Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na mimi kwa kunipa nafasi ya dakika hizi chache niweze kutoa mchango wangu kwenye wizara hii muhimu sana ya ulinzi wa Maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, na mimi nianze kwa kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Afya, Naibu Wake pamoja na Katibu Mkuu na Sekretarie nzima ya afya kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kusimamia Ilani ya Uchaguzi ambayo imeelekeza kuhakikisha ya kwamba Watanzania wanapatiwa afya na tiba ambazo zinalinda afya zao.

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizi ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu maelekezo yake mengi yamekuwa yakifanyiwa kazi kwa usahihi. Pale Mwanza kwenye Jimbo la Nyamagana ambapo kuna Hospitali ya Mkoa wa Mwanza inayoitwa Seketoure, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu sasa baada ya kupata takribani shilingi bilioni 10 jengo limekamilika zaidi ya asilimia 98. Na hivi ninavyozungumza Mheshimiwa Waziri, leo narudia tena, niwapongeze sana kwa maamuzi mazuri yaliyofanywa na Mheshimiwa Rais zile fedha za UVIKO zilipelekwa kwenye maeneo ya afya ili kwenda kutatua changamoto vya vifaa.

Mheshimiwa Spika, Seketoure peke yake ilipata takribani bilioni mbili na milioni mia saba, Mheshimiwa Waziri kwa maelekezo imetumia zaidi ya asilimi 68, bilioni moja na milioni mia nane kununua vifaa vya lile jengo lote ulilolishuhudia pale, lakini asilimia 32 peke yake ndiyo imekwenda kwenye matumizi mengine ikiwemo nyumba ya muuguzi atakayekuwa anakaa pale, furniture na vifaa vingine.

Mheshimiwa Spika, sasa haya ni moja kati ya matokeo ambayo tunaamini wizara hii; Mheshimiwa Sekiboko amesema pale juu ya kulinda vifo vya mama na Watoto, na Mheshimiwa Waziri nikuhakikishie baada ya kuimarisha Hospitali ya Seketoure imeendelea kupunguza vifo vya mama na mtoto kutoka 18 mpaka vifo nane leo. Hatuna shaka ya kwamba vifo hivi vitaendelea kushuka sana kwa sababu ya uimarishaji bora wa huduma hizi za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini la pili kwa haraka sana kwa sababu ya muda, ni kuhusu ulinzi na uimarishaji wa viwanda vyetu vya ndani vya dawa. Nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri na nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu alipotembelea pale MSD. Miongoni mwa mambo aliyoyapongeza ni kuona Kiwanda cha Keko Pharmaceutical pamoja na jitihada ndogo zilizokuwepo kimepiga hatua ya kuendelea kuzalisha dawa zinazohitajika ndani.

Mheshimiwa Spika, lakini nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, kiwanda hiki uwezo wake ni asilimia 36 peke yake. Tumekwenda pale na kamati yako ya PIC tumejionea shughuli na changamoto nyingi zilizokuwepo pale. Niombe, MSD, Keko Pharmaceutical wanahitaji bilioni 12 peke yake ili wafikie uwezo wa dawa zote 10 zinatakiwa hapa.

Mheshimiwa Spika, na nimpongeze sana mkurugenzi mpya wa MSD, ninaamini Serikali, Waziri Mheshimiwa Ummy na Serikali mmefanya nafasi yenu. Hili wala si la kufumbia macho, popote jicho lako linapokwambia kuna shida inaweza kukwamisha maendeleo ya sekta ya afya chukua maamuzi na amua mara moja ili tuweze kutoa tija kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo tunamkurugenzi mpya MSD, sina shaka na yeye atakuwa na nafasi yake kwenye maeneo ya ndani ya utawala wake. Na Mheshimiwa Waziri tukifumbiana macho katika sekta ya afya ambayo ni moja ya sehemu ya ulinzi wa taifa hili hii ni zaidi ya kiwanda cha mabomu. Mheshimiwa Waziri usipolinda sekta ya afya vizuri nataka nikuhakikishie watu wako watakufa kwa magonjwa, watu wako watashindwa kupata tiba na sisi tutakuwa hatuna maana ya kuwepo hapa ndani kwa sababu moja ya jukumu letu ni kuwapa nguvu viongozi mliopewa nafasi ya kusimamia sekta hii; na sisi tunawaunga mkono tunaamini sasa changamoto zote zilizokuwepo MSD zitakwisha na hata hiki kiwanda cha Keko.

Mheshimiwa Spika, tumetembelea pale sisi, meneja anayekisimamia na wasaidizi wake wengi wote ni akina mama. Kwa hiyo, tunaamini akina mama katika ile eneo la kusimamia kazi zenu kwa nguvu mkurugenzi atasimamia na atafanya kazi yake vizuri. Tunataka tuione MSD kwenye kiwango cha kimataifa. Tupate ithibati ili tuuze dawa mpaka kule kwenye nchi za SADC kwa kufanya hivyo itatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini lingine tunaomba kufahamu, Mikoa ya Kanda ya Ziwa sasa hivi ugonjwa wa kansa umeendelea kuwa mkubwa sana. Mimi niwapongeze, sana mlipoweka nguvu kuhakikisha Hospitali ya Bugando inajenga jengo kwa ajili ya wagonjwa maalumu wa kansa, na sasa hivi jengo hili lipo takribani asilimia 98. Watu wa Bugando wamesimamia vizuri; na nimpongeze sana Mkurugenzi wa Bugando na timu yake nzima. Unajua watumishi wa afya hawa pamoja na changamoto nyingi tulizonazo lakini hakika wanajitahidi kufanya kazi yao vizuri na wanastahili sifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa jengo hili la Bugando kukamilika kwake tunahitaji vifaa; kwenye bajeti yako hakikisha kadiri unavyoweza. Niwapongeze kwa sababu mmeshaanza na Ocean Road. Mmeweka kiwanda ambacho viwanda vya aina hii katika Afrika vipo vinne peke yake; na sisi dawa zote tunategemea Afrika Kusini. Leo tukiongeza cha kwetu kitakuwa cha tano katika Afrika. Maana yake ni kwamba, sasa ukiongelea lile suala la Mama anaupiga mwingi ulitazame kwenye angle hii, ambayo inakwenda kuokoa maisha ya wananchi wengi wa kanda ya ziwa; na kwa kufanya hivyo mtakuwa mmelisaidia sana taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya mambo tunayoyasema si mambo mepesi. Wenzangu wameongea hapa juu ya mfumo wa ulinzi wa mapoteo ya pesa za NHIF. Leo ukitibiwa Bugando au Seketoure ukapata referral kwenda Muhimbili ukifika kule unaenda kuanza upya. Kumbe kungekuwa na mifumo hii ambayo inasomana vizuri ingekuwa ni rahisi daktari aliyepo kule Muhimbili kuona taarifa zako za Bugando na akawa na ulinzi mzuri kwa ile kadi na fedha ambayo mnaitoa ya NHIF. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, najua kengele imegonga, hasa kwa sababu nilikuwa kwenye moto sijui ni ya pili sijui ni ya kwanza.

SPIKA: Ya pili Mheshimiwa.

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana, lakini niwaombe Waheshimiwa Wabunge tumpe ushirikiano wa kutosha Mheshimiwa Waziri tuipe ushirikiano wa kutosha Wizara hii, Katibu na timu yake nzima. MSD pia tuipe nguvu ili ifanye kazi vizuri.

SPIKA: Haya, ahsante sana.

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)