakwenda kwenye shamba la kilimo la Bugwema. Barabara ile ni pamoja na barabara ile ambayo inatoka Musoma Mjini kwenda Majita ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo Barabara hii nayo ya Manyamanyama, Kabulabula, Muhoji, Masinono ikijengwa kwa kiwango cha lami itawasaidia wale watu wenye magari makubwa ambao wanalazimika kwenda kupita kuzunguka kule mbali, wakapita hapa ikawa ni rahisi kwenda kwenye shamba letu la Bugwema na kwenda kuchukua mazao ya wananchi huko. Kwa hiyo niwaombe sana Wizara jambo hili na lenyewe waliangalie ili waliweke kwenye mpango wao ili liweze kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii itakapokamilika vizuri itaufanya Mji wetu wa Bunda ukae vizuri. Na sasa hivi tatizo kubwa ambalo tunalo pale lililobakia ni hizo barabara za mitaa. Niwaombe sana Wizara, na kwa sababu bahati nzuri tumepata Meneja mzuri pale wa TARURA wa Wilaya ndugu yangu Baraka na Meneja wa TANROADS wa Mkoa, tunashirikiana nao vizuri kuhakikisha kwamba tunatatua tatizo hili la uchakavu wa barabara katika maeneo yetu. Niwaombe sana Wizara watu hawa twende nao vizuri ili waweze kutusaidia kuhakikisha kwamba changamoto zetu hizi za wananchi tunazitatua vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninakushukuru na ninaunga mkono hoja.