Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

hon Hassan Seleman Mtenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kukushukuru kwa kupata nafasi hii adhimu ya kuchangia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Nami niungane na mwenzangu kumshukuru Rais wetu mpendwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na ni wajibu wetu kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa sababu kwenye jimbo langu ni mabilioni ya shilingi ambayo yameingia kwa kipindi kifupi na kazi zinaendelea. Mungu ambariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitoe pongezi kwa Waziri wetu Mheshimiwa Mbarawa, lakini na Naibu Mawaziri kwa kazi kubwa wanazozifanya kwenye Wizara hii. Kule kwangu siwezi kumuacha Engineer wa TANROADS, Ndugu yangu Dotto, kwa kweli anaiwakilisha Mtwara vizuri na utendaji kazi wake ni mzuri kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maeneo kama kama matatu ya kuchangia, lakini eneo la kwanza ili kupunguza urasimu wa mambo yote ambayo tunayajadili ndani ya Bunge hili. Tunazungumza mambo mengi sana ya msingi, lakini kila tutakalozungumza kwenye Bunge hili linagusa sheria kwenye eneo husika. Sasa kwa nini nimezungumza sheria. Tunaizungumzia sheria leo tunazungumza masuala ya uwekezaji ndani ya nchi yetu lakini kwenye suala la uwekezaji bado kuna sheria ambayo zinatufungwa, tunashindwa kuondoka pale tulipokuwa kuelekea kwenye eneo lingine. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri katika Wizara yake watuletee sheria hapa, hata kesho tuweze kufanya mabadiliko ili tusonge mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi wagonjwa wa malaria nyumba moja hawawezi wakaamshana kwenda hospitali. Sasa kwa nini nazungumza hivi? Ziko hoja ambazo tunazungumza kuhusu uwekezaji wa bandari. Uwekezaji huu wa bandari kila mtu ana mawazo yake ndani ya Bunge hili, lakini kuna wengine wanasema tuendelee kujifunza, lakini TICTS wana miaka mingi wako pale bandarini na kama ni shule kwenye Serikali wamepata kupitia TICTS. Ni vyema sasa shule ile tulioipata kutokea TICTS twende tutafute wawekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja ambayo inazungumza kwamba bandari yetu ni ndogo, bandari ile imeingia kwenye upanuzi zaidi ya mara tatu, wakati tunaanza Bandari ya Dar es Salaam haikuwa vile. Kama tunampata mwekezaji na tunasema bandari ile itakuwa ni busy zaidi kwenye mikataba tuingize suala la yeye kupanua bandari, ni kitu ambacho kinawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bandari yetu ya Dar es Salaam inatumika na nchi zaidi ya nne na ndio maana tunaiona ipo busy sana. Sasa niishauri Serikali katika Bandari ya Dar es Salaam pamoja na uwekezaji mkubwa tunaotaka kuufanya, ziko bandari zingine ambazo inawezekana vile vile tukazisaidia. Mfano, leo tunaichukua Zambia na Malawi tukasema wafanyabiashara wote wa Zambia na Malawi watumie Bandari ya Mtwara. Tukaichukua Burundi na nchi zingine na Congo waje watumie Bandari ya Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili inawezekana likatupatia kipato kikubwa sana na hili nimekuwa napiga kelele sana Bungeni. Yawezekana naeleweka au inawezekana nisieleweke, lakini kwa hali nyingine nimshukuru Rais, nilikuwa napiga kelele sana kuhusu Daraja la Mto Ruvuma kule Kilambo. Naishukuru Serikali imeridhia kujenga daraja lile. Daraja lile ukubwa wake inawezekana ukawa zaidi ya kilometa mbili na point au tatu. Katika Afrika inawezekana likawa ni daraja la kwanza kuwa na ukubwa mrefu namna ile ambalo litatumia mabilioni ya shilingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu amefanya maamuzi magumu ya kuwasaidia Wananchi wa Mtwara, lakini ujenzi wa daraja lile sio la wasaidie Wananchi wa Mtwara, daraja lile ni ujenzi wa Kitaifa kwenye rasilimali ya Kitaifa kwenye mapato ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie suala la reli. Tulikuwa na package ya Mtwara Corridor, tunazunazungumza bandari, tunazungumza airport, tunazungumza na reli. Reli ya Mtwara Mbamba Bay imekuwa ipo kwenye makabrasha miaka yote toka mimi nazaliwa na Wabunge wote waliopita kutoka Mtwara wanaizungumzia reli hata kama ilikuwepo na ikaondolewa. Sasa leo Mchuchuma na Liganga tayari tuna madini ghafi na madini haya yanatakiwa lazima tuwe na reli ya ufanisi ili yaweze kusafiri kwa wakati na mzigo ifike ikiwa salama.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri, suala la Reli ya Mtwara Mbamba Bay ipewe kipaumbele sasa…

