Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Azza Hilal Hamad

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia hotuba ya Wizara ya TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu muweza wa yote. Amenipa afya njema na hatimaye kusimama katika Bunge lako Tukufu. Kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kuchangia katika bajeti hii, natumia fursa hii kuwashukuru wanawake wa Mkoa wa Shinyanga kwa kuniamini kwa mara nyingine kuweza kuwatumikia. Nawaahidi sitowaangusha kama kawaida yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Magufuli. Mheshimiwa Rais hongera sana pamoja na Baraza lako la Mawaziri, chapeni kazi, tuko bega kwa bega na ninyi mpaka kieleweke. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nijielekeze katika hotuba ya Waziri wa TAMISEMI. Ukurasa wa 65 anasema ujenzi wa miundombinu ya Mikoa na Wilaya mpya. Baada ya kusoma hotuba ya Waziri wa TAMISEMI nimesikitika sana kwa sababu maeneo ambayo yanatazamwa ni maeneo mapya ya utawala, wakati kuna maeneo yaliyopo ya zamani hayana miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na mfano wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ni Halmashauri mama kwa Mkoa wa Shinyanga, ni Halmashauri ambayo imezaa Wilaya zote na Halmashauri zote za Mkoa wa Shinyanga. Hivi sasa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga iko ndani ya Manispaa ya Shinyanga, majengo yake yako ndani ya Manispaa ya Shinyanga. Halmashauri za Wilaya ya Shinyanga ina Tarafa tatu, Kata 26, Vijiji 126, ina watu laki 355,930.
Mheshimiwa Naibu Spika, lilitoka agizo kwa Mkuu wa Mkoa kwamba tunapaswa kuhamia kwenye maeneo yetu ya utawala, tusifanyie vikao Manispaa ya Shinyanga. Kinachonishangaza unapotuambia tuhamie kwenye maeneo yetu ya utawala hatuna chumba hata kimoja cha ofisi, vikao vyote vya Baraza la Madiwani kwa sasa hivi vimehamia eneo moja la Iselamagazi ambapo ndiyo tulitenga kuwa Makao Makuu ya Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafanyia wapi vikao vyetu? Tunafanyia kwenye majengo ambayo ni ujenzi wa hospitali ya Wilaya. Inasikitisha na inakatisha tamaa, kama tunasema tunataka kupunguza matumizi, unapunguzaje matumizi kwa kuondoa gari za Halmashauri zaidi ya sita kutoka Manispaa ya Shinyanga halafu zikafanye vikao zaidi ya kilometa 80, hayo matumizi unayapunguzia wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Waziri wa TAMISEMI aliangalie hilo. Hoja siyo kuangalia maeneo mapya, angalieni na maeneo ambayo ni ya muda mrefu ambayo yanahitaji miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kulisema hilo, naomba sasa nijielekeze upande wa afya. Nimepitia bajeti yote ya TAMISEMI katika vitabu vyote lakini sijaona, Mkoa wa Shinyanga tuna ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, sijaona tumepangiwa kiasi gani cha fedha. Siku zote nimekuwa nikisimama humu ndani nasema hospitali ya Mkoa wa Shinyanga ina msongamano mkubwa wa wagonjwa, ukizingatia Wilaya zetu zote hazina hospitali za Wilaya isipokuwa Wilaya ya Kahama. Nilitegemea basi katika bajeti hii nitaona bajeti ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, lakini sijaona! Kama ipo naomba Waziri uniambie iko wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini gharama yake ni zaidi ya bilioni 10. Toka ujenzi huu umeanzishwa kwa nguvu za wananchi, Serikali imechangia milioni 270 tu mpaka hivi tunavyoongea, bado mnatuambia turudi kwenye maeneo yetu ya kazi, tunarudi kwenda kufanya kazi gani wakati hata miundombinu haituruhusu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunategemea nini iwapo hospitali hizi hatujazikamilisha, bado naendelea kusema hospitali ya Mkoa wa Shinyanga itakuwa na mrundikano wa wagonjwa kwa sababu hatuzitazami Wilaya zetu, miundombinu yake ikoje na wale ambao wameanzisha ujenzi wa hospitali hizi hamjatutengea fedha hata kidogo. Inasikitisha, naomba mtutazame Mkoa wa Shinyanga na