Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

Hon. Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii lakini kwa kutusimamia kwenye hiki kipindi kigumu kidogo naanza kuona matumaini tumekaribia na mwisho, lakini tumshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye siyo tu kwamba amekuwa kiongozi wetu lakini amekuwa mentor wetu. Wabunge ni mashahidi akija Majimboni kwetu anatuita Wabunge wenzangu nasi anatuita Mawaziri wenzangu wakati mwingine tunaenda kwa Waziri Mkuu tunaongea tunajisahau tupo na Waziri Mkuu baadaye tukitoka sisi tunajiuliza hivi pale tuliharibu lakini anakuwa ametuvumilia, tunakushukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwashukuru ninyi Wabunge wenzangu mmetuchanganya Mheshimiwa Ummy Mwalimu alikuwa ananiambia haya madeni tutayalipaje, lakini mmetuheshimisha na wakati mwingine tunawaza sasa je, tutaitunzaje, shida siyo kuambiwa mmefanya vizuri shida nitutatunzaje hiki mlichokiaminisha kwetu. Lakini mimi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Ndugu yetu Makubi tulikuwa tunashangaa tukiwa nje kwamba ule umahiri wa Mheshimiwa Ummy Mwalimu ambao tunauona sisi na ninyi mnauona tunasema ahsanteni sana Wabunge wenzangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaambie Waheshimiwa Wabunge Mheshimiwa Kingu na wenzangu ambao tulikuwepo Bunge lililopita, nilipokwenda kwenye uchaguzi 2020 tulikuwa tukipigiwa kura na tukizungumzia performance zilizofanywa kwenye Wizara ya Afya, aliyetusaidia tukafika hapo ni huyu Mheshimiwa Ummy Mwalimu ambaye tunae leo. Niseme tu alipokuja Wizara ya Afya akasema sisi tunaanzia strategy inayoitwa Samia Suluhu Hassan strategy ya 1.3 Trilioni ambayo imekuja yote ikaelekea kwa wananchi akatwambia tukae chini, akaita watu wanaosimamia mradi wa investing to people akakaa nao bila kuwagombeza akapunguza kwenye posho, akapunguza kwenye semina, akapunguza kwenye nini, leo tunazo Bilioni 10 tunaenda kujenga hospitali ya akina Mama Dodoma huyo ndiyo Mheshimiwa Ummy Mwalimu.

Mheshimiwa Spika, hata siyo muda na ninafiriki mtaona kwenye Majimbo kama 100 fedha zinakuja Bilioni 7.8 ambazo hazikuwa kwenye bajeti kabisa, ni katika kukaa kupunguza kwenye posho, kupunguza kwenye nini zikapatikana Bilioni 7.8 na ndani ya wiki zilizopita zimepelekwa TAMISEMI kwa ajili ya kuja kwenye Majimbo yenu, huyo ndiyo Ummy Mwalimu ambaye mmesema hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, alikuja tulikuwa tumepanga ilipangwa kwenye bajeti ya kawaida na kwenye utaratibu wa kawaida ilipangwa kwamba tununue ambulance 503 akasema hebu niachieni niwapigie UNICEF alipowapigia UNICEF makubaliano yaliyofanyika kule ambulance 503 tukajikuta kwa kununua kupitia UNICEF tunanunua ambulance 663 maana yake zimeongezeka ambulance 160. Maana yake nini Waheshimiwa Wabunge tunapozungumzia sasa hivi suala la ambulance kila Jimbo linaenda kupata ambulance mbili. Jana alikuwa anatuambia tuhangaike kwenye Global Fund tutafute nyingine 150 Mungu akisaidia inawezekana zikaendelea kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wenzangu, Dada yangu Msambatavangu Jesca amezungumizia suala la tiba ya akili, jana tulikaa vilevile Mheshimiwa Waziri akawa anasema hebu tuitishe Kongamano la Afya ya Akili. Tena nilikuwa namwambia hapa lile kongamano unaweza nimuombe akubali awe ni Balozi kuhakikisha kwamba tunapigania suala la Afya ya Tiba ya Akili. Niwaambie tu, shida moja afya tumekuwa tukiliangalia kwamba tatizo la maendeleo ya jamii tu, lakini tiba vilevile ni suala la uchumi. COVID ilivyokuja tulizungumzia COVID kama ugonjwa lakini tukazungumzia kama suala la kiuchumi, lakini leo ukizungumia kuanzia mtoto anapozaliwa inavyobebwa mimba unapompa lishe na mambo mengine yanakuja kutokea hayo ambayo anayasema Mheshimiwa Mbunge pale na kwamba hata tunapotoa fedha nyingi kwa wanawake kule vijijini, kwa vijana halafu outcome ya fedha tunayo dish kule kwa ajili ya kukuza uchumi na kufanya mambo mengine, inapokuwa haitokei ina mahusiano makubwa sana na lishe na namna gani tunavyofanya lishe kuanzia watu wanapokuwa wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile wenzetu sasa hivi mashindano tunakwenda dunia ambayo tunaizungumzia dunia ya artificial intelligent, wafanyakazi watakaotakiwa kesho kutwa siyo wafanyakazi wenye uwezo wa kufanya kazi ni wafanyakazi wenyewe uwezo wa kufikiri nakuja na mawazo mapya. Kama hujaboresha lishe, kama hujaboresha tiba ya afya ya akili huwezi kupata hiyo kaliba ya watu ambao ni innovative na wenye uwezo wa kufanya mambo hayo. Ndiyo maana nasema Mheshimiwa Waziri amesema hapa hilo kongamano akilitayarisha ni muhimu Wabunge wote tushirikiane.

