Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

Hon. Florent Laurent Kyombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi ya kuweza kuchangia katika bajeti yetu ya Wizara ya Afya. Niungane na wachangiaji wengine kumpongeza Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri anayoifanya kuhakikisha maendeleo ndani ya nchi yetu yanasonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kimahsusi nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa mabadiliko makubwa anayoyafanya ndani ya Wizara ya Afya na mahsusi zaidi ndani ya Taasisi yetu ya MSD tulishauri hapa Bungeni na kupitia Wizara yetu chini ya Mheshimiwa Ummy Mwalimu na msaidizi wake Dkt Mollel na wasaidizi wao na Mheshimiwa Rais akaitikia wito akabadilisha uongozi ndani ya taasisi yetu ya MSD na kuweka viongozi ambao ni wataaluma wa dawa, naamini tukiboresha mazingira ndani ya taasisi hiyo tutaona mabadiliko makubwa.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mageuzi hayo ya kiutawala lakini bado niendelee kuiomba Serikali. Viongozi hao tumewaweka katika kazi mahsusi. Tusipoweka mazingira ambayo ni wezeshi mazingira ambayo ni rafiki inawezekana tukawakwamisha sisi wenyewe.

Mheshimiwa Spika, sasa niombe, katika eneo hilo la MSD zipo changamoto mbalimbali ambazo tunahitaji kuzifanyia kazi; zingine ni za kikanuni, na zingine ni za kisheria. Mimi nimuombe Mheshimiwa Waziri kwa sababu ni msikivu na ni mtenda kazi anayeamini katika taaluma, hivyo uwape nafasi uliowateua kukusaidia kazi waweze kuleta yale mahitaji na muyafanyie kazi yaweze kufanyika na dawa ziweze kufika katika vituo vyetu na wananchi wapate dawa.

Mheshimiwa Spika, katika eneo hilo kwa uchache tunaona kwamba kazi ya clearance ya dawa kwa Sheria ni kweli imepewa GPSA, lakini bidhaa za dawa vifaa tiba na vitendanishi ni bidhaa ambazo ziko sensitive sana. Unakuta katika process ya manunuzi kuanzia kununua mpaka kusafirisha mpaka kuzi-clear pale bandarini hata ule muda wa matumizi unakuwa umepungua. Hatimaye hizi bidhaa zinaingia mtaani zikienda kusambazwa kwa walaji muda wa matumizi unakuwa umekaribia kuisha. Kwa hiyo saidia, najua ni sheria zipo na GPSA wanafanyakazi kwa mujibu wa sheria lakini bado Bunge Tukufu linaweza likafanya mabadiliko kwa ajili ya kuboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika eneo lingine ningependa kutoa mchango wangu mdogo katika jukumu la udhibiti wa chakula na vipodozi. Mwaka 2019 suala la chakula na vipodozi lilihamishwa kutoka Wizara ya Afya likapelekwa katika Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara chini ya TBS. Katika utaratibu wa kidunia tukiangalia basic practice duniani kote kwa kweli kidogo katika eneo hilo mpaka leo Tanzania bado watatushangaa.

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue historia kidogo. Tukiangalia kuanzia mwaka 1946 tulikuwa na sheria ya The Food and Brad Ordnance Cap. 93. Hii tangu tunatawaliwa na wakoloni mpaka Mwalimu Nyerere mwenyewe alivyokuja hizi bidhaa zilikuwa zinadhibitiwa chini ya Wizara ya Afya. Ilipofika mwaka 1978 Serikali ikaona iboreshe kwa kutenganisha bidhaa hizi kwa kutunga sheria zingine mbili. Ikatunga sheria ya kwanza ya The Pharmacy and Poison Act. ya Mwaka 1978, ikatunga The Food Control Quality ya mwaka 1978. Nia ilikuwa ni kuboresha bidhaa hizi kwa sababu zina linda afya ni kwa ajili ya manufaa ya wananchi wetu. Na Serikali katika taasisi hizi chini ya sheria hizi ikawezesha miundombinu na wataalamu, kazi zikaanza kufanyika.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa mabadiliko ya kidunia ilipofika mwaka 2003 kuangalia na mwenendo wa dunia nzima Serikali ikaamua kuziunganisha tena bidhaa hizi na kuvunja sheria hizo mbili na kuunda sheria moja; Sheria ya Chakula Dawa na Vipodozi na Vifaa Tiba Na. 1 ya Mwaka 2003. Katika eneo hili taasisi ambazo zilipewa dhamana ya kusimamia hivi chini ya Wizara ya Afya zimefanya kazi kubwa. Serikali imewekeza fedha nyingi sana katika eneo hili. Imeweka miundombinu ya kutosha mpaka nchi yetu ikapata vigezo vya kimataifa mpaka tukawa na maabara inayotambulika kimataifa tukapata WHO pre-qualified laboratory ambayo unaweza ukapima bidhaa zote ndani ya nchi na nje ya nchi. Haikuishia hapa, tukapata ithibati kutoka WHO ambayo ilikuwa inaonyesha kwamba mifumo ya udhibiti imehakikiwa na inakidhi vigezo vya kimataifa

