Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Ndaisaba George Ruhoro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa nami niweze kuchangia kwenye hotuba ya Waziri. Siku ya leo nitazungumzia Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, na nitazungumzia narrative na mkanganyiko uliopo kwenye eneo la maadili, umasikini, uzalendo na utajiri katika Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nimekuwa nikiona mtumishi yeyote wa umma anapotajirika, anapomiliki gari, anapomiliki nyumba, umbea unaanza kwenye maeneo mbalimbali ya kazi. Inafika mahali baadhi ya viongozi, hata Waziri akienda nje ya nchi, akikutana na wawekezaji wakimpenda yule Waziri kwa utaalamu wake na uwezo wake alionao wakataka kuja kuwekeza nchini, hata kama wanataka washirikiane naye, yule Waziri anaruka maili 100. Anaogopa, anajiuliza, hii fedha nikiipata kwa kuwekeza na hawa watu, nitaiweka wapi? Ni kwa sababu kwenye Taifa letu kumekuwa na mkanganyiko kati ya hayo mambo matatu mpaka manne.

Mheshimiwa Spika, wale watu wa Tume ya Maadili ya Utumishi wa Umma, wame-focus mara nyingi kwenye kuangalia properties na kwenye fedha za watu, wakichukulia hicho kama kigezo kikuu cha kujua kwamba huyu ni mzalendo ama sio mzalendo. Sijui hiyo narrative imetengenezwa kuanzia mwaka gani? Inafika mahali mtu kuwa na mali, kuwa na utajiri anakuwa na msongo wa mawazo, anawaza atauweka wapi.

Mheshimiwa Spika, Taifa letu katika mchakato wa maendeleo na makuzi ya Watanzania tunapopeleka watoto shuleni, wanakwenda kusoma kuanzia Chekechea mpaka Vyuo Vikuu. Wanasoma, wanamaliza degree zao, wanakuwa na kipindi kile cha kuhangaika kutafuta ajira. Kipindi kile vijana wengi wanakuwa wametawaliwa na mawazo ya ku- enterprise, wanakuwa na startups nyingi sana. Asilimia 99 ya startups nyingi zinafia pale kwa sababu nyingi zinakosa mitaji ya kuziwezesha ili ziweze kukua. Sasa wale Watanzania wachache wanaobahatika, labda ataajiriwa TANESCO, Wizara ya Madini, au eneo lingine, ile knowledge aliyoipata shuleni inamsaidia kupata ajira kwenye ile taasisi ya umma.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuwa ameingia kwenye taasisi ya umma, atafanya kazi miaka mitano mpaka 10, na pale ataweza kupata uzoefu wa kutosha. Eneo sahihi ambalo binadamu yeyote anaweza akawekeza ni eneo lile ambalo amelifanya kazi na amelisomea. Sasa Watanzania kwa hizi sheria zetu tulizoziweka za Tume za Maadili ya Viongozi wa Utumishi wa Umma, wanapoanza kuwekeza siku ile ile tu amejenga kakibanda, umbea unaanza. Ataandikwa kila sehemu, atashtakiwa kwa bosi.

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri amejitihadi basi kwenye zile fomu zetu tunazozijaza kila mwaka za maadili ya viongozi, awe ameandika nina nyumba mbili, nina viwanja viwili, basi nimenunua na Subaru. Sasa figisu zitakazoanzia hapo, pamoja na ku-disclose ile, pamoja na ku-declare kwamba mimi pamoja na kwamba ni mtumishi wa TANESCO ninamiliki hiki na hiki na hiki kinachofanana na yale ninayoyafanya. Bado figisu ni nyingi, ni nyingi tena huyo ndio asahau kabisa hata kuja kupandishwa cheo. Kwa sababu ataonekana sio mzalendo, ataoneka huyu mtu hana maadili, ni mwizi.

Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine tunataka Taifa letu liendelee, tunataka Watanzania wawekeze, tunataka Watanzania wawe na mali, tunataka makampuni ya Watanzania, tunataka tutoze kodi. Sasa hii confusion mimi huwa najiuliza, ni lazima ifike mahali kama Taifa tuweke mipaka ya definition ya conflict ya interest. Mwisho wa siku
tunajikuta sheria tunazoziweka kama Taifa zinakuja kuwabana Watanzania na watu wanashindwa kuwekeza kwenye Taifa lao.

