Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

Hon. Ummy Ally Mwalimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa fursa hii hili niweze kuhitimisha hoja yangu na nianze kwa kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa maoni na ushauri wenu ambao mmetupatia ili tuweze kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa watanzania. Kipekee tushukuru sana maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii chini ya mwenyekiti wetu Mheshimiwa Stanslaus Nyongo kwa kweli wanatupa ushirikiano mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme kwamba maoni na ushauri wa Wabunge tumeuchukuwa na tutaufanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee kwa kweli niwashukuru niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa pongezi ambazo mmetupatia, mmetutia moyo mmetupa ari mmetupa nguvu ya kuendelea kusimamia Sekta ya Afya nchini na ni kweli kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri tuna deni kubwa sana kwenu Waheshimiwa Wabunge tuna deni kubwa sana kwa watanzania na tuna deni kubwa sana kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Spika, tunatambua dhamana kubwa tuliyonayo katika wizara hii, afya ni jambo kubwa afya ni jambo linalomgusa kila mtanzania awe tajiri awe maskini. Kwa hiyo, tunawaahidi Waheshimiwa Wabunge kwamba tutasimamia vyema Sekta ya Afya nchini kuhakikisha watanzania wanapata huduma za afya afya ni mali afya ni mtaji afya ni uchumi.

Mheshimiwa Spika, kipekee nishukuru Wabunge ambao wamechangia tumepata wachangiaji 31 nikiongeza Mheshimiwa Naibu Waziri na Mwenyekiti wa Kamati lakini pia kuna Wabunge kumi wamechangia kwa maandishi na Wabunge saba walichangia wizara yangu wakati wa mjadala wa Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, tuseme kwamba yote ambayo Wabunge wamechangia tutayafanyia kazi na kubwa tumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa maono yake, kwa utashi wake, kwa dhamira yake ya kutaka kuona watanzania wanapata huduma bora za afya, hususan afya ya uzazi mama na mtoto. Kama mtakumbuka Wabunge ambao mlikuwa katika Bunge la kumi na moja, Rais Samia Suluhu Hassan akiwa Makamu wa Rais alijifanyisha kazi usiku na mchana ni kama vile alikuwa ndiye namsaidia kuhusu Sekta hii ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, alikuwa anafuatilia huduma za Afya alianzisha kampeni ya jiongeze tuwavushe salama ili tuweze kuokoa wanawake wajawazito Rais Samia huyu ndiye aliweza kuzindua chanjo ya kuwakinga wasichana dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi, ndio alitusukuma tukapata fedha kutoka Benki ya Dunia kwa mara ya kwanza kujenga Vituo vya Afya vitakavyofanya upasuaji wa dharula ikiwemo kumtoa mtoto tumboni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hayo yalikuwa pia ni maono ya Rais Samia Suluhu Hassan alituwezesha kuzindua pia kampeni ya usichukulie poa nyumba ni choo ambapo pia tunaona sasa kaya za watanzania zina vyoo. Kwa hiyo, suala la afya kwetu sisi tunafahamu kwamba linamgusa kwa karibu sana Rais wetu Samia Suluhu Hassan. Pia ameingia madarakani tumeona fedha nyingi zinaenda kwenye miundombinu kwenye ambulance kwenye watumishi.

