Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

Hon. Salim Alaudin Hasham

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

MHE. SALIM A. HASHAM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye Bunge lako Tukufu. Kwanza pia namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya ya kuweza kusimama na kuweza kuchangia kwenye Wizara ya Afya. Pia nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi anayofanya. Anafanya kazi kubwa sana. Kiukweli tumpongeze, anafanya kazi kubwa, ameweza sana kuwekeza kwenye Wizara ya Afya na ameweka pesa nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampongeza pia Mheshimiwa Ummy, amejaribu sana kujibu maswali yangu kwenye hotuba yake, lakini naamini kwamba itaenda kufanya kazi vizuri zaidi. Kiukweli Wabunge wengi ambao wakisimama hapa kuchangia hawatakosa kutaja vitu vitatu tu ambavyo vinawaathiri Watanzania kwenye suala la afya. Hatuwezi kujenga Taifa lenye uchumi mkubwa kama watu wetu hawana afya ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kila anayesimama hapa, changamoto ya kwanza atakwambia ni dawa, changamoto ya pili atakwambia vifaatiba na changamoto ya tatu atakwambia upungufu wa watumishi. Hatuwezi kukwepa. Mheshimiwa Ummy nikwambie, huwezi kukwepa hilo, unatakiwa uende ukafanye kazi kubwa sana kwa kushirikiana na Naibu wako. Kwa sababu ukitoa mfano kwenye jimbo langu, nina deficit ya wafanyakazi wa utumishi wa afya asilimia 67. Mbunge mwenzangu aliyepita hapa amesema anao watumishi asilimia 22, kwa maana maana deficit ni asilimia 78. Ukipiga hesabu kwenye nchi nzima, inawezekana deficit ikawa asilimia zaidi ya 60 watumishi wa afya hamna. Hatuwezi kufika.

Mheshimiwa Spika, ukizungumzia kwenye suala la vifaatiba, vifaatiba hakuna. Jimboni kwangu kuna X-Ray ya miaka 20 na zaidi haifanyi tena kazi, tumehangaika kuitengeneza na Mkurugenzi wangu wa Wilaya zaidi ya mwaka mzima, imeshindikana kabisa. Hakuna taasisi yoyote inayotoa huduma ya mionzi kwenye jimbo langu.

Mheshimiwa Spika, wananchi wanatakiwa waende kilometa 75 wilaya nyingine kupata huduma ya mionzi kwa maana ya X-Ray. Huyu mwananchi ataweza wapi ku-afford hiyo gharama? Gharama ya X-Ray ni Shilingi 10,000/=. Nauli Shilingi 10,000/= kwenda, kurudi Shilingi 10,000/=, hajala, huyo mtu hawezi kufanya hivyo vitu. Tunaomba sana Mheshimiwa uende ukalifanyie kazi. Nafikiri kwenye ofisi yako nina maombi ya X-Ray muda mrefu sana. Naomba pia hilo uende ukalifanyie kazi.

Mheshimiwa Spika, hatuna ambulance kwenye Jimbo langu. Ukiwauliza Wabunge wengi hapa watakuwa wamenunua vigari kwa ajili ya kusaidia wananchi wao kama ambulance, na ndiyo ukweli ulivyo. Ina maana vifaatiba bado havitoshi. Changamoto bado ni kubwa! Hizi changamoto tatu ni lazima ukazifanyie kazi, vinginevyo hatuwezi kujenga Taifa lenye uchumi mkubwa kwenye nchi hii.

Mheshimiwa Spika, lingine lazima niseme, nilileta tena maombi kwenu kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya yangu ya Ulanga. Hospitali hii hali yake ni mbaya sana. Ukienda maabara ya Hospitali ya Wilaya ya Ulanga, unaweza kusema labda hiki ni chumba na sebule ya Manzese. Ni kitu ambacho kinawakwaza sana wananchi. Miaka sita iliyopita tulipata pesa kwa ajili ya kufanya ukarabati wa hospitali ile. Hospitali imejengwa enzi ya mkoloni, lakini kila ilipokuwa inaguswa kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati, ilikuwa haiwezekani, inaharibika zaidi. Wakafanya maamuzi ya kujenga majengo mengine. Sasa ardhi imejaa, hospitali imejaa, haiwezekani tena kwenda kuongelea majengo.

Mheshimiwa Spika, sisi ardhi tunayo, tunaomba mtujengee Hospitali yetu ya Wilaya ili tuweze kupata huduma bora. Kiukweli kuendelea kujenga Zahanati na Vituo vya Afya, kama hatuna huduma za kutosha ni sawa sawa tutakuwa tumejenga magofu, hali ya afya bado ni ngumu. Fanya tathmini ya Wabunge wote wanaochangia hapa ndani, hizi ndiyo changamoto wanazozitaja. Vinginevyo ni kwa sababu tunatakiwa tuendelee kuchangia, lakini vinginevyo changamoto zako ambazo unatakiwa kwenda kuzifanyia kazi Mheshimiwa Waziri zote zinatamkwa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna changamoto kubwa sana kwenye dawa. Inawezekana kuna tatizo MSD na Serikali, sijui ni ipi, lakini inawezekana kuna tatizo. Mwingine amezungumzia suala la wizi. Wizi kweli haukwepeki. Ni lazima tunapotoa hizi fedha tuangalie na mfumo wa udhibiti wa dawa. Ni lazima tuangalie mfumo wa udhibiti, ni mbaya mno. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Hospitali yangu ya Wilaya mwaka 2010 population ya watu ilikuwa 150,000. Ndani ya miaka 10 tu leo tunaenda kuzungumzia watu 200,000, bado hospitali ni ile ile ya mwaka 1970, hatuwezi kufika. Tunaendelea sana kujitahidi na tunampongeza sana Mheshimiwa Rais, lakini tunambebesha tena huu mzigo mwingine, bado huduma ya afya siyo salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda vijijini ukianza kuzungumzia suala la Bima ya Afya, wanakijiji wanaweza wakakutukana matusi. Hawaelewi suala la huduma ya Bima ya Afya, kwa sababu anabeba kadi yake, akienda hospitalini hapati huduma. Bado utamshawishi huyo mtu akate bima! Ya nini?

Yaani umeenda hospitalini na kadi yako na unaambiwa dawa hamna. Hakuna sababu. Kwa hiyo, wananchi hao pia kuzungumza nao kuhusu kuwashawishi kukata huduma za bima, inakuwa ni vigumu sana kwa sababu ni wagumu pia kuelewa pia kwamba kweli wakienda na hizo kadi wanaweza kupata huduma katika hospitali.

Mheshimiwa Spika, haya niliyozungumza ndiyo changamoto ya Tanzania yetu. Mheshimiwa Waziri naomba uyapokee, uyafanyie kazi. Vile vile napenda sana utembelee kwenye jimbo langu baada ya Mkutano huu kuahirishwa ili ukajionee haya ambayo nimekwambia.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kuunga mkona hoja. (Makofi)