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Hassan kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kingu.

TAARIFA

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nimpe taarifa mchangiaji kwamba, kwa mujibu wa feasibility study iliyofanywa mwaka 2016, jumla ya tani 500,038 za makaa ya mawe zilipita kwenye barabara na kwa feasibility study ya mwaka 2022 tani milioni 1,233,000 zimepita kwenye barabara na feasibility study ya mwaka huu tani milioni 2.3 zimepita kwenye barabara. Kwa trend hii naomba nimpe taarifa mchangiaji kwamba anachokizungumza kina make sense kujenga reli ya kusini ili kuokoa barabara zetu kwa maslahi ya Taifa. Natoa wito kwa Mheshimiwa Waziri feasibility study ya ujenzi wa reli hii uanze haraka kwa maslahi ya Taifa na kuwasaidia watu wa Kusini, wamelia muda mrefu, inatosha. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Mtenga taarifa unaipokea?

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, microphone zimegoma.

MWENYEKITI: Hamia kwa jirani yako hapo Mheshimiwa.

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, niko sawa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Hassan taarifa unaipokea?

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii naipokea kwa mikono yote na miguu na ninampenda sana, mtoaji taarifa huyu ana akili kubwa sana,Mungu akubariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la International Airport Mtwara. Uwanja huu naishukuru sana Serikali namshukuru Rais, tumejenga uwanja zaidi ya shilingi bilioni 14 na something lakini uwanja huu tunazungumza leo katika fedha zote zilizopangwa kwenye bajeti tulikuwa tupate na gari ya zimamoto (fire), lakini kila ukiuliza watu wa manunuzi leo ni mwaka wa tatu tunazungumza kwenye manunuzi ya kuleta gari la zimamoto Uwanja wa Ndege Mtwara, ni mwaka wa tatu tunazungumzia manunuzi. Ni vitu vya hatari sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni Sheria ya Procurement inakuwa hivi, tunatokaje hapa tulipo? Uwanja wa ndege kulikuwa kuna package ya kujenga majengo ya kukaa abiria mpaka leo kwenye bajeti hii nimechungulia sijaona na wala sijasikia. Sasa nikuombe Mheshimiwa Waziri unapokuja hapa utupe majibu mazuri kuhusu uwanja ule, gari la zimamoto, tunahitaji na jengo la abiria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza utanuzi ndani ya nchi haswa wa barabara na mimi naipongeza sana Serikali yangu, imefanya kazi kubwa kwenye miundombinu. Watu ambao wanatoka Mtwara na Lindi wanakwenda zao Dodoma au wanakwenda Morogoro, iko shortcut ambayo inawezekana Wizara ikakaa ikajipanga tutengeneze barabara ambayo ni shortcut. Tunafika mpaka Kibiti, unaingia mpaka Mloka, Bwawa la Mwalimu Nyerere tunakwenda hadi Morogoro. Barabara ile inakuwa ni fupi kuliko gari za mizigo zinazunguka mpaka zinaenda Dar es Salaam, zikitoka Dar es Salaam zitafute Kibaha, zitafute Morogoro, mambo mengine ya msingi yapo kwenye uwezo wetu. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mtenga, muda wako umeisha.

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)