Mheshimiwa Spika, kipee pia nimshukuru Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.Mheshimiwa Waziri Mkuu kwetu sisi ni mlezi, mwongozaji, ni mwongoza njia amekuwa akituelekeza usiku na mchana kufanyia kazi changamoto mbalimbali za Sekta ya Afya, Mheshimiwa Waziri Mkuu tunakushuru sana kwa usimamizi wako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge ni nyingi lakini naomba niongee kwa sababu ya muda hoja kama tano au sita ya kwanza ambayo imeongelewa na Waheshimiwa Wabunge wengi ni suala la upatikanaji wa dawa na vifaatiba katika vituo vyetu vya kutoa huduma za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa ufupi ni kwamba hoja hii sisi tutaenda kuifanyia kazi zaidi tumegawanya katika maeneo makubwa matatu eneo la kwanza ni ngazi ya wizara, tutahakikisha tunakata maoteo sahihi ya mahitaji ya dawa na vifaatiba. Kama Jiji langu la Tanga linasema litatumia kwa mwaka kopo za paracetamol 100 kwa hiyo, lazima tutaangalia je wamepata kopo 100 katika kipindi hiki na hii ndio hoja ambayo pia imeangaliwa imesemwa na Waheshimiwa Wabunge kutumia TEHAMA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, TEHEMA itatusaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za afya lakini pia sambamba na maoteo tutasimamia miongozo ya kamati za dawa therapeutic committee mwongozo wa standard treatment guideline wa matibabu ya kitaifa na miongozo mingine. Tunakushukuru sana Mheshimiwa Kingu kwa kuleta hoja ya kuanzisha drug revolving fund kwa kweli hili jambo litasaidia uwepo wa upatikanaji wa dawa katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tutafanya audit ngazi ya pili ni bohari ya dawa MSD kwanza nimeshawaelekeza MSD tutawapima kwa upatikanaji wa dawa za miezi minne na sio mwezi mmoja hili tumewaambia tunataka dawa zote 290 pamoja na vifaatiba vipatikane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hili pia tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa maagizo yake tumeshaanza kuyafanyia kazi sambamba na Mheshimiwa Rais kubadilisha uongozi Mtendaji Mkuu wa MSD pamoja na kumteuwa Mwenyekiti wa Bodi tunawaondoa Wakurugenzi watano wa MSD. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mkurugenzi wa Fedha MSD anaondoka, Mkurugenzi wa Manunuzi MSD anaondoka, Mkurugenzi wa Logistic wa MSD anaondoka, Mkurugenzi wa Sheria wa MSD anaondoka, na Mkurugenzi wa Utawala wa MSD wanaondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tumeshauriwa pia tutaenda kuwaangalia na mifumo supply chain system mifumo ya usambazaji wa dawa ndani ya MSD lakini kubwa tutaendelea kuitaka MSD kununua dawa na vifaatiba kutoka viwandani, kwa kuzingatia mikataba ya muda mrefu. Lakini Waheshimiwa Wabunge naomba niseme jambo moja nimepewa dhamana ya kusimamia sekta ya afya hatuta- compromise ubora wa dawa na vifaatiba kwa sababu tusije tukaenda kuwapa matatizo watanzania kwa kutoangalia ubora wa dawa na vifaatiba kwa hiyo, jambo hili tutalisimamia kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na nimpe pole Mkurugenzi mpya wa MSD umepewa hongera lakini jana nilimwambia una kazi kubwa sana kwa sababu matumaini ya Mheshimiwa Rais ya Wabunge na mimi mwenyewe kwake ni makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tusema Tukai Mavele alikuwa ndiye mshauri wa Serikali kuhusu masuala mazima ya dawa akiwa upande wa ubalozi wa Marekani Mwenyekiti wa Bodi Rosemary William Slaa alikuwa ndio mshauri wa Serikali kwa upande wa Global Fund ambao wanatupa dawa za UKIMWI TB na Malaria. Kwa hiyo, juzi nilikuwa namwambia Mheshimiwa Waziri Mkuu ni sawa Rais amewaambia nyie si mnatukosoa nyie si mnashauri haya sasa nendeni mkafanya hayo ambayo mlikuwa mnayaeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo DG MSD una kazi kubwa na Waheshimiwa Wabunge nataka kusema tumemwambia tunataka ndani ya miezi mitatu dawa zifike katika vituo na hospitali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho katika eneo hili la dawa ni suala la matumizi ya dawa katika ngazi ya hospitali na vituo, MSD anaweza akapeleka dawa lakini je madaktari wetu na wataalam wetu wanazingatia miongozo ya matibabu ya Kitaifa? Kwa sababu ziko taarifa tumezipata dawa ambazo zipo katika hospitali zilizonunuliwa na Mfamasia zilizoagizwa na Mfamasia daktari anaandika dawa zake mwenyewe ambazo ni kinyume na standard treatment guideline kwa hiyo hili tutalisimamia kwa kiasi kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia Waheshimiwa Wabunge mtusaidie mnapokaa kwenye mabaraza ya Madiwani ni lazima tuhoji kamati za afya za kusimamia vituo je zinafanya kazi je zinafuatilia upatikanaji wa dawa. Lakini kubwa kwenye eneo la dawa ni TEHAMA mifumo ya TEHAMA itatusaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha mnyororo mzima wa dawa. Lakini kamati pia imetoa maoni kuhusu matumizi holela ya dawa tutaendelea kuyafanyia kazi eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo pia la mwisho katika dawa tutafufua au kuimarisha uzalishaji wa ndani wa dawa kiwanda cha Keko tutapata fedha tuweze kuwekeza kununua mashine za kisasa na kiwanda kile cha TPI Arusha ambacho pia kimeelezwa na Mheshimiwa Catherine Magige tutahakikisha pia tunapata wawekezaji tayari kesi imemalizika mahakamani TR anafanya mawasiliano tunatafuta wawekezaji waweze kufufua kiwanda kile cha TPI ambacho kipo Arusha pamoja na kuendeleza viwanda vingine vya Keko na Idodi.

Mheshimiwa Spika, suala la Bima ya Afya hili niseme tutaendelea kutoa elimu kuwahamasisha watanzania kuona umuhimu wa kuwa na Bima ya Afya ili waweze kupata huduma za matibabu kabla ya kuugua. Lakini pia tutakamilisha haraka Muswada ule wa sheria wa Universal Health Insurance.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa huduma za kinga Mheshimiwa Shigongo amesema jambo zuri pamoja na Dkt. Paulina pamoja na Mheshimiwa Cecilia Paresso ni kweli ukiangalia hii bajeti tunazungumzia tu tiba tunatakiwa pia ku- foccus kwenye preventive Intervention.

Mheshimiwa Spika, na mimi ndio maana ukiniuliza waziri chagua kipaumbele chako cha kwanza sina hela nitafanya chanjo za watoto kwa sababu ile ni moja ya njia ya kuwakinga Watoto. Lakini Mheshimiwa Shigongo kuhusu homa ini tunakubaliana na wewe kwamba nalo ni janga kwa sababu prevalence ni asilimia 4 kwa hiyo tayari nimeshamwelekeza Katibu Mkuu ule mpango wa Taifa wa kupambana na UKIMWI tunaenda kuubadilisha utakuwa ni Mpango wa Taifa wa kupambana na UKIMWI pamoja na homa ya ini. Kwa hiyo, tunakuwa na integrated programme tutaamasisha wananchi wapime na wapate chanjo ikiwemo kuhakikisha wanapata chanjo kwa gharama nafuu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Furaha Matondo umezungumza saratani ya mlango wa kizazi kwa uchungu mkubwa. Ni kweli ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge katika mikutano yetu saratani zinazoongoza kuwakumba watanzania ni saratani ya matiti na saratani ya mlango wa kizazi kwa hiyo, naomba pia tuendelee kuwaambia wazazi na walezi wawapeleke watoto wetu hasa wa kike kupata chanjo ya kuwakinga na maambukizi ya saratani ya mlango wa kizazi.

Mheshimiwa Spika, suala la kinga pia Mheshimiwa Dkt. Paulina tutaweka nguvu katika environmental health katika usafi na afya ya mazingira hivi kwa nini vijiji vyetu na miji yetu ni michafu, kwa nini kuna mabwana kwa nini hatufyeki nyasi kwa nini hatuwekezi katika kuhakikisha pia tunazingatia kanuni za usafi na afya bora kwa hiyo, ni eneo ambalo tutalipa kipaumbele.

Mheshimiwa Spika, lakini pia suala la kinga amezungumza Muuguzi mzuri Mheshimiwa Tecla NCD (non- communicable disease) ni jambo ambalo linaongezeka kila siku na hela hii ya bajeti Waheshimiwa Wabunge haitatosha hata siku moja kama hatutadhibiti magonjwa yasiyoyambukiza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sambamba na kutoa elimu ya watu kuzingatia ulajji wa vyakula kuwekeza kwenye kupima kuepuka unywaji wa pombe kupita kiasi kuvuta sigara lakini pia tunataka kuhakikisha kwenye zahanati wananchi wanapata huduma za kupima au kufanya uchunguzi ili tuweze kugundua mapema magonjwa haya yasiyo ya kuambukiza.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ukisubiri saratani imefika hatua ya nne hatua ya tatu inakuwa ni matibabu yanakuwa kidogo ni ghali lakini pia hatupati matokeo mazuri. Suala la afya ya uzazi mama na mtoto mdogo wangu Mheshimiwa Husna ameongea kwa uchungu lakini pia mtani wangu Mheshimiwa Kabula pamoja na Mheshimiwa Mabula. Kwanza nataka kusema hatujabadilisha sera ya afya sera ya afya inasema huduma kwa akina mama wajawazito na watoto wa chini ya umri wa miaka mitano ni bure.

