Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Suma Ikenda Fyandomo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Ujenzi. Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na uzima ambao nipo nao sasa hivi, nimepata nguvu ya kusimama, kuongea kwenye Bunge hili Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Mbarawa pamoja na Naibu Waziri, kaka yangu Kasekenya; Mheshimiwa Naibu Waziri, kaka yangu Fredy Mwakibete; nawapongeza kwa kazi nzuri mnazozifanya na namna ambavyo mnazipitiapitia hizi barabara zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiomba kitu ukapewa unapaswa kushukuru. Nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyoguswa na barabara yetu ya Inyala. Ajali zilikuwa nyingi sana, akatutumia fedha kiasi cha shilingi 6,998,000,000 tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuokoa uhai wa watu wengi pale Inyara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ahadi ya awamu ya nne, ahadi ile ni ya barabara ya kutoka Katumba kupita Suma kwenda Mwakaleli, Ruangwa, Mbwambo mpaka Tukuyu Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile barabara ni muhimu sana, kwa sababu inapita barabara inatokea Rungwe inatokea Busekelo kule halafu inarudi tena Tukuyu Mjini. Naiomba sana Serikali, sijasikia hapa kwamba kuna fedha yoyote ambayo imetengwa kwa ajili ya barabara hiyo ya kutoka Katumba Suma - Mwakaleli kutokea Tukuyu Mjini. Hivyo, naomba kwenye mipango yenu ya bajeti msiisahau barabara hiyo kwa sababu tumeiomba kwa muda mrefu. Naishukuru sana Serikali kwa kipande kwa sehemu kuanzia Tukuyu Mjini kule imeanza kufanya kazi nzuri ya kuweka lami, ninaishukuru Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ambayo ilikuwa ni korofi sana Barabara ya Ibanda kwenda Itungi Port. Barabara hiyo ni muhimu sana ambayo inapitia Kyela Mjini. Naishukuru Serikali ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ni Sikivu, hiyo barabara mkandarasi yuko site inafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya kutoka Igawa kwenda Tunduma Mkoa wa Songwe. Ile barabara ni barabara muhimu sana. Zinapita gari ambazo zinakwenda kwenye border mbili; border ya kwenda Malawi na border ya kwenda Zambia. Ile barabara ni barabara ambayo ninaiongelea kila wakati hapa Bungeni. Ile barabara ni nyembamba ambayo inapitisha makontena ya 40ft, 20ft, pamoja na petrol-tank, lakini na mabasi yote yanapita hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile barabara ni nyembamba halafu ina corrugation ajali kila siku. Wananchi wa Mkoa wa Mbeya kwa tatizo la barabara ile, wengi wamekuwa walemavu, lakini wengi wamepoteza familia zao kwa ajali zinazotokea kutokana na barabara ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali ilipokuwa inawasilisha hapa sijasikia hizo kilometa 181 kwamba ni lini itaanzwa kujengwa hiyo barabara. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, hiyo barabara ni barabara ambayo ina misiba, kila siku tunalia wananchi wa Mkoa wa Mbeya. Tumechoka kulia misiba. Pia walemavu wengi wanapatikana kupitia barabara ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, sijajua kwamba Mheshimiwa Waziri ile misiba ungekuwa unaona namna tunavyolia, ni kwa sababu huoni. Ungekuwa unaona, nakwambia ungepata uchungu kwamba ile barabara uipe kipaumbele. Naongea kwa uchungu kiasi kwamba natamani hata misiba wakati fulani tukiihamishia humu Bungeni kupiga yowe labda ndiyo Serikali itasikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa namna ambavyo imetenga fedha, ile barabara ya kilometa 29 ya Mbeya Mjini barabara nne. Pia namshukuru Mheshimiwa Rais, katuongezea kilometa nne zingine za kuanzia pale Uyole kwenda mpaka Mlima Nyoka. Mheshimiwa Waziri akiwasilisha hapa ameongea kwamba mkandarasi yupo ameishafika na andaa utaratibu. Wananchi wa Mkoa wa Mbeya hatuona kwamba ameshaanza huyo mkandarasi, kwa sababu hatuoni mitambo yoyote, tungeanza kuona mitambo imefika, hekaheka zimeishaanza za kuandaa juu ya barabara ile basi tungejua barabara ile imeshaanza rasmi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa namna ambavyo umenipa hii nafasi, Kkuna barabara ya kutoka Makongorosi – Lupa mpaka Rungwa ile barabara ni kilometa 356 ni barabara muhimu ambayo inakwenda kuunganisha Mkoa wa Singida na Tabora. Ningeiomba sana Serikali angalau kwa kilometa 100 ingewekea bajeti ya kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya Rujewa – Madibila; barabara ya Rujewa – Madibila ni kilometa 92, ni barabara muhimu sana kule kuna mazao mengi, mazao ya kutosha ile barabara ni mbaya. Ninaomba sana Serikali kwa matamko mliyotamka hapa kwamba mnaitambua, naomba muiwekee bajeti ya fedha ile barabara ikikamilika kilometa hiyo 92 inakwenda kuunganisha na barabara kilometa 60 kutoka Madibila mpaka Mafinga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa namna ambavyo unavyoendesha Bunge letu hapa mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wastaafu ambao walistaafishwa Air Tanzania, wana kilio kikubwa sana, mwaka jana kuna fedha za waastafu ambazo tulipitisha hapa Bungeni, wastaafu wale wana kilio kikubwa sana, wafanyakazi ambao walikuwa wakifanyakazi ATC. Ninaomba usikie kilio cha wale watumishi wa Air Tanzania tangu walivyostaafishwa wengine miaka kumi mbili imepita hawajapewa mafao yao, wengine miaka sita na wengine wamekufa bila kupata fedha zao, ninaomba hili ulichukulie kipaumbele. Hawa watu mkiwafuta machozi yao, mkawapatia fedha zao za kustaafu basi watawashukuru sana, lakini sijajua ni nini kina zuia kama mwaka jana tulipitisha bajeti hapa mlisema ni za wastaafu ni kwa nini hamjawafikishia fedha zao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nimshukuru na kumpongeza sana Engineer wa TANROADS wa Mkoa wa Mbeya Engineer Masige, amekuwa akisimamia vizuri sana hizi barabara za mkoani kwetu Mbeya, pongezi nyingi sana zimuendee Mheshimiwa Engineer Masige chini ya kiongozi mkuu ambaye ni Mkuu wa Mkoa wetu Homera.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Suma ahsante sana. Muda wako umeisha.

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia.