Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nawapongeza sana kwa utendaji mwema, pamoja na changamoto kadhaa kama vile rasilimali watu na fedha kwa ujumla mnafanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Spika, nina mchango katika maeneo yafuatayo; kwanza ni kuhusu kulegeza masharti kwa watumishi wanaokaimu.

Mheshimiwa Spika, wapo watumishi ambao wanakaimu kwa dokezo na sio kwa barua ile ambayo inatoka Utumishi. Kwa mfano nina mwanasheria katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga, yeye alikuwa mwalimu akasoma sheria, na amekuwa msaada katika Halmashauri. Kwa mfano Mafinga TC imetokana na kugawanywa kwa Halmashauri mama ya Mufindi, bahati mbaya sana japo ndio utaratibu katika kugawana mali na madeni, Mafinga TC ilirithi migogoro mingi ya ardhi kutoka Halmashauri mama ya Mufindi ambayo ilikuwa migumu sana. Ni kweli kwamba ni wajibu wa mwanasheria kutetea kesi za Serikali/Halmashauri, hata hivyo ameshiriki kuokoa Halmashauri kulipa mamilioni ya fedha ambayo ni kutokana na kesi za madai ya migogoro ya ardhi ambayo tulirithi kutoka Halmashauri mama ya Mufindi. Mwanasheria huyu alifanya kazi bega kwa bega na mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kesi za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Mheshimiwa Spika, kwa vipindi vifupi tuliletewa mwanasheria kamili kuwa Mkuu wa Idara lakini hakukaa sana, kwa hiyo katika kipindi cha miaka takribani nane kutoka Julai, 2015 mwanasheria huyu amefanya kazi kwa miaka zaidi ya sita akiwa ni Mwanasheria Daraja la II.

Mheshimiwa Spika, ninaleta hoja hii kama case study ya suala la watumishi wanaokaimu kwa madokezo na hususani wale ambao wametokea katika kubadilishwa kada kwa maana ya recategorization.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa kuwa mtumishi wa aina hii na wote wa aina, wamethibitisha uwezo katika kazi na kwa kuwa walishakuwa watumishi, napendekeza moja; wafanyiwe mserereko ili kuwasogeza kwenye ngazi ambayo wanaweza walau wakawa wanakaimu sio kwa dokezo bali kwa barua rasmi kutoka Utumishi, nasisitiza hili la Mwanasheria wa Mafinga TC nimelitumia kama mfano.

Mheshimiwa Spika, pili, kuwaachia mshahara binafsi watumishi waliofanyiwa recategorization; ninashauri, pale ambapo mtumishi amekidhi vigezo na kufanyiwa recategorization, nashauri ikiwa alikuwa amefikia TGS F kwa mfano lakini baada ya recategorization akarudi katika kada mpya kwa kuanzia daraja la kuingilia ambapo mara nyingi ni daraja la pili la kada husika, mshahara wake ubakie TGS F kuliko kurudi TGS D. Hii itasaidia sana kuwapa morali watumishi.

Mheshimiwa Spika, tatu, wastaafu kulipwa kwa wakati; lipo tatizo kubwa kwa watumishi wanapokaribia kustaafu au wakishastaafu hasa walimu. Kuna hali fulani kama ya kuwa desperate mtu anapoingia hatua ya kustaafu, wanakuwa na hofu kubwa, stress na mashaka kwamba je, nitalipwa kwa wakati au nitacheleweshewa kama mwenzangu fulani.

Mheshimiwa Spika, suala hili lipo zaidi kwa walimu, kiasi Mbunge kila mara unapokea simu au ghafla mwalimu mstaafu anakupigia anakuambia nipo Dodoma naomba nikuone nimekuja kufuatilia suala la mafao. Mara nyingi wakienda kwenye mifuko hupewa majibu mapokezi kwamba jambo lako linashughulikiwa, hii anaweza kujibiwa mara kadhaa na baadae anakata tamaa, anafunga safari anakuja Dodoma. Hili hujitokeza mara nyingi kama kwa mfano, kuna michango haikuwasilishwa kwa wakati, hufikia hatua mstaafu kuamua kujilipia ile tofauti kusudi tu mafao yake yawe processed. Nashauri tuwe na utaratibu mzuri zaidi wa kuandaa mafao ya wastaafu wetu kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.

Mheshimiwa Spika, angalizo; nashauri suala la ajira libakie huko huko na kwa mfumo huu, suala la kusema mnagawa nafasi kwenda kwenye majimbo ni hatari, ni ugomvi kwetu Wabunge, fikiria jimbo lipate nafasi 20, wahitaji wako 200, wakikosa 180 lawama kwa Mbunge, sisi tubaki na kazi ya kushauri.