Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Hassan Elias Masala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nachingwea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hoja iliyoko Mezani. Kabla ya kuendelea mbele naomba nijumuike na wenzangu waliotangulia kutoa shukrani lakini pia kutoa neno la pongezi kwa Serikali yetu ya Awamu ya Tano ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Magufuli kwa kazi kubwa na kazi nzuri ambayo imekuwa inafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kuwapongeza Mawaziri wote wa Wizara zote mbili kwa uwasilishaji mzuri na yale waliyoyawasilisha ambayo leo hii tunayajadili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie maeneo makubwa yasiyopungua matano lakini nitajielekeza zaidi katika Jimbo ambalo natokea la Nachingwea, lakini wakati huo huo tutakwenda kuangalia namna gani ambavyo yana-reflect Taifa kwa ujumla katika kuhakikisha tunasonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ambalo napenda kuchangia ni elimu. Katika Jimbo la Nachingwea na kwa ukongwe wa Wilaya ya Nachingwea tuna kazi kubwa ambayo tunatakiwa tuendelee kuifanya pamoja na jitihada ambazo Serikali imeendelea kuzifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kwenye suala la elimu bure ambayo imeanza kutolewa mwaka huu ni jambo ambalo limepokelewa vizuri sana na wananchi wa Jimbo langu la Nachingwea. Nimefanya ziara katika kata zangu zote 34, maeneo yote niliyopita takwimu za uandikishaji zimekwenda juu, hii tafsiri yake ni nini? Kwa mwananchi wa kawaida ambaye alishindwa kupeleka mtoto wake shule sasa hivi jambo hili limepokelewa kwa namna ambayo kwetu sisi wanyonge limekuwa ni jambo la kheri. Kwa hiyo, lazima tuipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi hii ambayo imeamua kuifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na kupokelewa kwa elimu bure, yako maeneo ambayo nimeona kuna changamoto ambazo ningependa kuishauri Serikali yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ni kuangalia namna gani tunaweza tukaongeza bajeti ili tuweze kukabiliana na hizi changamoto ambazo tumeanza kuziona katika kipindi hiki cha mwanzo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo sasa hivi watoto wanakaa chini kama ambavyo tumezungumza, hii ni kutokana na ukosefu wa madawati lakini pia yako maeneo ndani ya Jimbo la Nachingwea watoto wanasomea nje kwa maana hawana madarasa. Kwa hiyo, naomba niungane mkono na wale wote waliotangulia kuomba Wizara ya TAMISEMI ijielekeze kwenye kuongeza bajeti ili tuweze kupata majengo ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba wananchi wanaendelea kutu-support kufyatua tofali na kujitolea wao wenyewe kujenga miundombinu hii, lakini ni muhimu pia Serikali ikaona umuhimu wa kuongeza jitihada ili tuweze kupata pesa hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kuishauri Serikali ni eneo ambalo linahusiana na uendeshaji wa mitihani. Nimefanya mazungumzo na walimu katika shule zote za ndani ya Jimbo langu. Moja ya changamoto kubwa ambayo naiona ni lazima tuiwahi, ni eneo la ukosefu wa pesa za uendeshaji wa mitihani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mitihani hii kwa kipindi cha nyuma kwa sehemu kubwa ilikuwa inategemea michango ya wazazi, sasa hivi baada ya kuondolewa, tayari pesa inayopelekwa kwa idadi ya wanafunzi katika shule, haiwezi kutosheleza kuendesha mitihani mitatu mpaka minne kwa mwaka. Na mimi kama mwalimu natambua umuhimu wa kutoa mazoezi kwa watoto. Usipotoa mazoezi kwa watoto, watakwenda kufanya mitihani vibaya.
