Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Khatib Said Haji

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Konde

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nianze kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kunijalia leo kusimama hapa nikiwa na afya njema. Pili, niwashukuru kwa dhati sana wananchi wa Jimbo la Konde kwa kunirejesha tena hapa ili niweze kuwawakilisha.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, kwa umuhimu mkubwa sana natoa pongezi kwa wananchi wa Zanzibar kwa maamuzi mema na ya dhati ya kumchagua Maalim Seif Sharif Hamad kuwa Rais wa Zanzibar. Suala la Jecha kasema nini, Mwenyezi Mungu ataisimamisha haki hapa duniani na watu wote wataona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ilikuwa ni bashrafu, sasa nataka nianze kuchangia. Ukurasa wa nane wa hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyeitoa hapa alisema, naomba ninukuu:- “Eneo lingine linalolalamikiwa ni Polisi. Kuna malalamiko mengi ya wananchi
kubambikiwa kesi, upendeleo, madai ya Askari kutotimizwa, ukosefu wa nyumba za Maaskari na kadhalika”.
Mheshimiwa Naibu Spika, malalamiko ya raia wa nchi hii juu ya Polisi ni mengi sana. Wakati mwingine tunaweza kuwalaumu Polisi wakati amri hizi wanazozitekeleza Polisi zinatoka kwa viongozi wa CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya uchaguzi mkuu ilitoka amri ya Kiongozi Mkuu wa Serikali, Waziri Mkuu akiwaambia ni marufuku vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara hasa kwa wale waliokuwa hawakushinda. Kiujumla tangazo lile lilihusu kutubana sisi vyama vya
upinzani kuonana na wananchi wetu kuwaeleza ukweli juu ya yaliyotokea katika uchaguzi mkuu, hii siyo sawa! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vyama vya siasa vipo kwa mujibu wa Katiba. Tunapoapa hapa kabla ya kuanza kazi hizi tunaapa kuilinda, kuitetea na kuiheshimu Katiba hii. Leo unapokurupuka na amri zako zilizo kinyume na Katiba hii, wewe ndiyo unayesababisha fujo, tukubaliane! Kuna mambo tunayoinishiwa kama vyama vya siasa kwa mujibu wa Katiba tuna haja ya kuyatenda. Hatulazimiki kuomba vibali kwa Polisi tunapotaka kufanya mikutano yetu ya hadhara, tunalazimika kutoa taarifa, leo imepotea hii na badala yake twende tupige magoti
kwao wao ni nani? Hilo ni moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukurasa wa kumi wa hotuba ya Mheshimiwa Rais alizungumzia suala la Zanzibar kwa kifupi sana kana kwamba si jambo muhimu sana. Naomba ninukuu sehemu tu:-
“Mheshimiwa Spika, aidha, kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wadau wa siasa hususan vyama vya CUF na CCM, tutahakikisha majaribu ya kisiasa yanayoikabili Zanzibar yanamalizika kwa usalama kabisa”.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya neno hili alilolisema Rais mpaka leo hii Mheshimiwa Magufuli hajasema tena neno lingine lolote linalohusiana na Zanzibar, hajasema! Ameishia kuwaalika Ikulu baadhi ya viongozi na pale alipokuwa akitoka hakuna lolote alilolizungumza
kuweka njia ya kuonyesha kwamba analichukulia uzito suala la Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka nieleze sisi ni wawakilishi wa wananchi. Mimi kabla ya kuja hapa Bungeni nilikutana na wananchi wangu wa Jimbo la Konde na kimoja walichotaka niseme nitakisema hapa bila kujali kwamba litawapendeza au litawakasirisha.
Sikuja hapa kwa mapenzi ya yeyote, nimekuja hapa kwa mapenzi ya Mungu kwa uwakala wa watu wa Konde. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mnaposimama mkasema kwamba uchaguzi wa Zanzibar, wengine wamesema hapa, utarudiwa tarehe 20…
MHE. KHATIB SAID HAJI: Tulieni mgangwe maradhi si kitu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tujiulize hao waliosimamia hilo waliapa kutii Katiba wanarudia uchaguzi, Tume ya Uchaguzi, Jecha alipofuta uchaguzi ule alifuta kwa aya ya ngapi ya kanuni na sheria za nchi hii?
MHE. KHATIB SAID HAJI: Akamuulize, nitawauliza ninyi mliomuweka. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, alivunja sheria za nchi, mtu anayestahiki kuweko gerezani, Magufuli anakwenda Zanzibar kwenye sherehe za Mapinduzi anakaa ubavuni kwake, anatujojea Wazanzibari. Tunasema haki itasimama kuwa haki hata mfanye nini hamtaipinga.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, anayepigwa, anayedungwa sindano kila mmoja anahisi maumivu anayopata mdungwa sindano lakini tako linalodungwa sindano ndiyo linaloathirika zaidi na maumivu ya sindano hiyo.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Spika, mambo ya Zanzibar yanachukuliwa kiutani, mnalifanyia jambo hili utani ndugu zangu. Ni wajibu tujue kwa mfano Jimbo langu la Konde uchaguzi uliopita CCM mlipata kura 700 mwaka huu mmepata kura 500.
Kwa mujibu wa sensa Jimbo lenye wananchi 50,000, CCM wako mia tano. Leo mnapofanya masihara ya kusema kwamba uchaguzi unarudiwa, kwa wana CCM 500 walioko kwenye Jimbo la Konde mnatutakia amani kweli ninyi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliangalia jambo hili kwa ujumla wake. CCM katika Kisiwa cha Pemba hakuna, vurugu ikianza wale watu hata tukisema nyumba kumi zizunguke nyumba moja, haiwezekani hawatafika popote. Msiweke mazingira ya kuitia nchi ile kwenye joto la uhasama na uuwaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mwalimu Nyerere aliwahi kunukuliwa katika miaka ya sitini akiwa Marekani au Uingereza, akisema kwamba: “Laiti angekuwa na uwezo angevihamisha visiwa vile vya Zanzibar vikawa mbali na Bahari ya Hindi kwa sababu anahisi vitakuja kutuletea
shida hapo baadaye”. Mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hilo halikuwezekana. Nawauliza CCM mliobakia, nia yenu sasa ni kutuua Wazanzibar wote ili lengo lile mlilolikusudia Wazanzibar wasiwepo duniani mlitimize?
Kama lengo si hilo, kwanza kabisa nachukua nafasi hii nikiwa mwakilishi wa wananchi wa Konde na Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuziomba Jumuiya za Kimataifa, walioshuhudia ukweli na uhalali wa kazi waliyoifanya Wazanzibar ya kuchagua Rais
wanayemtaka walisimamie hili kwa nguvu zao wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo Watanzania wanahukumiwa kwa kukosa msaada wa mabilioni ya shilingi kwa kuwalinda wahuni wa Zanzibar wasiozidi kumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Bunge lililopita, kuna Mheshimiwa Mbunge mmoja, alitamka yafuatayo naomba kunukuu, alisema na akamuomba Rais Kikwete, nia yake ya kuiona Zanzibar inabaki na ustawi ni wakati wa utawala wake tu. La pili..
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. KHATIB SAID HAJI: Ole wenu…
SPIKA: Mheshimiwa muda wako umekwisha, naomba ukae.