Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Pauline Philipo Gekul

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niweke mawazo yangu katika hoja ambayo iko mbele yetu. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kutupa afya njema ili tuendelee kutekeleza wajibu wetu ambao Watanzania wametukabidhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najielekeza katika suala zima la ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Jambo la kwanza ambalo Serikali imeona na naomba ninukuu na hili jambo limenishtusha. Ukurasa wa 22 katika kitabu cha Hotuba ya Waziri, anasema kwamba; “Mapato yote yatakusanywa na Wizara ya Fedha, mapato ambayo yanatoka katika Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa watatakiwa kuwasilisha mapato yote yatakayokusanywa yawasilishwe kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali na yatagawiwa kulingana na bajeti za mafungu zitakazoidhinishwa.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo ni kubwa sana, picha ninayopata hapa Halmashauri zetu zitakufa. Amesema mapato yote na kimsingi ukiangalia tunakwenda kuua Serikali za Mitaa. Leo tutakusanya mapato ushuru wa stendi, wa wafanyabiashara, chochote ambacho Halmashauri zetu wanakusanya tuweke kwenye Mfuko wa Serikali. Tukumbuke historia ya ugatuaji madaraka katika Serikali zetu (decentralization).
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1982 Baba wa Taifa alijuta tulivyofuta mfumo mzima wa Serikali za Mitaa; barabara hazikwenda, hospitali zilikuwa mbaya na mwaka 1980 wanakumbuka wale waliosoma historia, kwamba ilifikia hatua hata outbreak ya cholera ilishindikana kuzuiwa huko chini kwa sababu kila kitu kilifanywa na central government.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunarudi kule ambako Muasisi wa Taifa hili aliona kulikuwa na tatizo na alijutia na akasema hili jambo halitojirudia tena. Serikali hizi za Mitaa wamepewa mamlaka kwa mujibu wa Sheria zetu za mwaka 1982. Wana mamlaka ya kuajiri, mamlaka ya kukusanya mapato na kuyatumia kwa kiasi fulani, lakini wana mamlaka pia ya kutunga sheria mbalimbali ambazo zinasaidia katika kukusanya ushuru huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unapotaka pesa zote katika nchi hii tukusanye at central level, halafu tutengeneze bajeti zetu huku chini, tupeleke Serikali Kuu wao ndiyo waanze kutupimia, athari yake ni nini? Athari yake tutaua morali ya wale wanaokusanya hizo kodi ndogo ndogo huko chini, kwa sababu maendeleo hayataonekana; kutakuwa na ubaguzi wa kupeleka fedha hizo katika Halmashauri hizo, japo watu wengine wanakusanya, lakini pia hapatakuwa na maendeleo huko chini kwa sababu fedha haziendi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwe wakweli; ukiangalia bajeti ya Serikali kwa muda mrefu, fedha za own source katika Halmashauri zetu ndiyo zinasaidia miradi ya maendeleo mbalimbali, miradi midogo midogo. Hizo fedha ndiyo zinasaidia kuchonga barabara zetu, lakini angalia fedha zinazotoka Hazina haziendi kwenye Halmashauri zetu kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, angalia kwenye bajeti ya mwaka jana, mwaka juzi, hata katika hivi vitabu, inaonyesha fedha za wafadhili ndiyo zinakuja kuliko fedha zinazotoka Hazina. Nitoe mfano, katika Halmashauri yangu ya Mji wa Babati, 11% tu ya fedha za Hazina ndiyo zimeingia na ni miaka yote fedha zinazotoka Serikali Kuu haziingii. Kwa kubariki kila kifanyike at central level, huku chini watu wakusanye tu halafu watu wachache wapange, tupeleke sehemu fulani, tusipeleke sehemu fulani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo nakuhakikishia tunaua Halmashauri zetu, hakuna maendeleo yatafanyika, mtafanya mambo yenu makubwa makubwa katika central level, lakini yale yanayohusu maslahi ya wananchi wa hali ya chini na maendeleo yao nakuhakikishia tunarudi kwenye historia ya mwaka 1980 ya jinsi ambavyo decentralization, Baba wa Taifa Mwalimu aliona kwamba ni jambo muhimu sana kwa sababu central level hawawezi kufanya wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati pia imebariki kwamba hizo sheria ziangaliwe, maana yake Sheria inayotajwa ni mwaka 1982 ya Serikali za Mitaa, kwamba sasa tunachukua uhuru wa Serikali za Mitaa kukusanya kodi zao na kuzifanyia matumizi, Serikali Kuu ndiyo