Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Kwanza nitoe pongezi kubwa sana kwa Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Naibu Waziri, lakini vile vile naipongeza Idara ya Magereza na Idara ya Uhamiaji kwa kazi nzuri wanayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nalipongeza Jeshi la Polisi kwa ujumla kwa kulinda amani na kulinda raia na mali zao hasa wakati wa uchaguzi uliopita huku Bara na uchaguzi ule wa marudio wa Zanzibar baada ya Mheshimiwa Jecha kuufutilia mbali uchaguzi wa awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo naomba niongelee suala la kurasimisha Sekta ya Ulinzi binafsi. Sekta hii ya Ulinzi inafanya kazi nzuri sana sambamba na Jeshi la Polisi. Wako Askari wengi sana, lakini naiomba Serikali ilete mchakato wa kuanzisha Sheria ya Ulinzi Binafsi (Private Security Industry Act) pamoja na Sheria ya Kuanzisha Mamlaka ya Sekta ya Ulinzi Binafsi (Private Security Industry Authority)
Mheshimiwa Mwenyekiti, makampuni haya yalianzishwa mwaka 1980 yakiwa mawili tu, lakini makampuni haya yamekua na kuwa makampuni 850 yakiajiri watu zaidi ya milioni moja na nusu kama Askari; lakini yanafanya huduma zifuatazo: ulinzi wa watu (Man Guarding) wanafunga mitambo kama hiyo tunayoiona hapo nje tunapoingilia, vilevile wanafanya upelelezi binafsi na wanafanya kazi ya ushauri (Security Consultancy).
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu makazi yao yanaonekana, iko haja ya kuwatungia sheria. Sasa hivi hakuna sheria yoyote ya Sekta ya Ulinzi Binafsi na kwa bahati mbaya zaidi hata GN ya kuonyesha hii Sekta haipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze pia kutaja matukio ambayo yametokea kwa sababu hakukuwa na sheria. Liko tukio la Temeke pale NMB, ambapo walinzi binafsi waliuawa na majambazi na pia Polisi wakauawa. Sekta ya Ulinzi Binafsi ilipata tabu kujiamini kwa sababu Polisi walisimamia marehemu, yule wa Polisi na kumhudumia na kusahau yule Polisi au Askari wa Ulinzi Binafsi, jambo ambalo lilileta kidogo mkanganyiko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mnakumbuka kesi ya Kasusura, ambapo walinzi walitumwa kwenda kuchukuwa fedha Dar es Salaam, Airport wakaondoka na hizo fedha. Kulikuwa na kesi ya NMB wakati walinzi walitumwa kugawa mishahara, wakaondoka wakawavua nguo wakaacha na masanduku wakachukuwa fedha zao. Kwa hiyo, pangekuwa na sheria wangekamatwa wenye kampuni, siyo wale walinzi walioshitakiwa kwa sababu ya jinai!
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko kesi ya Shule ya Upili ya Tabora Girls, ambapo walinzi waliokuwa wanalinda lindo hilo mchana, usiku wakarudi wakaja wakaiba na bahati mbaya mlinzi mmoja akapigwa na kuuawa pale. Pangekuwa na sheria, mambo haya yasingetokea. Pia walinzi wanashtakiwa wanapoua, wanapopiga majambazi, lakini Polisi wakiua majambazi wanapongezwa. Hawa nao wanafanya kazi ile ile, kwa hiyo, kungekuwa na sheria, wangetambuliwa hao kwamba walikuwa nao wanapigana wakati wanalinda mali za raia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala lingine baya; makampuni haya yalianzishwa mwaka 1980 kwa kupewa vibali, lakini bahati mbaya vibali vile sasa vinakaribia miaka 36 na waliopewa vibali hivyo wameshafariki, wamekufa, hawapo. Watu walioyarithi makampuni yale hawana taaluma kabisa ya Sekta ya Ulinzi Binafsi, lakini bado wanatumia vibali vile kuendesha Sekta ya Ulinzi Binafsi na mbaya zaidi, wana silaha. Kuna kampuni za silaha, mpaka 50, bunduki mpaka 100, mpaka 200 na hawa hawana taaluma yoyote ya ulinzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile napenda kuongelea kwamba kuna dhana tu kwamba inawezekana ziko sheria ambazo zinatumika kulinda au kuendesha Sekta ya Ulinzi Binafsi. Sheria hizi hazipo na imethibishwa kwamba sheria zote ambazo zipo hapa nchini hazikutungwa wala hazikuandaliwa kwa ajili ya kuendesha Sekta ya Ulinzi Binafsi, kwa sababu Sekta hii imeanza mwaka 1980 na Sheria nyingi zimetungwa kabla ya hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizitaje Sheria hizo: Criminal Procedure Act ya Mwaka 1985; Penal Code Cap 16; Law of Contract Ordinance; The Evidence Act ya 1967; Civil Procedure Code ya Mwaka 1966 na; Police Force Ordinance Cap 322.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria zote hizi zinaanza kutumika baada ya sheria inayofikiriwa ipo, kufeli, yaani Sekta ya Ulinzi wanalinda raia na mali zao, likitokea tukio, mali ikapotea au maisha yakapotea ndipo sheria hizi zinakuja kuchukua nafasi yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napendekeza, kwa kuwa makampuni ya ulinzi binafsi yanafanya kazi nzuri sana na kwa upande mwingine yametoa ajira zaidi ya milioni moja na nusu, lakini vilevile kila mahali penye uwekezaji kuna Sekta ya Ulinzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ndani mkishafunga Bunge kuna kampuni za ulinzi zinalinda hapa nje, Wizara zinalindwa, lakini vilevile kila mahali ambako sasa hivi kuna gesi, kuna makampuni ya ulinzi binafsi. Makampuni haya hatuwezi kuyaondoa sasa, lakini tunaweza kuyatungia sheria tuweze kuyadhibiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho yake, aje na mpango au mchakato wa kuanzisha Sheria ya Sekta ya Ulinzi Binafsi. Sekta hii ya Kampuni binafsi na kampuni za ulinzi, tunaweza kuitungia sheria na kuiwekea mamlaka ya kuziongoza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sielewi tatizo ni nini, lakini miaka 25 ambayo nimefanya katika Sekta hii sikuona tatizo. Liko tatizo dogo tu kwamba, baadhi ya Polisi wana makampuni ya ulinzi na hiyo imekuwa inaleta hali ya migongano ya maslahi na wanashindwa kuishauri Serikali kwa sababu na wao ni wadau wa Sekta ya Ulinzi Binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi wengine wa Polisi wanaendesha kampuni za ulinzi na Ma-IGP karibu wote waliopita wana kampuni za ulinzi. Pia wana kampuni za ulinzi, yaani Polisi wengine wapo kazini na mchana ni Maafisa wa Polisi lakini jioni wana kampuni za ulinzi binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wamekuwa kikwazo kutunga sheria na kuanzishwa mamlaka, kila mara wanajitetea kuwa eti Ibara 147 ya Katiba, ibara ya (1) inazuia kutungwa kwa Sheria hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunatunga Katiba inayopendekezwa, tulitafsiriwa nini maana ya majeshi yanayoelezwa katika Ibara ile ya 147 kwamba, majeshi haya maana yake ni majeshi ya JWTZ, Majeshi ya Anga, Majeshi ya Ardhi na Majeshi ya Maji. Siyo idara ndogo ndogo hizi za Sekta ya Ulinzi Binafsi na ndiyo maana Sekta hii imeendelea kuwepo kwa muda wa miaka 36 na hakuna mgongano kati ya yenyewe na Jeshi la Wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ni la maslahi binafsi ya viongozi wa Jeshi la Polisi wenye Kampuni za ulinzi; tuseme sasa basi, miaka 36 inatosha kuendesha nchi na Sekta hii bila Sheria, yaani Private Security Industry Authority pamoja na mamlaka ya kuendesha sekta hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niachie wenzangu waongee, naunga mkono hoja hii moja kwa moja, lakini pia naomba kurasimishwa kwa Sekta ya Ulinzi Binafsi. Ahsante sana.