Mheshimiwa Spika, nimefundishwa kusema ukweli hiyo sera inatamkwa ni bure kihalisia ni kweli wanawake wengi hawapati huduma za bure kwa ajili ya akinamama na Watoto. Kwa hiyo, hili tunalichukuwa tunafanya calculations kwa mfano mwanamke anapoenda clinic anapoenda kuhudhuria uzurio la kwanza na la pili na tatu na la nne anatakiwa kuangalia wingi wa damu anatakiwa kupimwa urine ili tuangalie kama kuna maambukizi yeyote katika mkojo ili kuhepusha kifafa cha mimba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia shinikizo la damu afanyiwe pia na ultra sound kwa hiyo, tunafanya calculation tuone ni gharama zipi ambazo tunaweza kuzibeba kama Serikali na wananchi tuone ni gharama zipi lakini Bima ya Afya tunaamini ndio itakuwa ndio mwarobaini wa sera hii ya bure au ya msamaha kwa wagonjwa wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini la pili kwa upande wa mama na mtoto ni suala la ubora wa huduma tunakubaliana nanyi Waheshimiwa Wabunge amesema pia Mheshimiwa Paresso kama asilimia 99 ya wanawake wanaenda clinic je wanapata huduma bora na Waheshimiwa Wabunge mimi sina ajenda nyingine nilivyorudi Wizara ya Afya ajenda yangu ni ubora wa huduma na sio bora huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunataka Watanzania wapate huduma bora za afya akifika pale achunguzwe vizuri apate vipimo vyote apate dawa anazohitajika mmesema vizuri Waheshimiwa Wabunge hata ile lugha tu mgonjwa pale tayari ni mgonjwa, anapoenda pale anafokewa ananyanyaswa anasemwa tayari unamwongezea magonjwa kwa hiyo, hili ni eneo ambalo tutalipa kipaumbele.

Mheshimiwa Spika, kwenye hii huduma za afya mama na mtoto Waheshimiwa Wabunge kama alivyosema Naibu Waziri tunawabana wizarani tuna fedha nyingi nataka kukiri sisi Wizara ya Afya tuna fedha nyingi za wadau lakini hatuoni matokeo ya fedha hizo ambazo hizi zinawekezwa tumefumuafumua tumepata NICU (Neonatal Intensive Care Unit) vyumba vya watato wachanga mahututi 100 tunaenda kujenga katika Hospitali za Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia tumepata fedha kwa upande wa Benjamin Mkapa tunakwenda kuanza kujenga Hospitali ya Taifa ya mama na mtoto lakini pia tutajenga hospitali ya saratani, kwa hiyo hili ni eneo ambalo tutalipa kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la afya ya akili Mheshimiwa Jesca Msambatavangu ameongea hapa kama kiutani lakini ni jambo kubwa sana na mimi nimeshawa-challenge watu wangu ni lazima pia tutoe taarifa na kuwekeza katika afya ya akili na bahati mbaya Tanzania afya ya akili tunaichukulia kama criminal issue kama suala la jinai hapana ni suala la afya na hapa tunaweza tukajiona wote tuko sawa lakini afya ya akili ni changamoto kubwa.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Jesca kama utaridhia naomba nimteuwe Mheshimiwa Jesca Msambatavangu kuwa balozi wa Afya ya Akili nchini Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hili jambo lazima tusione aibu kulisema hata nyumbani ndoa divorce frustration ni kwa sababu pia ya afya ya akili, hata huu ukatili nilikuwa naongea na Waziri Gwajima wiki iliyopita hivi baba mzazi unambaka vipi mtoto wako wa miaka minne, mitano kama sio tatizo la Afya ya Akili tumeongea kwa kweli hili jambo tutalipa kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la afya kwa watu wenye ulemavu Mheshimiwa Hadija Taya umeliongea vizuri na hili bahati nzuri nimeshaongea na wataalam wangu nimewaambia taarifa zetu za Wizara ya Afya nataka pia tulipoti kuhusu rehabilitative services huduma za utengamao ikiwemo huduma kwa watu wenye ulemavu. Mheshimiwa Stella Ikupa amekuwa akizungumza huduma za wanawake wenye ulemavu katika kujifungua kwa hiyo tumeshapeleka maombi tunaifumua Wizara ya Afya pia nimesema lazima tuwe na kitengo maalum unit ambayo itahusika na masuala ya rehabilitative services huduma za utengamao ikiwemo huduma kwa watu wenye ulemavu na watoto wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, nimepigiwa kengele ya kwanza niseme tu kuna suala la gharama za kuwaona daktari ni kubwa ni kweli na hata jana nawa-challenge watu wangu tumegeuza hospitali kama vile TRA, hospitali kazi yetu ni kutoa huduma sio kukusanya mapato kwa hiyo, sasa hivi unakuta gharama kubwa na nimemuomba Waziri Mkuu ridhaa ukiangalia mwongozo ule ni wa 1997 nitatoa mwongozo wa kusema zahanati ya kumuona daktari isizidi kiasi gani, Kituo cha Afya isizidi kiasi gani, Hospitali ya Wilaya isizidi kiasi gani Hospitali ya Rufaa ya Mkoa isizidi kiasi gani na Hospitali za Taifa isizidi kiasi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunawaumiza watanzania na ndio maana wanakimbilia kwenda kuwaona waganga wa kienyeji, Mheshimiwa Tabasam pia nimpokea mchango wako wa maandishi gharama za dialysis ni very expensive mtanzania gani ataweza kulipa laki mbili na nusu kwa siku mara tatu ni laki saba na nusu kwa wiki, kwa hiyo, ni eneo hili nalo Rais Samia ameshatuelekeza tunalifanyia kazi na tutahakikisha huduma bora za wagonjwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tunarudi kulekule kabla hujaenda kuhitaji dialysis tunataka tuepuke tujikinge na magonjwa haya yasiyoyakuambukiza watanzania nawaomba sana tuwekeze kwenye afya zetu kwa kujali tunavyokula tujiulize wangapi mmekula mboga, wangapi mmekuala matunda katika wiki hii tumeambiwa angalau bia usinywe nyingi bia mbili tatu kwa siku lakini watu wanapiga mpaka bia 10/15 sigara kupita kiasi, pombe.