mtazame Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, imeanzisha ujenzi wa hospitali ya Wilaya. Kwa sasa hivi taratibu imeanza kufanya kazi lakini kuna baadhi ya majengo hayajakamilika na Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu imeomba ombi maalum la shilingi milioni 600 angalau kujaribu kusogeza tu zile huduma, sijui ombi hilo mpaka sasa hivi limefikia wapi? Hiyo yote ni kujaribu kuondoa msongamano mkubwa uliopo katika hospitali ya Mkoa wa Shinyanga. Naiomba Serikali, Mheshimiwa Waziri namwomba sana atutazame kwa jicho la huruma Mkoa wa Shinyanga kwa sababu hatuwatendei haki wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, maombi yanayotakiwa katika hospitali ya Wilaya ya Kishapu ni bilioni tatu, lakini tumeomba milioni 600, sijui imefikia wapi, nitaomba majibu Waziri utakapokuwa umesimama.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kuishauri Serikali, huu utaratibu wa kila mwaka kuanzisha majengo mapya kama Wilaya imeanza mpya, Halmashauri mpya, mnaanzisha majengo, hebu tuusitishe, tumalize kwanza miradi iliyopo. Hakuna sababu ya kila siku kuanzisha miradi wakati tuna magofu mengi hayajakamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kila ninaposimama humu ndani huwa nasema, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga tuna zaidi ya zahanati 28 ambazo tumeanza kujenga ambazo hazijakamilika. Tuna zaidi ya vituo vya afya nane ambavyo havijakamilika, sijaona kwenye bajeti hii tunafanya nini. Niombe tusianzishe miradi mipya, tukamilishe kwanza ile iliyopo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu wa watumishi katika Wizara ya Afya. Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, mahitaji yake katika watumishi wa afya ni 726, watumishi waliopo ni 227, upungufu ni 499. Tunategemea watu hawa wanafanya kazi kwa kiasi gani? Nawaomba sana tuangalieni muweze kutuongezea watumishi ambapo tuna upungufu mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nielekee upande wa maji. Nasikitika sana Bunge lililopita la mwezi wa Pili Mheshimiwa Naibu Waziri Suleiman Jafo alijibu swali langu la Mradi wa Maji wa Mji Mdogo wa Tinde, alisema ndani ya Bunge kufikia mwezi wa Nne Mradi wa Maji wa Mji Mdogo wa Tinde utakuwa umekwishaanza kufanya kazi, lakini mpaka hivi ninavyoongea hapa mradi haujakamilika na SHIWASA hawajapewa fedha ambayo ilikuwa imebaki. Nawaomba sana mtakaposimama kujibu, Waziri wa Fedha aniambie ni kitu gani ambacho kimesababisha mradi huu ulikuwa ukamilike kutoka 2014 na mpaka leo ni milioni 100 tu inayosumbua ili mradi ukamilike. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo, nijielekeze katika mradi wa TASAF. Mradi wa TASAF wa awamu ya tatu ni mradi mzuri sana, kinachosikitisha Kamati zilizowekwa pamoja na baadhi ya watendaji wanautumia mradi huu kwa kudanganya, kuweka watu ambao hawastahili kupata ruzuku hii. Niombe ukafanyike uhakiki wa kila kaya kwa wale ambao wamechukua ruzuku hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, niwashauri Serikali, Mheshimiwa dada yangu Kairuki, kwa sababu TASAF imeazimia kuwasaidia watu hawa upande wa afya, isiwe ombi, iwe ni sheria kwa watu wote wanaopewa ruzuku kutoka TASAF wakatiwe bima ya afya moja kwa moja na wasipewe zile pesa wapewe huduma ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na Mheshimiwa Subira upande wa Wabunge wa Viti Maalum. Imekuwa ni mazoea Wabunge wa Viti Maalum hawaruhusiwi kuingia kwenye Kamati za Fedha. Ukienda Halmashauri zingine wanaingia. Namwomba sana Waziri Mkuu atuangalie Wabunge wa Viti Maalum, mnatuogopa nini kuingia kwenye Kamati za Fedha? Kila unapokwenda Wabunge wa Viti Maalum hawaruhusiwi kuingia kwenye Kamati za Fedha, naomba sana Wabunge wa Viti Maalum turuhusiwe kuingia kwenye Kamati za Fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kuwaomba Wenyeviti wa Vijiji waweze kulipwa posho ukizingatia asilimia 20 haifiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja.