Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

Hon. Elibariki Emmanuel Kingu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nitumie nafasi hii kukushukuru kwa kunipatia nafasi ili kutoa mchango wangu mfupi katika Wizara hii ya Afya ambayo kimsingi ni Wizara muhimu sana kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa letu na sustainable development kwa ujumla katika Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nataka niseme kwamba, imani kubwa ambayo Watanzania wameendelea kuwa nayo kwa Serikali yetu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kiwango kikubwa imani hiyo inachagizwa na mambo makubwa ya msingi yanayotokana na upelekaji wa huduma za msingi kwa wananchi. Jambo ambalo limeendelea kuwafanya Watanzania waendelee kuwa na trust na Serikali iliyoko madarakani.

Mheshimiwa Spika, nayasema haya kwa sababu kubwa mbili. Kwanza kabisa, Rais wetu Mama yetu aliyoko madarakani Mama Samia Suluhu Hassan amefanya juhudi kubwa sana na hatuwezi kuacha kulisema hili. Tumekuwa tukizungumza habari ya revolution kubwa iliyofanyika katika kuboresha masuala mazima ya Afya katika Mikoa, Wilaya mpaka Kata. Rais wetu tunampongeza sana na jambo hili mimi nasema kwamba tukiendelea kumpongeza Rais kwa mambo haya anayoyafanya tukaacha kuifanya Serikali na baadhi ya watendaji kuwajibika kwa makosa ambayo yanaweza yakamtia Rais doa tutakuwa hatulitendei haki Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nayasema hayo kwa sababu kubwa mbili. Miezi minne iliyopitia tumemsikia Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akipita na kulalamika nchi ikiwa inakumbwa na upungufu mkubwa wa madawa kuanzia kwenye Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya na Hospitali za Mikoa mpaka Hospitali za Rufaa. Kama hilo halitoshi, tumemsikia Waziri wa Afya akilalamika upungufu wa madawa kwenye hospitali zetu.

Mheshimiwa Spika, nataka niseme na Mheshimiwa Ummy naomba anisikilize kwa makini sana Bunge hili sisi tuko hapa kwa sababu ya legacy ya kuhakikisha kwamba wale wananchi waliotuchagua ambao ndiyo walipa kodi tunakuja kuwasemea na kuhakikisha kwamba welfare zao zinatekelezwa na Serikali iliyoko madarakani. Kitendo cha wapiga kura wetu ambao ndiyo wananchi tunakwenda kwenye mikutano ya hadhara, tunahutubia mikutano tukimaliza tunaambiwa Mbunge mmetujengea Kituo cha Afya dawa ziko wapi. Jambo hili lazima lifike mahali likome kwenye Taifa letu, watu wanaotuchagua na sisi kama Wabunge ambao tunatokana, kwa mfano kama mimi natokana na Chama Tawala. Chama changu kimepewa ridhaa ya kuongoza Taifa kwa sababu kilikuwa na election manifesto, kimeahidi mambo ya kutekeleza.

Mheshimiwa Spika, jambo la ukosefu wa dawa nakwambia limekuwa kero kubwa kwa wananchi huko mtaani na wananchi wetu wapiga kura wamekuwa hawatuelewi. Jambo la kusikitisha Serikali inatoa fedha, MSD inapelekewa pesa, Mheshimiwa Waziri Ummy watuambie jambo gani linatokea dawa haziendi kwa wananchi? Jambo gani linatokea MSD huko dawa hazifikiwa kwa wananchi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waziri Mkuu analalamika, Waziri analalamika, what’s going on kule MSD. Hili jambo nalisema kwa dhati ya moyo wangu, sisi kama Wabunge na mimi kama Mbunge ninayetokana na chama kilichopo madarakani, tunawapa Wizara muda wa matarajio, tunaomba jambo la ukosefu wa dawa kwenye Taifa hili, tunawapa miezi minne au mitano, tutakuja hapa Bungeni… (Makofi)

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Kingu, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Lucy Thomas Mayenga.