Mheshimiwa Spika, muda hautoshi. Nimalize kwa kukushukuru wewe kwa kusimamia vizuri mjadala huu. Narudia tena kwa Waheshimiwa Wabunge, afya siyo jambo la kuchekea chekea, afya ni jambo kubwa. Tunatambua dhamana kubwa ambayo tumepewa ya kusimamia afya za Watanzania.

Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri, amekuwa mwepesi sana wa kufanya ziara katika majimbo, lakini amekuwa mwepesi sana wa kusimamia masuala ninayoyaelekeza. Mheshimiwa Dkt. Mollel nakushukuru sana. Nimshukuru Katibu Mkuu Prof. Makubi pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Shekalaghe pamoja na Mganga Mkuu wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema; samahani mtani wangu Mheshimiwa Kabula na Mheshimiwa Mkundi wa Ukerewe, hii tunavyofumua, fedha ziko Wizara ya Afya. Nataka kuwaambia, fedha zipo. Tunakwenda kununua ambulance boat mbili kwa ajili ya Ukerewe na Mafia ili tuwezeshe pia rufaa za wagonjwa katika maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, nimeshamwelekeza Katibu wangu Mkuu kuwasiliana na Katibu Mkuu TAMISEMI tufanye assessment ya zahanati zote nchini, wana vipimo gani na vipi hawana? Vituo vya afya na hospitali, tutakwenda kununua kwa kutumia fedha hizi ambazo zipo, zinatumika kwa ajili ya semina, kwa ajili ya safari, kwa ajili ya kongamano, kwa ajili ya mambo ambayo hayawagusi wananchi moja kwa moja. Jana nimewauliza wenzangu Wizarani, mnaposema tumefanya hivi, mimi Waziri na Naibu Waziri tutasimama kwenye mkutano wa hadhara kuwaambia Watanzania, tumetumia Shilingi bilioni 10 kwa ajili ya semina, kwa ajili ya kongamano, kwa ajili ya matamasha, Hapana. Fedha tutaipeleka kwenye mambo yanayowagusa Watanzania hususan wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalize kwa kukushukuru, pia kuishukuru sana familia yangu, kuwashukuru wapiga kura wangu wa Jiji la Tanga. Tanga tunasema, jiji la mahaba na ukarimu, lakini tunataka liwe la mahaba, ukarimu na maendeleo zaidi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naafiki.