Kwa hiyo, ni lazima tujielekeze kutenga pesa ya ziada ambayo itaelekezwa katika kutoa huduma hii ya mitihani ili kuwapima watoto wetu waweze kufanya vizuri katika mitihani yao ya mwisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine katika upande wa elimu ni ujenzi wa maabara. Ujenzi wa maabara umefanyika Tanzania nzima. Kwa Jimbo la Nachingwea, ndani ya kata 29 tayari wananchi walishapokea wito wa kujenga maabara. Maabara hizi zitatupelekea kupata walimu wa masomo ya sayansi; na hili ndilo tatizo kubwa sasa hivi tulilonalo Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Jimbo la Nachingwea walimu wa masomo ya sanaa siyo tatizo, sasa hivi tatizo ni walimu wa masomo ya sayansi. Ili tupate walimu wa masomo ya sayansi ni lazima tukamilishe ujenzi wa hizi maabara ambazo zimejengwa.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Simbachawene, una kazi ya kufanya sasa kaka yangu ili tuweze kupambana. Pale wananchi walipofanya na wameshamaliza nguvu zao, sasa ni muhimu na sisi tukaelekeza pesa ambayo itaenda kumalizia ujenzi wa haya majengo, lakini pia tupate vifaa ambavyo tutakwenda kufundisha watoto wetu kwa vitendo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili liende sambaba na suala zima la uboreshaji wa stahiki za walimu. Walimu wetu wanafanya kazi katika mazingira magumu. Tunahitaji kulipa madeni yao yote ambayo wanatudai. Nakubaliana kwamba madeni hayawezikuisha kwa sababu kila siku walimu wanaajiriwa na hii ni sekta kubwa ambayo imebeba watumishi wengi, lakini ni muhimu tukahakikisha tunalipa madeni ya walimu wetu kwa wakati ili waweze kufanya kazi na waende sambamba na hili suala la utoaji elimu bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo napenda kulichangia ni suala la maji. Nachingwea kuna tatizo la maji. Nachingwea ni Wilaya kubwa kama ambavyo nimesema, lakini pia nachukua nafasi hii kumpongeza Naibu Waziri wa Maji, Mzee wangu Mheshimiwa Kamwelwe; alifika Jimbo la Nachingwea akajionea hali halisi ya pale. Ipo miradi ya World Bank ambayo inatekelezwa ndani ya Jimbo la Nachingwea, lakini bahati mbaya tulishamwambia, miradi saba iliyopo ndani ya Jimbo la Nachingwea haifanyi kazi mpaka sasa hivi, pamoja na kwamba pesa nyingi imetumika kujenga miradi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mzee Kamwelwe, lakini pia naomba niseme Mheshimiwa Waziri wa Maji, ambaye nafikiri atakuwa ananisikia, wananchi wa Nachingwea bado kuna ahadi walipewa na wanasubiri majibu juu ya miradi hii ambayo nimeisema ambapo inaonekana kuna uzembe wa baadhi ya watendaji wameamua kutumia pesa kinyume na utaratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara hizi, jibu linasubiriwa na wananchi wa Nachingwea, na mimi nimetumwa, naomba niliwasilishe mbele yenu ili tuweze kusaidiana kulifanyia kazi, tuhakikishe tunachukua hatua pale ambapo mambo hayajaenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine katika upande wa maji, ni ukamilishaji wa mradi wa maji ya Mbwinji ambayo unatoka Masasi, lakini inagusa Vijiji vya Nachingwea na Vijiji vya Ruangwa ambako anatoka Mheshimiwa Waziri Mkuu. Hali ya maji katika baadhi ya maeneo ndani ya maeneo yanayopita mradi wa Mbwinji siyo nzuri. Kwa hiyo, naomba nikumbushe Serikali yetu, katika bajeti hii tunayoenda kuipitisha, ni lazima miradi hii twende tuifanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu ambalo napenda kulizungumzia; na hili nitoe ushauri; ni miradi ya TASAF. Naomba niungane na Watanzania wote kuthamini na kutambua kazi kubwa ambayo inafanyika katika kutekeleza miradi ya TASAF.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo ambayo nimeona kuna upungufu. Wakati pesa za kutoa kwenye kaya masikini zinatolewa, kuna ushauri tuliutoa, lakini haukupokelewa. Sasa hivi naona kuna umuhimu Serikali hii ya Awamu ya Tano ifikirie namna ya kuboresha eneo hili. Pesa hii kuwapa wale wananchi mkononi kama ambavyo inafanyika sasa hivi, haina tija. Nimezunguka katika vijiji vyangu, nimefanya tathmini kuona ni kwa namna gani wananchi wananufaika na hizi pesa, bado sijaona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Mheshimiwa dada yangu Angellah, kama tunaweza kubadilisha mfumo, ni vizuri pesa hizi sasa hivi na hasa kwa wananchi wa Jimbo la Nachingwea, tukawanunulia matrekta badala ya kuwapa pesa. Matrekta haya yatawasaidia wao wenyewe katika vijiji vyao, kwa sababu kutibulisha ekari moja shilingi 50,000; wanaweza wakatibulisha kwa shilingi 20,000 au shilingi 30,000 tukapunguza gharama. Baada ya kufanya hivyo, nafikiri tunaweza tukaona tija ya pesa hii badala ya kuwapa pesa mkononi ambayo mwisho wa siku wanatumia kutafuta chakula na bado wanaendelea na umasikini wao. Kwa hiyo, hili niliona nilitoe kama ushauri. Eneo hili pia naomba liendane na ile shilingi milioni 50 ambayo inaenda kutolewa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi milioni 50 hii lazima tuwe makini, nayo pia tuwe makini; nayo tungeiratibu, siyo kwa kwenda kutoa katika vikundi kama ambavyo imeshauriwa. Hii bado nilikuwa naona vijiji vipewe maelekezo ya namna gani vinaweza vikabuni miradi ambayo itaenda kunufaisha kijiji na ikasimamiwa na kijiji, badala ya kuwapa pesa ambazo tuna hakika zinakwenda kupotea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vikundi vingi sasa hivi vinafufuliwa kwa sababu kuna hii pesa. Baada ya hii pesa kutolewa nina hakika vikundi hivi vitakufa na vitapotea kitu ambacho sioni kama tutakuwa tumeisaidia nchi yetu na Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho ambalo ningependa kulizungumzia, ni afya. Zipo changamoto ambazo tunaziona lakini bado tunahitaji kuendelea kuiunga mkono Serikali yetu. Kuna eneo la CHF…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana.