Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Savelina Slivanus Mwijage

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu na napenda kumpongeza Katibu wangu Mkuu Maalim Seif kwa kuwa na msimamo wa kukataa kuburuzwa kwenye uchaguzi wa marudio wa Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi napenda nichangie kwenye bajeti hii. Mkoa wa Kagera naona una tatizo kwenye Serikali kwa sababu kila wakipanga bajeti unaangalia huo Mkoa unatupwa pembeni. Bajeti yake ni ndogo sana na matumizi yao ni makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitaanzia kwenye usafiri wa majini, Ziwa Victoria, kila Rais anayeingia kwenye madaraka anaahidi meli mpya, meli tatu mpya, meli mbili mpya mpaka anamaliza uongozi wake anaingia Rais mwingine. Tumekuwa watu wa kujaribiwa kila miaka mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliahidiwa meli na meli tuliyonayo ya Victoria wamepanga bajeti ya kufanya ukarabati. Meli hiyo ni ya miaka, imeshazeeka, hata wakifanya ukarabati siku mbili, tatu lazima yatokee maafa. Kuliko kukarabati, hizo pesa kwa nini wasikusanye wakawaletea meli mpya ya kuweza kuwasaidia ili isiwe mitego ya kuwa watu wanadumbukia kwenye maji mara kwa mara?
Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye kilimo. Mkoa wa Kagera kilimo chetu hasa ni ndizi na kahawa na ndizi ni zao la chakula na la uchumi, sasa hivi zao hili limekuwa na matatizo. Halmashauri nyingi ziliandika barua na kuomba Serikali kuwasaidia kuwaletea wataalam wa kutibu ugonjwa ambao umeleta madhara, kwa kweli miaka miwili inayokuja mbele watu watakufa na njaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kahawa ni zao kuu ambalo sisi toka tumezaliwa tumekuta ni zao kuu la kiuchumi. Ukiangalia Uganda hilo zao lina bei kubwa lakini Mkoa wa Kagera zao hili limerudi chini. Inafika mahali watu wanakata miti ya kahawa na kuifanya kuni kwa sababu hawana faida nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye barabara. Fedha ya barabara inayotengwa ni ndogo kweli lakini ukiangalia ni barabara ambazo zina fursa ya kuingiza uchumi katika Mkoa wetu, imepakana na Uganda, Rwanda na Burundi. Ukiangalia barabara ya kutoka Kayanga kwenda mpaka Kyerwa, Karagwe ni barabara ya vumbi miaka nenda miaka rudi, hawakumbuki hata kuwatengenezea barabara lakini tukija humu ndani tunauingiza ushabiki wa vyama bila kuwafikiria watu wetu wanapata shida. Ukiangalia barabara ya kutoka Kanazi kwenda mpaka Katoro, kuzunguka kwenda mpaka Kyaka, ni barabara nzuri ambayo ina fursa nzuri ya kuzalisha uchumi katika mkoa wetu lakini mpaka sasa hivi Serikali haijagusa hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Jimbo la Bukoba Vijijini wana tatizo la kivuko na nimepiga kelele hapa kuanzia mwaka 2006. Mara kwa mara kivuko kilichopo kinakwama katikati ya maji na watu wanapata shida. Niliiomba Serikali angalau wawaletee kivuko hata kama kimetumika lakini kiwe na uimara siyo mara kwa mara kuwa kinatengenezwa, watu wanapata shida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi kwenye maji. Mkoa wa Kagera umezungukwa na mito mingi lakini akina mama wanapata shida ya maji. Unashangaa ukienda sehemu za Katoro, Karagwe, wanakunywa maji ambayo rangi yake utafikiri wameweka maziwa, lakini tukija hapa tunashabikia kuzomeana hatukumbuki watu wetu tuliowaacha nyuma wana matatizo makubwa. Akina mama wanapata shida, wanatembea zaidi ya kilometa 20, zaidi ya kilometa 50 wanatafuta maji. Ukienda pale mgeni wakikuletea maji utafikiri wamekuwekea maziwa kumbe ni maji ya kunywa lakini tukija hapa kazi ni kelele ya upinzani-upinzani, tunasema kitu ambacho kinatusaidia na sisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye usafiri. Sisi Mkoa wa Kagera usafiri ni wa matatizo, mabasi yakishaharibika huku ndiyo wanatuletea kule kama nilivyosema kwenye meli. Sasa ni lini Serikali itaona umuhimu angalau wa kututengenezea bandari mbili, Bandari ya Kemondo na Bukoba Mjini kwa sababu bandari iliyopo ya Bukoba Mjini ilikuwa inaingiza meli kutoka Bukoba inabeba mizigo inapeleka Uganda, inatoka Uganda inapeleka Mwanza inakwenda Musoma, leo hii hakuna.