T A A R I F A

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kutokana na tatizo kubwa lililotokea MSD, naomba Bunge na nimwongezee Mheshimiwa Kingu kwenye taarifa yake, ni vizuri Wizara hii ifanye special audit MSD ili ambaye anatuhumiwa, kazi iendelee.(Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Kingu, unapokea taarifa hiyo.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo naipokea kwa sababu mimi nimetumwa na wananchi nije niwe sauti yao kwenye matatizo yao. Wananchi wa jimboni kwangu moja ya changamoto zinazowakumba hakuna madawa, Mama Rais anatoa fedha na Serikali sisi Wabunge tunaidhinisha hapa bajeti, Bunge lako linaidhinisha bajeti zinakwenda kwa nini dawa hazifiki? Hili jambo nataka niwaambie Wabunge sisi ndiyo tutakaoenda kuulizwa kule, sisi ndiyo tunaounda Serikali, lazima tusimame imara hapa Bungeni kuhakikisha Serikali yetu tunai-task, kuhakikisha kwamba dawa zinawafikia wapigakura wetu na walipakodi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, hilo hilo linaloendana na dawa. Nataka nimshauri Waziri waende wakalete Sheria tuje tuwapitishie. Tuunde kitu kinaitwa Health Commodity Revolving Fund, tuweze kuwaundia chombo cha Kisheria. TANROAD wana chombo chao cha kuleta fedha kwa ajili ya dawa, maji wana chombo chao. Afya ni jambo muhimu linalohusiana na masuala mazima ya usalama wa Taifa, waende wakalete Sheria tutawaundia Mfuko wa Fedha wa Dawa. Mfuko huo utafutiwe vyanzo vya uhakika vya fedha ili kuwasaidia watu wetu waweze kuhakikisha kwamba wanapata uhakika wa dawa.

Mheshimiwa Spika, Mfuko huu tutautafutia vyanzo vya uhakika vya fund ili kusudi uweze kuwasaidia watu wetu na tuweze kulisaidia Taifa letu. Nataka niwaambie nipo kwenye Kamati ya Katiba na Sheria, Makamu wangu Mwenyekiti yuko jirani hapa, hapa kuna wajumbe tuko tayari, Wizara ilete hiyo sheria, tutaichakata, tutaileta Bungeni, tulisaidie Taifa waweze kuwa na special fund ya kusaidia mambo ya dawa katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa tatu, Madaktari wetu, naomba wanisikilize kwa makini sana Waheshimiwa Wabunge. Tunapozungumzia jambo la Madaktari kwenye Hospitali za Umma, public facilities, Daktari anakwenda pale anakaa dakika 20 anatibu, anakimbia anakwenda hospitali B, anatoka hospitali B anakaa dakika 10 anakimbia, anakwenda hospitali C. wanahangaika kujikimu maskini, Mheshimiwa Ummy dada yangu niwaombe Madaktari hawa kama walivyo watumishi wengine ni watu wamesoma hizi taaluma zao, wanatibu, haya mambo ni mambo ya usalama wa Taifa.

Mheshimiwa Spika, naomba Wizara waende wakahakikishe zile package za percentage wanazozipata private, wawape wanapofanya kazi kwenye hospitali za umma. Waende wakawape Madaktari wetu, hili jambo la Madaktari kukimbia hawataliona, wata-concentrate kuwatibu watu katika public facility. Jambo hili litaongeza tija ya utendaji na tutakuwa tumewasaidia Watanzania na tutaleta tija na sisi wataturahisishia kazi ya kwenda kuomba kura 2025 kuhakikisha kwamba Mama ambaye huyu ameleta matumaini kwa Taifa na kwa kweli kwenye hili wanawake shikamooni, mmetisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye hili nasema kwa dhati ya moyo wangu, kwenye hili mimi mwenyewe sasa hivi kwa dhati ya moyo wangu nimeamua kuwa advocate wa akinamama. Akinamama mkiaminiwa uwezo wenu wa kufanya kazi na sema kwa dhati ya moyo wangu, wanawake shikamooni, uwezo wenu wa kufanya kazi ni mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia hapa hata utulivu huu wa Bunge aliyekaa hapo ni mwanamama, ukiangalia hata namna Taifa linavyokwenda, mimi juzi nilikuwa nasoma statistic, Afrika nzima Rais wa Tanzania mwanamama amepandisha mishahara Afrika nzima 23 percent, nani kama mama? Kwa uwezo huu akina mama, nashawishika kabisa hata kuamini hata baadaye tukileta sheria hapa wanawake tuawaongeze kwenye Uongozi watalisaidia sana Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo langu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Kingu kengele imeshagonga. Ahsante sana.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Point zangu zingine nitaziwasilisha kwa maandishi. Ahsante sana. (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge walimtunza fedha Mhe. Elibariki Kingu kutokana na mchango wake)