Mheshimiwa Spika, tumshukuru Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kipindi kidogo cha mwaka huu mmoja, kwenye hospitali yetu ya Ocean Road tumekwenda kwenye Afrika nzima kuna nchi nne tu ambazo zinazalisha mionzi tiba zinaviwanda za mionzi tiba. Leo tunaenda kuingia kwenye historia ya Afrika kuwa nchi ya tano kwa Afrika kuzalisha mionzi tiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana tulikuwa tunazungumzia mgonjwa wa Mheshimiwa Saashisha ambaye amechelewa pale tukigojea mionzi tiba itoke kwa ndege siku ya Jumatano kutoka Afrika Kusini. Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kiwanda kimefikia asilimia 95 na sasa ndani ya miezi mitatu tunaenda kuzalisha hapa, na watu wetu watatibiwa hapa na nchi zinazotuzunguka zitaanza kuja hapa kwetu. Ukizungumzia hospitali yetu ya Ocean Road kwa maana ya uboreshaji uliofanyika pale utakwenda pale nchi 16 zinakuja pale kuchukua ujuzi wa namna gani unaweza kufanya mionzi tiba, ukienda JKCI mpaka kuna watu wametoka nchi zingine za Ulaya wanakuja kutibiwa pale, siyo tu kwa sababu moja kwamba kule wanatoa standard ya Ulaya lakini kwa bei rahisi zaidi. Kwa maana hiyo tunapozungumzia Wabunge suala la medical tourism Serikali yetu imejipanga na Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan amejipanga vizuri kwenye eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, amesema waziri hapa suala la upandikizaji wa Uroto na amesema Waziri hapa kwamba kwa Afrika kwa Mashariki na Kati sisi wenyewe ndiyo tunafanya, lakini Waheshimiwa Wabunge muelewe kitu walichofanya Rais wetu kwa kipindi hiki kidogo cha mwaka mmoja, kufanya Uloto kwa mgonjwa mmoja alikuwa anapelekwa India kwa thamani ya Milioni 250 kwa mgonjwa mmoja, leo hapa Tanzania baada ya Rais wetu kununua vifaa na vipo Muhimbili inafanyika kwa Shilingi Milioni 70 na anafanyiwa mgonjwa bure, maana yake tunaokoa Milioni 180 zinakwenda kufanya shughuli zingine za maendeleo. Hayo ndiyo mambo tukisema Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan anaupiga mwingi hiyo ndiyo maana yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia suala zima la ubora wa huduma. Kwa kweli ukizungumzia ubora wa huduma utazungumzia suala la dawa, utazungumzia suala watumishi, utazungumzia masuala mengine yote na upatikanaji, vilevile kwenye ubora wa huduma utazungumzia suala la ujenzi, majengo ambayo yanajengwa na mmeona wenyewe kwamba yamejengwa tunaenda kujenga EMD’s kwenye Wilaya zetu, tunaenda kujenga ICU’s na kuweka vifaa, lakini utazungumzia kusomesha wataalamu.

