Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuweza kunipa na mimi fursa hii niweze kuchangia kwenye bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Utawala Bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia maeneo kadhaa kwa sababu dakika 10 ni chache sana. Nianze na suala zima la utawala bora na utawala bora wenyewe nitaanzia suala la kuwanyima fursa Watanzania kuweza kuona ni nini wawakilishi wao wanafanya Bungeni. Ni dhahiri kwamba tumesikiliza michango mingi sana na mingine kwa kweli inasikitisha, ukimwona Mbunge anasimama, anaunga mkono hoja hii dhalimu ya kupoka haki ya uhuru wa wananchi kuweza kujua wawakilishi wao wanafanya nini then unatakiwa ujiulize mara mbili mbili kwamba hata hao wananchi waliomleta huyu mwakilishi huku walifanya makosa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nilisikitishwa na Mheshimiwa kijana kabisa Halima Bulembo, anasema tukionekana kwenye televisioni ni kwamba tunatafuta umaarufu. Nikasema labda nitembee kwenye hoja yake hiyo hiyo nimuelimishe kidogo huyu mdogo wangu. Akumbuke kwamba sisi wengine tuliweza kupata morale ya kutaka kuingia kwenye siasa baada ya kuwaona wanawake wenzetu akina Mama Abdallah, Anna Kilango, Halima Mdee na wengine na hata ukiwaona watu waliogombea Udiwani na Wenyeviti wa Mitaa wanapata inspiration wanapomwona Esther Matiko anachangia nini, fulani anachangia nini, wanaona kwamba hata sisi wanawake kumbe tunaweza tukiingia kwenye uwanda huu wa siasa. Sasa leo mwanamke kabisa anapiga vigelegele hiyo fifty fifty mnafika vipi? Yaani mnaungana na wanaume ambao wanaona hii ni njia pekee ya kuwakandamiza ninyi msifikie lengo lenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wengine tuna malengo makubwa, kuna Mheshimiwa mwingine alichangia kaka yangu Chegeni anasema kwamba twende tukafanye kazi Jimboni. Mimi lengo langu siyo kulitumikia Jimbo la Tarime tu kuna siku nataka niwe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, ninachokiwakilisha hapa nataka Tanzania nzima itambue Esther Matiko anafanya nini kwa Taifa lake wala siyo Tarime tu.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Kwa hiyo, kama ninyi mna short vision ya Jimbo tu na mnaamua kuwanyima Watanzania haki zao, jitafakarini mara mbili na mkienda pale mnaapa kuitumikia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania halafu mnaikiuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani alisema na Wabunge wengine wamechangia mkubali, msikubali suala hili liko wazi na nitaomba mpitie hii Katiba, tulipokuja tulipewa kibegi kina hivi vitu vyote msiende kuweka ndani ya uvungu pitieni hii Katiba. Mwanasheria Mkuu, Waziri wa Fedha na wengine waliochangia juzi hapa mlikuja mkapotosha lakini ni dhahiri Rais hawezi kuhamisha fungu moja kwenda lingine bila idhini ya Bunge tunaopitisha hapa, Mwenyekiti wewe ni Mwanasheria unajua, ni Mfuko wa Dharura tu. Kasomeni vizuri kuanzia Ibara ya 135 mpaka 140, kama hamna Katiba nitawatolea copy niwape ili tuweze kumshauri Rais asivunje Katiba na sheria yetu ya nchi. Inawezekana kabisa Rais ana lengo zuri aje sasa watuletee statement ya reallocation tuipitishe, mwenye mamlaka hayo ni Waziri au ndiyo hiyo tunasema kwamba hamna instrument kwa hiyo Rais inapoka mamlaka ya Waziri wa Fedha na kufanya anachokifanya ninyi mnapiga makofi, haikubaliki! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie sasa, TAMISEMI na nachangia kwenye Jimbo langu, nimechangia Kitaifa narudi sasa kwenye Jimbo langu.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu bure ni sawa sawa na mgonjwa yuko ICU. Kuna siku nilisema tuseme tumepeleka unafuu kwa wananchi, tusiseme elimu bure. Kwa sababu leo utasema elimu bure lakini Serikali Kuu mnasema Halmashauri ndiyo ijenge maboma, ihangaike kupata madawati lakini hazina uwezo. Kwa mfano kwangu Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI pitia uone, kadri tunavyozidi kwenda mbele Halmshauri ya Mji wa Tarime kwa mwaka huu unaomalizika makusanyo ni shilingi milioni 300. Leo Halmashauri hiyo ijenge maboma ya shule za msingi za Tarime, ipeleke madawati na afanye na mambo mengine kwa fedha zipi? Walau mlitoa Waraka Na.5 wananchi walikuwa wameshaanza kujitolea mara tena Rais Magufuli akasema usichange labda upate kibali, wameacha, watoto wetu wanakosa mahali pa kusomea. Kama mnataka kutoa elimu bure jipangeni tunahitaji madarasa ya kutosha watoto wa Kitanzania wasome. Leo ukienda Tarime watoto zaidi ya 200 kwenye darasa, madarasa yenyewe hayapo. Walimu wanakaa kwenye miti, Tarime Mjini pale ofisi inatazamana na ofisi ya Chama cha Mapinduzi, walimu ofisi zao ni miti. Halafu mnakuja mnasema elimu ni bure. Mheshimiwa Cecilia Paresso hapa kasema do you have seven hundred billions kuweza kufanya elimu bure i-take off. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hamna madawati, hamna madarasa, Sera ya Elimu inasema walau watoto 45 kwa darasa moja wanakaa zaidi ya 200. Walimu wenyewe hawawi-motivated, hawana nyumba, umesema umejenga nyumba 183; sijui 188 kwa sekondari, mimi najiuliza mwalimu apange mjini, achukue sijui ni pikipiki au gari aende kufundisha Kenyamanyori hiyo fedha ni ya kwake kwenye kamshahara kale unakompa hana motivation allowance yoyote ile halafu mtasema elimu bure inaenda kuwa elimu ambayo haina manufaa yaani bora amefika la saba au la kumi na mbili lakini anarudi kitaa hajapata elimu bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili mtu afanye kazi vizuri lazima walau ufanye akili yake itulie yake, mwalimu anayekwenda kumfundisha mwanafunzi ni lazima awe ametuliza akili. Mwalimu hana nyumba na wenye vinyumba vyenyewe wakikaa wananyeshewa nilisema mwaka jana hapa, shule ya sekondari nyumba zao zinavuja wanahamisha vigodoro huku na huku halafu leo useme kwamba watoto wale wa maskini watafundishwa waelewe, hata siku moja. Tuwe na vitabu vya kutosha, tuwe na madawati, tuwe na madarasa ya kuweza kuhakikisha wanafunzi wanakaa walau 45 ili mimi mwalimu ninavyofundisha waweze kunielewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye afya. Sera ya Afya inasema walau kila kijiji au mtaa wawe na zahanati, mmeonyesha mna zahanati 4,500 tangu uhuru mpaka sasa hivi bado kuna upungufu wa zahanati 8,043. Vituo vya afya mnavyo 488 upungufu wa 3,506 na mnajua Maazimio ya Abuja walau asilimia 15 ya bajeti ya Serikali iende kwenye afya tumekuwa tukiimba, you don’t do that. Leo mnasema mnaboresha afya, kama imewachukua miaka 50 tuna vituo vya afya 484 itatuchukuwa zaidi ya miaka 350 kutimiza hivi vituo vya afya vinavyohitajika, watu wetu wanakufa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano kwa Tarime kuna Zahanati ya Gamasara ambayo iko Kata ya Nyandoto inahudumia wananchi wa Kata ya Nyandoto kama kituo cha afya wakati ni zahanati, inahudumia wananchi wa kijiji cha Kongo na Ketere hiyo ni Wilaya ya Rorya na inahudumia wananchi wa Kewamamba na Nyagisya hiyo ni Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Jimbo la Vijijini). Zamani walau mlikuwa mnapeleka shilingi milioni nne kwenye Halmashauri ya Mji leo mnapeleka shilingi166,000 baada ya miezi mitatu, hawa Watanzania tunawapenda au tunachezea afya zao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije tena kwenye Hospitali ya Mji ambayo mliishusha hadhi kutoka Hospitali ya Wilaya mkaifanya Hospitali ya Mji na niliuza swali hapa nikasema ilitakiwa iwe Hospitali ya Rufaa maana inasaidia wananchi wa Rorya, Serengeti na Tarime kwa ujumla siyo mji tu, mnapeleka ruzuku ya shilingi milioni 51 halafu Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mnapeleka shilingi milioni 91 wakati mkijua kabisa kwamba ile Hospitali ya Mji iliyoko mjini inahudumia huko kote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi milioni 51 iweze kutibu Wilaya nzima maana kiuhalisia haitibu wananchi wa Mji wa Tarime tu. Ndiyo maana nasema hivi mna watendaji na watu wenu wanafanya kazi ku-check uhalisia? Halmashauri ya Wilaya ya Tarime haina hospitali, wanakuja kutibiwa kwenye Halmashauri ya Mji wa Tarime, kwa nini mnaweka allocation za kitoto namna hii? Mnachezea afya za Watanzania, tunaendelea kushuhudia wananchi wakifa, waoneeni huruma. Nipeni mwanga maana sioni na mniongezee dakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo. Halmahsuri ya Mji wa Tarime tuna Mogabiri Extension Farm...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Nitachangia siku nyingine kwenye Wizara zingine, nina nondo nyingi sana.