Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Julius Kalanga Laizer

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MWENYEKITI: Mheshimiwa Julius Kalanga Laizer, atafuatiwa na Mheshimiwa Emmanuel Papian, atafuatiwa na Mheshimiwa Jamal Kassim Ally, atamalizia Mheshimiwa Peter Serukamba!
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nitumie fursa hii kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Monduli kwa kuniamini na kunituma kuwa mwakilishi wao katika jengo hili lakini pia nimshukuru Mungu kwa kuendelea kutupa afya njema hadi muda huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango ulioko mbele yetu kwa mtazamo wa kimaandishi ni mpango mzuri sana, kama ambavyo wamesema wengine, nchi yetu tunalo tatizo la kutekeleza Mipango, lakini mmekuja na kaulimbiu hapa kazi tu, tunataka tuwapime katika hili. Kumekuwa na excuses nyingi na ni Tanzania pekee duniani nchi inayofanya trial and error kwa miaka 54 ya uhuru kutafuta msimamo wa uchumi wa nchi na elimu ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara ya kwanza tulikuja na Kilimo Kwanza, tukaja na BRN imekwama, leo tumekuja na nyingine ya viwanda ambao umekuwa ni wimbo wa Taifa kila wakati, kila wakati tunabadilisha. Amekuja Waziri hapa wa Elimu amebadilisha elimu yetu mara nyingi, tunamshukuru Profesa Ndalichako amesema yeye anarudisha ile division na ni kweli ali-sign vyeti vyetu.
Katika hili lazima tuwe na misingi inayodhibiti elimu, haiwezekani kila Waziri anayekuja anaamua yeye aina ya elimu tunayotaka, lazima kuwe na mjadala unaoshirikisha wadau hasa Walimu na wenye professional hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni aina gani ya elimu ya watoto wetu tunahitaji! Leo tunataka tuagize wageni kutoka nje kwa sababu ya gesi na tunajua tuna rasilimali hii ya gesi, lakini hatujafanya investment ya kuwasomesha vijana wetu kuanzia ngazi ya chini kuhusu rasilimali tuliyonayo. Ni ajabu kwenye nchi tuna gesi ya kutosha, tuna madini ya kutosha, lakini hatuna wataalam wa kutosha kwa sababu hatuwajengei msingi wa elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunaendelea kufundisha kwamba binadamu aliwahi kuwa sokwe, ndiyo masomo tunayofundisha watoto wetu, watategemewaje! Kwa hiyo haiwezekani tukawa na nchi ya namna hiyo kwamba mpaka leo hatujui aina ya elimu tunayotaka kuwapa Watanzania wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo kama walivyosema wenzetu katika suala la elimu tunawashukuru, kwa hii kaulimbiu ya elimu bure. Wengine wamezungumza sana habari ya miundombinu, lakini nashukuru na niseme niipongeze Serikali kwa kuleta fedha ya chakula yote kwa wakati katika Jimbo la Monduli katika shule zote za sekondari kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Waziri Mheshimiwa Simbachawene, nilimpigia simu na nikawashukuru sana. Hili ni jambo jema sana, lakini walimu wetu hawana mahali kwa kulala na mnafahamu maeneo ya vijijini. Tatizo la mipango ya nchi yetu, wataalam wengi wanafikiri nchi yetu ni Dar es Salaam, nchi hii siyo Dar es Salaam peke yake. Mnapanga mipango kwa kuangalia pale Dar es Salaam siyo kweli! Yako maeneo ya nchi hii mnatakiwa mfike muangalie namna ya kujenga rasilimali za Taifa zinufaishe Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnasema mnafanya tafiti lakini kwenye Majimbo ya Wabunge hao wote hata wengine wanaowashangilia wanaotoka CCM hamjafika kwenye Majimbo yao. Sasa hizi term of reference, hizi sampling mnazozichukua mnachukulia Dar es Salaam, mnachukulia wapi! Nchi yetu ni kubwa lazima mfike muone maisha ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza uchumi wa kati, lakini uchumi huu hau-reflect maisha ya kawaida ya Mtanzania na hau-reflect kwa sababu hatu-invest katika miradi midogo inayosaidia Watanzania wenzetu.
Leo mnazungumza viwanda vikubwa, lakini hamzungumzi habari ya mifugo ambayo kwato ni rasilimali, nyama ni rasilimali, ni malighafi ya kubadilisha, ngozi, maziwa, lakini sehemu kubwa ya wafugaji wa nchi hii, eneo kubwa ni la wafugaji pamoja na kwamba mnatufukuza kila mahali, lakini hamzungumzi habari ya kubadilisha mifugo kuwa kama zao la biashara, bali mnaangalia kama wanyama waharibifu tu, kila siku kuwahamisha, kila siku kuwafukuza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipotazama sekta ya mifugo kwa mtazamo wa kuona kama zao la biashara kama mazao mengine, hatutaweza kuwaendeleza wafugaji wetu. Hatutaweza kwa sababu lazima kama tunatafuta masoko kwa ajili ya mifugo, ni lazima wananchi wetu watapunguza mifugo wenyewe kwa sababu wanajua kuna masoko ya kwenda kuuza mifugo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijielekeze katika suala lingine la wanyamapori. Ni kweli nchi yetu ina wanyama wa kutosha, lakini kama hatuzungumzi namna ambayo wananchi wataona hawa wanyama ni faida kwao, hatuwezi kuwa na wanyamapori na wataendelea kufanyiwa ujangili kadri iwezekanavyo kwa sababu hatujali wananchi wanaozunguka maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwananchi anatakiwa aone wanyama wale ni muhimu, pale ambapo mazao yake yameharibiwa na wanyama basi fidia inayolingana na madhara yaliyofanyika, ifanyike kwa wananchi, yule mwananchi atamlinda yule mnyama. Ikiwa yule mnyama atakuwa ni sehemu ya kuharibu rasilimali zake, akija mtu wa kuua, anasema mwache aue tu, ananipunguzia kero ya kuharibu mazao. Kwa hiyo, tutazame kwamba wananchi wanaozunguka maeneo yale waone faida ya kuwa na wale wanyama, watawalinda wala hatutahitaji kupeleka bunduki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Maliasili anazungumza habari ya wanyama Monduli, maeneo mengi Simanjiro, hakuna magari ya kulinda wale wanyama. Hivi unafanyaje doria kama huna magari, huna silaha, huna wataalam. Huu ni mchezo na ndiyo maana wanyama wataendelea kuuawa. Unapiga simu watu watoke Ngorongoro waje kufanya doria Mto wa Mbu pale baada ya wanyama kuuawa, baada ya masaa sita, huyo jangili anayekusubiri masaa sita ametoka wapi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama tunataka kulinda wanyama wetu ambao ni chanzo cha mapato ya nchi yetu, ni lazima tufanye investment ya kutosha, tuwe na magari ya kutosha katika kudhibiti ujangili, maana wananchi wetu wanatoa ushirikiano lakini unapiga simu, wale watu wa game controller wanakuja baada ya masaa manne, baada ya masaa matano kwa sababu ya tatizo la gari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko gari moja Monduli pale la Misitu, linaangalia Longido, Kiteto, Simanjiro na maeneo mengine ya Tarangire, gari moja la misitu tena bovu. Hatuwezi kulinda wanyama wetu kwa sura hiyo, lazima kama tunadhibiti ujangili tuhakikishe tunapata vifaa vya kudhibiti suala la ujangili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la afya. Hatuwezi kuwa na Taifa linalozalisha rasilimali kama afya zao zina mgogoro. Katika maeneo mengi tatizo hili la afya ni kubwa sana kwenye nchi yetu, tunajenga majengo lakini hakuna dawa, tunajenga majengo lakini hakuna watumishi. Hivi Taifa gani, ni nguvukazi gani itakayofanya kazi ya kuzalisha kama hawana afya nzuri? Kila siku tunazungumza habari ya upungufu wa dawa, lakini ni story ya kila siku Serikali kusema tunaendelea, tunaendelea kuboresha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba kwa kweli katika zahanati hizi lazima tuboreshe afya za watu wetu ili waweze kushiriki katika shughuli za uzalishaji. Vinginevyo hatutaweza kuwa na maendeleo katika uchumi, katika viwanda, kama jamii yetu inayoshiriki nguvukazi haina afya bora ya kufanya kazi hizo ambazo zinapaswa kufanywa kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la mwisho, ni suala la kukuza uchumi na kukusanya mapato ya Serikali. Tunavyozungumza habari ya kukusanya mapato lazima tudhibiti pia mapato hayo yatumike kwa njia inayostahili kufanyika. Tumeshuhudia, Mheshimiwa Waziri Mkuu alienda akavumbua makontena ambayo tunaambiwa yameibiwa karibu 2000 sijui na mia ngapi, lakini business as usual, story hiyo imekwisha, hatusikii wale wenye makontena wamekamatwa na wamefunguliwa kesi za uhujumu uchumi kwa kiwango gani! Kwa hiyo, tulikuwa tunafanya show ya kwenye TV. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana imezungumzwa hapa habari ya mabehewa hewa, unawashughulikia wataalam, lakini yule Waziri aliyekuwa anahusika katika kudhibiti suala hilo umemwacha. Hatuwezi kuwa na nchi ya double standard, unawaonea hawa, unawaonea huruma hawa, haiwezekani! Kama Mawaziri wamehusika, lazima Bunge lisimamie Serikali, Mawaziri waliokuwa wanasimamia Wizara wakati uhujumu unafanyika, washughulikiwe na ndiyo maana reports zote zinazohusu uhujumu wa uchumi haziletwi kwenye Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmekuwa na story ya tokomeza imefichwa; mmetengeneza Tume ya Majaji, imefichwa; mmekuwa na ile inayoshughulikia Migogoro ya Wakulima na Wafugaji, imefichwa; mmetengeza Tume nyingi za kuangalia hiyo ya bandari na wizi huo, umefichwa kwa nini? Ni kwa sababu wenyewe mnahusika na hivyo hamuwezi kujifunua kwa sababu ya utaratibu huo. Kama tunataka tujenge nchi yetu kila mtu atendewe haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuwafukuza tu Wakurugenzi, tukawaacha wanasiasa wanaoingilia kazi za kitaalam wao wakiwa salama. Ndiyo maana hawaogopi kwa sababu wanaagiza maagizo kwa mdomo, wataalam wanachukuliwa hatua, yeye anabaki salama. Tuanze na hao tuliowapa dhamana ya kusimamia Wizara hizo wakati uharibifu unatokea wao walikuwa wapi! Kama hatuchukui hatua hiyo tutakuwa tunacheza ngoma ambayo haina mwisho wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru sana. (Makofi)