Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hoja iliyoko mbele yetu ya Wizara ya Afya. Nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu pamoja na timu yake, kwa kweli wanajitahidi na wanafanya vizuri. Pia Wizara hii imekuwa ikitupa ushirikiano sisi wajumbe wa Kamati kwa kadri inavyowezekana hongereni sana.

Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia katika maeneo mawili. Hoja ya kwanza ni katika eneo ya magonjwa yasiyoambukiza. Tunapoongelea afya ya Watanzania au magonjwa ambayo mengi yanayowasumbua Watanzania leo, mengi ni magonjwa yasiyoambukiza. Tafiti zinaonyesha asilimia 40 ya vifo nchini vinatokana na magonjwa yasiyoambukiza na magonjwa haya ni kansa, sukari, pressure na kadhalika. Kwa kiwango kikubwa haya magonjwa yasiyoambukiza kwa namna moja ama nyingine kama tukiwa na mikakati ya kutosha kama Serikali lakini kama jamii ikatambua athari ya magonjwa yasiyoambukiza basi tunaweza kupunguza kwa kiwango kikubwa na badala ya Serikali kufikiria kutibu, kwa sababu tunavyoongelea Hospitali za Rufaa zina upungufu wa dawa na kila kitu ni kwa sababu ya ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza. Sasa tukiweka nguvu huko maana yake tutaweka kinga zaidi badala ya kutibu.

Mheshimiwa Spika, hata leo Serikali wanapoomba bajeti kwenye Wizara hii ya Afya zote zinaenda kutibu siyo kukinga, kwa sababu ya aina ya maisha ya Watanzania ambayo tulikuwa nayo huko nyuma, tumepata magonjwa yasiyoambukizwa kwa wingi. Hivyo tunaweka nguvu kubwa katika kuyatibu. Nashauri Serikali na wadau mbalimbali sasa tuweke pia nguvu kuhakikisha tunaweka kinga kwa magonjwa yasiyoambukiza ili hii asilimia 40 ya vifo inayotokana na magonjwa ya kuambukiza, basi tuweze kuipunguza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo lazima jamii ipewe elimu na kueleweshwa. Kuna mambo mengine kwa mfano mtindo wa maisha tunayoishi, wakati mwingine yanapelekea ndiyo tunapata sukari, tunapata pressure, mtu anaona anaishi maisha fulani ndiyo yuko sawasawa kumbe siyo sahihi. Kwa hiyo nadhani Serikali kwa kushirikiana na Wizara nyingine mtambuka pamoja na wadau tuone namna ya kubadilisha maisha ya Watanzania tunayoishi.

Mheshimiwa Spika, nitoe mfano, leo vijana wetu wa bodaboda wanaendesha bodaboda siku nzima, ok wamejiajiri wapate kipato lakini hawa vijana wanakunywa kinywaji maarufu kinachoitwa energy drink ambazo ziko za aina mbalimbali. Hawa vijana wanaweza kunywa energy drink tatu, nne, tano kwa siku, huyo utegemee baada ya miaka 10 au 20 Serikali tutaanza kumtibu kwa sababu amepata magonjwa yasiyoambukiza. Yeye leo anaona yuko sawasawa inawezekana hajui madhara na ni kweli kwamba wengi hawajui madhara.

Mheshimiwa Spika, siyo hao tu nimetoa mfano mmoja wa kundi moja la vijana wa bodaboda kwa sababu tunawaona, wako wengine wengi tu wa makundi mbalimbali hata watu ambao wapo maofisini, kwenye sekta binafsi mtu anaona kunywa energy drink labda ni Red Bull au nini ananunua 3,000 mpaka 4,000 anaona ni ufahari kwa sababu ni kinywaji ambacho angalau kina bei fulani, kumbe ni kinywaji ambacho tunajitengenezea matatizo mwisho wa siku tunapata kansa, tunapata kisukari, sijui wanasema maini yanavimba, mimi sielewi vizuri utaalam. Lakini yote hayo yanapelekea kwenye…

SPIKA: Mheshimiwa Cecilia Paresso ngoja, ngoja twende vizuri kwa sababu hapa Bungeni pamoja na mambo mengine hizo biashara zinazosemwa hapo ni biashara za watu, sijajua kitaalam kama hivyo vinywaji unavyovisema ndivyo vinavyoleta hayo magonjwa unayoyasema. Maana kama Serikali imeruhusu viuzwe halafu vina madhara hayo makubwa unayoyasema itakuwa mtihani. Hapa kuna kimoja ambacho umekitaja mahsusi. Sasa ili usitupeleke kwenye hiyo hoja, hoja yako ni ya msingi lakini usitupeleke kwenye hiyo hoja ya wafanyabiashara fulani kuona wao wanaonewa na Bunge. Hebu hiyo sehemu ya mchango wako rekebisha.

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa maelekezo. Nirekebishe tu kwa kusema vinywaji vya kuongeza nguvu kwa ujumla wake vinavyoitwa energy drink kwa ujumla wake, sasa pamoja na kwamba vinapata kibali vinaingizwa, lakini Serikali ione namna gani ya kutoa maelekezo ya unywaji ulio bora ili tusije tukaingiza Taifa au watu wetu kwenye magonjwa yasiyoambukizwa kwa kuleta madhara kimwili na kiafya. Kwa hiyo hilo ni upande mmoja katika vinywaji hivi vya kuongeza nguvu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna suala la utumiaji usio sahihi wa…

SPIKA: Sasa Mheshimiwa Paresso hapo umeeleza vizuri, hebu sasa ondoa yale maneno yako ya Red Bull.