Mheshimiwa Spika, nimeona hii Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma wamekwenda mashuleni, wanaanzisha club za wanafunzi, wamekwenda huko kwenye sekondari na shule za misingi, sijui wanawafundisha vitu gani kule. Maana unaweza ukakuta confusion ya narrative tuliyoanza nayo kwenye enzi zile pengine ni wakati wa ujamaa bado wanaiendeleza. Mimi ningejua kama wanakwenda kwenye ile shule ambako kuna mwanangu Ndairagije na Irakoze ningewaondoa pale ningewapeleka shule nyingine. Wasiwapelekee confusion hiyo.

Mheshimiwa Spika, matarajio yangu ni kwamba hawa watu wanavyofundisha maadili ya umma, basi wafundishe na Watanzania kujifunza kuwa na kiu ya kuwekeza, kutunza mali, ku-enterprise ili Taifa letu na sisi tuwe na mabilionea ambao ndani ya Afrika watasikika na ndani ya ulimwengu watasikika wanaotoka Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kama kweli tunaenda kuwapitishia bajeti na wameshaanza kazi ya kwenda mashuleni kwenye sekondari na shule za msingi kufundisha watoto wetu, naomba kabisa waende watengeneza mtaala mzuri unaochanganya maadili, uzalendo na utajiri. Isifike mahali kwenye Taifa letu mtu akiwa na hela kidogo anajiuliza Mungu wangu, nitazificha wapi?

Mheshimiwa Spika, hawa watu wanapokuja kwako, siku wakigundua kuna ka-issue ama labda kuna kiwanja kimoja ulikisahau, yaani wanakuja kama Polisi, as if gereza liko mlangoni kwako, kesho wanakufunga. Nilitarajia hawa wenzetu wawe facilitative, yaani wawe engaging, waende kuwa-engage Watanzania, umepataje hii? Okay ulipata vizuri, endelea kuwekeza na vitu vya namna hiyo.

Mheshimiwa Spika, sasa imefika mahali kwenye Taifa letu kwa kweli Watanzania wengi wanaishi kwa uoga, wale walioko kwenye Ofisi za Serikali ni waoga, hata Mawaziri wenyewe. Mimi nilitarajia kwenye Taifa letu tuwe na Mawaziri wanamiliki hata ndege, sasa sijawahi kusikia hata Waziri mmoja hapa anamiliki ndege. Ni waoga! Nilitarajia kwamba kwenye Taifa letu tuwe na Mawaziri ambao akienda nje kweli ametumwa na Serikali kwenda kufanya kazi hii na hii; pia ni expert kwenye eneo lile, watu wanapenda kufanya nao partnership, joint venture, lakini wote ni waoga. Sasa matokeo yake ni kwamba tunajinyima fursa. Kama mtu anataka kufanya partnership, sheria zetu zinatubana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba hii ofisi ya masuala ya Utumishi na Utawala Bora waende waangalie kwa kina haya masuala ya maadili, uzalendo, umaskini na utajiri. Waangalie confusion inatoka wapi? Watusaidie huko mashuleni wanakokwenda kuwafundisha watoto wetu masuala ya uzalendo, wakajifunze masuala ya kuwekeza, masuala ya kuweka akiba, masuala ya kutunza; yaani wawe na kiu ya kuwa matajiri. Hii narrative ya kuonesha kwamba mtu ukiwa na mali ni fisadi; yule ni fisadi yule, yule ni mwizi, ona sasa ameanza kuwa na kitambi, mwizi yule! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda kote Tanzania, vijiweni wapi, mtu yeyote, tena baadaye wanavuka wanasema, aah, yule ni Freemason. Kwa hiyo, tumekuwa na narrative ambayo kwa namna moja inaturudisha nyuma. Kwa unyenyekevu mkubwa, nimalizie kwa kusema kuwa, naomba watu wa Utumishi na Utawala Bora watutengenezee mtaala unaohamasisha utajiri ndani yake.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa. Naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)