inafanya. Naomba Bunge hili tusithubutu kufanya hivyo, bali tusaidie Serikali za Mitaa kubainisha vyanzo ambavyo hawakusanyi, tuviimarishe na Sheria hizo ziimarishwe badala ya Serikali kuu kuchukua madaraka yote. Sasa tunakusanya kila kitu at central level, hatuwezi tukapitisha kitu kama hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano wa retention premium ya ardhi 30%, hizo fedha huwa hazirudi. Tunauza viwanja huko, tunapeleka makusanyo yote ardhi, Wizara ya Ardhi hawapelekewi hizo pesa na Wizara ya Ardhi wao wakipata chochote na wanajitahidi chochote wanachopata kutoka Hazina wao wanapeleka 30% katika hizo Halmashauri, lakini Serikali Kuu, Hazina hawapeleki hizo fedha hata hiyo tu premium ya ardhi hawapeleki. Iweje leo tuwapelekee eti fedha zozote tunazokusanya kwenye Halmashauri zetu, tupeleke kwenye Serikali Kuu. Tunaua Halmashauri zetu na maana yake tunaua suala zima la Serikali hizi mbili Serikali Kuu na Serikali za Mitaa, wanataka sasa kila kitu wafanye wao. Hiki kitu Bunge hili tusifanye vinginevyo maendeleo yatakwama katika Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la service levy. Wamezungumza hapa ushuru wa huduma na vitu kama hivyo. Kwa muda mrefu tumeishauri Serikali, suala la mitandao ya simu ni chanzo kimojawapo katika Halmashauri zetu. Leo mitandao hii wamiliki wa makampuni haya ya simu ushuru wa huduma wanaolipa haueleweki kwa sababu Halmashauri imefikia hatua wanakusanya sijui ushuru wa nguzo, sijui service levy, hiyo asilimia zero point three Wizara ya TAMISEMI mwaka jana na Wizara ya Mawasiliano walikaa chini wakasema watashauriana na wakaandikiana barua kwamba wakusanye katika central level. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pata picha mpaka leo hawajawahi kukaa, hawajawahi kupeleka kwenye hizo Halmashauri kwamba ni kiasi gani wanastahili kupitia kwa makampuni haya ya simu, hata hilo kama tulishindwa, tunathubutuje leo, eti kwenda kuchukua hata vile vyanzo ambavyo kidogo tunajitahidi Halmashauri zetu zinakusanya, lakini sisi at central level kitu ambacho Wizara mbili walitakiwa wakae wa-reconcile wapi ambapo haya makampuni hayalipi, halafu zile asilimia zigawanywe zipelekwe kwenye Halmashauri zetu equally hawapeleki.
Leo tunaua Halmashauri zetu tunasema tunafanya sisi, wakati ya premium ya ardhi mmeshindwa, hii service levy mmeshindwa, halafu Serikali Kuu, hivi kweli hiki kiburi kinatoka wapi cha kusema kwamba, sasa ninyi mnakusanya, halafu mtugawie sisi tuwaletee tu bajeti. Hili ni jambo kubwa sana na ninaona kama hatujalipitia na hatujalielewa vizuri, lakini kama tukipitisha jambo hili ambalo linapendekezwa katika ukurasa wa 22, tumeua Serikali zetu za Mitaa totally.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisisitize sana kuhusu hili tusilipitishe na tuliangalie kwa upya, lakini suala zima la kurasimisha biashara zetu ni kwa nini sijaona Mpango unaoonesha vijana wetu ambao wanafanya biashara ndogo ndogo waweze kuboreshewa maeneo yao. Kwa muda mrefu hata kwenye Hotuba ya Rais alizungumzia suala zima la kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara kwa vijana wetu, Wamachinga. Hawa wakipangwa pesa zikatengwa, zikajengwa shopping malls ambazo zitasaidia vijana wetu tukawapanga, watalipa ushuru katika Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotokea leo, hawa wafanyabiashara wanaokuwa taratibu, hawajawahi kupangwa kokote, hawajawahi kutengewa maeneo, lakini kingekuwa ni chanzo kizuri ambacho tukakaa tukawaangalia jinsi gani Serikali za Mitaa wakapanga maeneo kwa ajili ya hawa vijana, wakafanya biashara wakalipa ushuru mbalimbali na tozo mbalimbali, itasaidia sana kuongeza mapato ya Serikali. Kwa hiyo, nishauri kwamba inawezekana Serikali inawaza mambo makubwa, bandari, sijui ndege, sijui vitu gani wakati kuna watu ambao wakipangwa tu wanaweza wakasaidia kuleta marejesho katika Mfuko wetu na katika Halmashauri zetu ili tuone ni jinsi gani ambavyo tunaweza tukafanya maendeleo zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la viwanda vidogo vidogo ambavyo vinaweza vikaajiri hawa vijana, limezungumziwa lakini…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa
muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Muda wako umekwisha.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.