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali hii inafanya mpaka mkoa wetu ushuke kiuchumi, Serikali ituangalie. Mara kwa mara watu tunakuja hapa tunapiga kelele, mimi nawaeleza Wabunge wa Mkoa wa Kagera, tukae pamoja tuangalie fursa za kuweza kutusaidia katika Mkoa wetu, vyama tuweke pembeni tuangalie fursa za mkoa wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri kuna wizi ambao hata pesa hizi zilizopangwa shilingi milioni 50 hazitafanya chochote bila kuwa na mikakati. Mfanyakazi wa Halmashauri anaiba pesa wanambadilisha hapo hapo wanamweka Wizara nyingine lakini anapokwenda kule anaendelea kufanya mambo kama hayo, kwa nini asifukuzwe? Mtu anakaa Halmashauri mpaka miaka 10 bado yuko Halmashauri. Anafanya kazi kwa mazoea, anafanya kazi kwa kujua hakuna mtu wa kufanya kitu chochote kwa sababu analindwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Muleba kuna mkandarasi ambaye alisimamishwa kazi na Mheshimiwa Mwanri, aliyekuwa Naibu Waziri wa TAMISEMI lakini mpaka sasa hivi huyo huyo ndiyo amepewa kazi kwa sababu ana ushirika na mtu wa Chama cha Mapinduzi, anamkingia kifua aendelee kupewa kazi. Hatutakwenda kwa sababu pesa zinatengwa hapa kwenda kufanya kazi lakini tunaendelea kuweka mtu ambaye ana makosa na alishasimamishwa asiendelee kufanya kazi. Tunaomba haya tunayoyaongea na kushauri sisi wapinzani muwe mnayaangalia, siyo yote yanakuwa mabaya. Tunaishauri Serikali ili ikafanye kazi vizuri siyo tusimame hapa tuanze kuimba ngonjera ya vyama, kitu kilichotuleta hapa ni kuwatetea wananchi ambao ni maskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wetu hawana uwezo wa kununua dawa. Anakwenda hospitali anaandikiwa dawa anaambiwa akanunue, pesa atatoa wapi? Kuna wazee ambao hawana uwezo, wanasema wazee watatibiwa bure, mimi sijawahi kuona wazee wanaotibiwa bure, anapanga foleni kama mimi, mzee anafia pale pale barazani hata kidonge hajapata. Naiomba Serikali kama wazee wanatibiwa bure wapewe bima za afya na watengewe dirisha lao ili wawe wanapata matibabu stahiki kwa sababu hawana pesa ya kununua dawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakwenda kwa wagonjwa walioathirika na UKIMWI. Tunaomba Serikali, kwa sababu inaonesha inawapa hata chakula, ni masikitiko makubwa, nilikuwa nashauri hata kwenye Kamati yangu, mtu anakwenda pale ameathirika badala ya kumweleza mapema kabla hajapimwa, anapimwa akirudi wanaanza kumwambia ukijua umeathirika utafanya nini, ukijua unaumwa utafanya nini? Mtu anaweza akafia palepale hajafika hata kuchukua dawa wala hajajua kama ameathirika ama hakuathirika. Naomba wale ambao wanawa-treat wale watu wawaeleze mapema kabla hawajaanza kuwaeleza kama wameathirika au hawajaathirika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Kamati tuliomba kwamba pale wanapopewa dawa wawe wanapewa na watu wengine kwa sababu ukiwaweka pale kwenye dirisha peke yao mtu mwingine anaogopa kuchukua dawa abaona aibu! Kwa nini umewatenga na hiyo ni kuwanyanyapaa. Naomba watibiwe na sisi lakini dawa zao zinakuwa zimeandikwa zinajulikana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye elimu. Watoto wa kike wanapata shida na elimu. Nashauri mtoto wa kike akipata mimba aliyempa mimba na yule aliyempa mimba apewe adhabu. Siyo msichana peke yake anapata mimba anarudi nyumbani anakaa chini kijana anaendelea na masomo, huo siyo unyanyapaa? Huyo kijana na yeye apewe adhabu ili kama wanapewa adhabu wapewe adhabu wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishie hapo lakini haya niliyoyaongea hapa naomba ushauri wangu ufanyiwe kazi na Mheshimiwa Waziri.