Mheshimiwa Spika, mwaka 2019, kama nilivyotangulia kusema, mabadiliko yakafanyika; inawezekana yalikuwa na nia njema. Hata hivyo, hata hivyo bidhaa hizi zikaenda kurushwa sehemu ambayo ukiangalia kwenye Blue Print ya Taifa letu si majukumu yake. Kwa hiyo kupelekwa TBS ambayo yenyewe inadhibiti viwango na ukaipelekea udhibiti tunaenda kuhatarisha afya ya wananchi.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia bidhaa hizo madhara yake ni makubwa sana, na taarifa za takwimu za WHO ukiangalia katika dunia nzima magonjwa zaidi ya 200 yanatokana na ulaji wa vyakula ambavyo si salama. Lakini ukiangalia watu milioni 600 katika uwiano wa mtu mmoja katika watu 10 wote hao wanapata madhara wanapokula vyakula ambavyo si salama. Lakini tukiangalia watu 420,000 hufa kila mwaka kwa kula vyakula ambavyo si salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukiangalia fedha zinazotumika duniani dola za kimarekani bilioni 110 zinatumika katika kutibu magonjwa yanayotokana na vyakula hivyo.

Mheshimiwa Spika, sasa mimi niombe sana katika eneo hili. Serikali inakuwa inafanyakazi nzuri kuhakikisha kwamba itapata matokeo mazuri lakini katika eneo hili matokeo siyo mazuri na mimi nishauri na nimshukuru Mwenyezi Mungu kwamba Mheshimiwa Ummy Mwalimu, nafikiri Mwenyezi Mungu ana makusudi yake. Wakati suala hili linafanyika najua ulipambana sana kulizuia katika Wizara yako, na kipindi hicho nilikuwa sijajua kama nitakuwa Mbunge; lakini halikufanikiwa na leo Mwenyezi Mungu amekurudisha humo humo katika Wizara hiyo hiyo na leo sasa na mimi naliongelea.

Mheshimiwa Spika Mheshimiwa Waziri na msaidizi wako suala hili; na inawezekana kwa kiasi kikubwa mlishaanza kuifanyia kazi. Okoa maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, vipodozi hivi vinaleta kansa ambazo nimesikia Waheshimiwa Wabunge wanasema. Hakuna mchawi, ni kwamba sisi tumeamua kuweka vipodozi watu watumie wanavyotaka. Unalala asubuhi unakuta mtu shape iko hivi, baada ya muda mfupi madhara yake ni yeye na hospitali, hospitali na yeye; kwa hiyo hatuwezi kusema kwamba tunatafuta mchawi ilhali hapa tumeongelea saratani na hivyo vipodozi ambavyo havijadhibitiwa vimekaa mtaani. Sisi tuna uchungu na wananchi, na Bunge lako Tukufu limepewa dhamana hii kushauri Serikali kuhakikisha kwamba inafanyia kazi maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tunaona matatizo ya figo pamoja na matatizo ya ini yataendelea kuongezeka. Nasimama hapa, nasema, tukiangalia miaka miwili ijayo mbele inawezekana tukawa na madhara ya magonjwa mengi kwa ajili ya kuziacha hizi bidhaa mtaani zikiwa hazina udhibiti na zikiachiwa taasisi ambayo si jukumu lake. Kwa hiyo niombe sana niombe sasa Mheshimiwa Waziri kupitia Wizara yetu ya Afya basi ifanye utaratibu mapema ili bidhaa hizi ziende katika eneo linalokubalika, ambalo ni Wizara ya Afya chini ya mamlaka ya Chakula na Dawa na vipodozi au yoyote itakavyoitwa….(Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nimalizie kusema…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. FLORENT L. KYOMBO: …nikushukuru, naunga mkono hoja, ahsante sana, nashukuru sana.