Mheshimiwa Spika, leo kama Tanzania watu wanatoka nchi zilizotuzunguka kuja kujifunza kwa wataalam wetu kuzungumzia nayo ubora wa huduma unazungumzia teknolojia nayo, kwamba tuwe na high standard ya teknolojia ambayo wakati mwingine tunaweza tukawa na mtaalam hapa lakini kama hatuna teknolojia inabidi mtu wetu aende kufuata kule, tukinunua teknolojia hapa ni gharama rahisi zaidi kumleta mtaalam kutoka nje akaja kutusaidia kwenye teknolojia iliyopo hapa na ikawa gharama zaidi na akawatibu wagonjwa wengi zaidi kwa muda mfupi na kwa gharama nafuu. Kwa hiyo hayo yote yanaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mmezungumzia suala la incentive, kwamba Madaktari wetu waache kukimbiakimbia kwenda sehemu tunafanya nini. Tunachowaambia tunampongeza sana Professor Mohamed Janabi wa Hospitali ya Jakaya Kikwete, amefanya kazi kubwa sana nzuri, Madaktari wake wanabaki pale pale na wanafanya na hawakimbiikimbii na Mount Meru hospitali wamefanya hivyo. Tutachukua model ya JKCI na model ya Mount Meru Hospital ambayo imeboreshwa pale halafu tuone ni namna gani tuna roll out kwenye nchi nzima ili iweze kufanyika namna hilo na lile ambalo mmeshauri Wabunge hapa liweze kufikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la damu salama kwa kweli damu hainunuliwi, damu hakuna sehemu damu wametembea nayo watu, tunaendelelea kuboresha Mheshimiwa Waziri ameitisha kikao na hii ilikuwa ni kuhakikisha kuboresha kwamba wataalam wetu wanapelekwa.

Mheshimiwa Spika, unajua wakati mwingine unaweza ukampeleka Mkurugenzi wa kukusaidia masuala ya damu kwenye Kanda lakini huyo mtu hata hawezi kuitisha kikao tu cha ukoo wake, unataka aitishe watu wakubali kutoa damu. Tunataka kuwaweka watu sasa ambao wana uwezo wa ku- mobilize kutumia mbinu mbalimbali kuhakikisha watu wanakuwa tayari kutoa damu.

Mheshimiwa Spika, mmezungumzia suala la tiba asili nakwenda haraka haraka, kama tulivyokwisha kusema tayari Rais wetu ametoa Shilingi Bilioni 2.8 zinakwenda kufanya utafiti pale NIMR kuhusu tiba asili mbalimbali. Pia kuna muda ambao Waziri wetu Mheshimiwa Ummy Mwalimu hivi karibuni ataenda kufungua hospitali ya tiba asili iliyopo kule Meru. Ni hospitali ambayo inatumia miti shamba kutoka Mlima Meru kutoka kule Umasaini lakini mengine kutoka Ulaya. Unaingiza kwenye maabara ya kawaida ya kisasa, inaingizwa kwenye vipimo vya kawaida vya kisasa lakini ukifika duka la dawa unapewa dawa za tiba asili.

Mheshimiwa Spika, wanaotibu ni Madaktari wazalendo lakini supervisors ni Wazungu wawili kutoka Australia, kwa namna hiyo tutachanganya ujuzi wa mwenzetu kutoka nje na sisi wenyewe tukimaliza tunaweza tukaboresha tibaasili zetu na kama ambavyo Mheshimiwa umesema tutatembelea Momba tutakuja Momba na tuangalie namna ya kufanya na kuhakikisha kwamba na wenzetu wa tibaasili kuhakikisha wanaweka hayo mambo sawa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga.

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Imeshagonga, nakushukuru mimi natoa hoja ili la TMDA na TBS mimi nafikiri tutaendelea kuwasilishiana kwenye Serikali na Waziri amelichukua litaenda kufanyiwa kazi kwa sababu ni kweli chakula ni sehemu muhimu sana lakini chakula usipo control tutapata matatizo ya figo, kansa na mambo mengi. Waziri amelichukua kwa uzito. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)