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naondoa yale maneno niliyotaja ya Red Bull.

Mheshimiwa Spika, suala lingine pia ni utumiaji usiyo sahihi wa viatilifu kwa wakulima. Wakulima wetu wengi wanatumia hayo madawa mashambani kwa namna isiyo sahihi, pamoja na kwamba vinapata vibali, vinaingia, kuna ukaguzi na vitu kama hivyo, lakini hawatumii kwa namna isiyo bora. Kwa hiyo wasipotumia kwa namna isiyo bora tutegemee mwisho wa siku na huko vijijini tunaona. Kwa mfano sisi tunaotoka Karatu kuna bonde moja linalima vitunguu pale.

Mheshimiwa Spika, ukifika wakati wa kupulizia dawa wanapulizia tu ilimradi mtu anachukua bomba anapuliza, hana namna yoyote ya kujikinga. Kule pia kuna shida kubwa watu wanaanza kuwashwa na wanaanza kupata magonjwa ya ngozi. Huyu mwisho wa siku akiendelea muda mrefu kuna nafasi kubwa sana ya kupata ugonjwa wa kansa. Kwa hiyo iko namna ya kutazama pia kwa wakulima wetu tuwasaidie, kuwepo na mbinu mbadala kwa kushirikiana Wizara husika na Wizara zingine Wizara za Kisekta tuone namna gani pia wakulima wetu watumie kwa usahihi hivi viatilifu ili kuondokana na hatari ya kuingia kwenye magonjwa yasiyoambukiza.

Mheshimiwa Spika, kuna suala lingine pia, suala la kutokufanya mazoezi ni sehemu pia ya namna ambavyo tunajiweka kwenye mazingira hatarishi ya kupata magonjwa yasiyoambukiza. Tunafahamu siku hizi kuna kampeni mbalimbali za kufanya mazoezi, ni kweli lakini ni wachache, Watanzania walio wengi bado hawajui manufaa ya kufanya mazoezi. Mfano mtu anakaa ofisini au yuko nyumbani anafanya hivi, anakula wanga wa kutosha akitoka hapo hafanyi mazoezi hajishuhgulishi hafanyi chochote. Huyu utegemee baada ya miaka 10, 20 anaanza sukari, anaanza pressure, Serikali inaanza kuweka nguvu kubwa sasa ya kutibu pressure yake na sukari yake, lakini kumbe tungeweza kuweka nguvu kubwa ya kupunguza hiyo life style yake au kwa kufanya mazoezi kwa kupunguza hatari kubwa ambayo iko mbele yake.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nitoe rai kwa Serikali pamoja na wadau tuweke nguvu kubwa ya kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza, tutoe elimu kwa Watanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, Watanzania wajue namna ya ulaji sahihi na kwa wakati, wafanye mazoezi, ili basi tuone kwamba tunapunguza haya yaliyoko mbele yetu ya vifo karibu asilimia 40 vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza.

Mheshimiwa Spika, suala la pili nizungumzie vifo vinavyotoka na uzazi. Kupitia Hotuba ya Waziri ameeleza vizuri sana angalau vinapungua vifo hivi vinavyotokana na uzazi, lakini bado takwimu zinaonyesha vifo hivi bado ni vingi sana. Pamoja na kwamba kuna jitihada zinazoendelea lakini pia uhudhuriaji wa clinic kwa akinamama wajawazito umeeleza na mpango wa kuhakikisha Serikali inatoa elimu kwa akinamama wanaohudhuria clinic ni jambo moja zuri, lakini hata pale wanapofika clinic wanapokelewaje, hapo pia kuna tatizo kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, mtu anaweza akaenda tu anapimwa anaondoka zake, yaani samahani kusema haya, baadhi ya manesi utakuta tu maskini anampokea mama mjawazito yeye mwenyewe amenuna kweli kweli. Yaani huwezi jua alikotoka kule ana mazingira gani, inawezekana ugumu wa maisha, inawezekana ndivyo alivyo, lakini tuangalie pia hii customer care kwa akinamama wanaofika pale clinic, anapokelewaje. Ndiyo atahudhuria, tutawahamasisha kweli wahudhurie na hapa wameonyesha takwimu zinaongezeka kidogo, lakini bado wako wengine wengi ambao hawahudhurii. Akifika pale anapokelewaje, anakaguliwaje, yuko katika hatua gani anapewa maelekezo gani na maelekezo gani na maangalizo gani ili anapofikia hatua za kujifungua au akiona dalili fulani hatarishi afanye nini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hilo ni muhimu sana, wakaweka ama ni dawati hapo pekee maalum, akishamaliza kwenye vipimo awe na mtu wa kumsemesha. Nikwambie ugumu wa maisha uliyopo leo pia kwa kiasi kikubwa unachangia, mama ametoka huko maskini ana stress za maisha huko, stress za familia, jamii inayomzunguka akifika pale anatamani apate comfort fulani kwa kuongea unajua sijui wataalam wanasema hata ukisema una-release stress uliyonayo. Kwa hiyo afike pale kwenye kituo anaenda clinic lakini anakutana na mtu ambaye pamoja na atampa ushauri wa hali yake ya ujauzito lakini apate hata haya mengine ya kupumua ili huyu mama mwisho wa siku aweze kujifungua salama.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, mchango wangu ni huo. (Makofi)