Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

Hon. Tecla Mohamedi Ungele

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Awali ya yote nampongeza Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kujali afya za Watanzania, na wote tunashuhudia miundombinu mbalimbali imejengwa sehemu zote nchini Tanzania kwa ajili ya huduma za afya.

Mheshimiwa Spika, pia hata bajeti naona inaendelea kuongezeka kidogo kidogo kwenye Fungu Na. 52, lakini naamini Mheshimiwa Rais kwa sababu anajali afya ya Watanzania, ataendelea kuongeza siku hadi siku.

Mheshimiwa Spika, pia napongeza Wizara ya Afya; Mheshimiwa Ummy Mwalimu na timu yake yote mpaka kule vijijini kwenye ngazi ya kaya, watoa huduma za afya wanaendelea kutoa huduma na ushauri nyumba kwa nyumba.

Mheshimiwa Spika, najikita kwenye magonjwa yasiyoambukiza. Magonjwa yasiyoambukizwa ni tatizo kubwa na ni kilio kikubwa nchini Tanzania, pia ni gharama kwenye matibabu na athari yake ni kubwa sana. Wote tunashuhudia, miaka iliyopita hakukuwa na tatizo kubwa la shinikizo la damu, wala moyo wala sukari, lakini sasa hivi kila familia, na kama siyo kila familia hiyo, basi hata jirani yako anakumbwa na tatizo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sababu za magonjwa yasiyoambukiza, machache ni mtindo wa maisha tunayoishi, vyakula vyetu, kutokufanya mazoezi, utumiaji wa tumbaku, matumizi makubwa ya sukari na kadhalika. Vitu hivi vinaweza vikazulika. Ukubwa wa tatizo, tunaona wakati wa janga la UVIKO lilivyoshamiri wagonjwa katika hospitali moja kule Dar es Salaam ilitoa taarifa kwamba asilimia 86 ya vifo ilitokana na wagonjwa ambao tayari walikuwa na kisukari, lakini asilimia 65 ya vifo vile vya UVIKO 19 tayari wagonjwa wale walishakuwa na shinikizo la damu na asilimia 45 tayari walishakuwa na pumu. Hivyo unaona magonjwa yasiyoambukiza ukiwa nayo, ukipata ugonjwa mwingine hali inakuwa ngumu zaidi.

Mheshimiwa Spika, tunaona pia hata mfuko wetu wa Bima ya Afya unalemewa kutokana na magonjwa yasiyoambukiza. Hata Mkoa wa Lindi kwenye Wilaya ya Nachingwea kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wenye magonjwa yasiyoambukiza kama presha na kisukari.

Mheshimiwa Spika, sasa nini kifanyike? Ni ushauri wangu kuwa imefikia wakati sasa naomba tume maalum ya kupambana na magonjwa yasiyoambukiza ianzishwe, kama vile tulivyoanzisha TACAIDS. Kwa nini nasema hivyo? Tunaona sababu zinazoleta magonjwa yasiyoambukiza nyingi ni za kijamii; mtindo wa maisha, kutokufanya mazoezi, consumption ya tumbaku; pia tunaona sababu nyingi ni za kiuchumi. Sehemu nyingi katika nchi yetu, tumbaku ndiyo uchumi, miwa ndiyo uchumi, na pombe ndiyo uchumi. Sasa tunafanye kujikwamua? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukiachia suala la magonjwa yasiyoambukiza kwenye afya peke yake itakuwa ngumu kama ilivyotuumiza kwenye UKIMWI. Hivyo basi, tuliache jambo hili, afya waendelee kushughulikia matibabu, lakini pia kijamii tuendelee kuwa na mkakati maalum wa kuendelea kushughulikia magonjwa yasiyoambukiza. Tunaona hata wakati wa masuala ya UKIMWI, sasa hivi tayari wenye maambukizi ya virusi vya UKIMWI wana uwezo kabisa wa kutambua kwamba hapa nifanye jitihada za kuzuia ili nisipate maambukizi mapya. Pia wale hawajapata kabisa, jamii inaelewa kwamba tusipate maambukizi mapya.

Mheshimiwa Spika, hivyo basi, naomba hata kwenye magonjwa yasiyoambukiza, suala hili tuliache kwenye jamii, kwa sababu ni suala mtambuka, kila sekta ina husika kwenye masuala haya katika kuhamasisha kuzuia magonjwa yasiyoambukiza. Vinginevyo tutaendelea kugharamika bajeti itaendelea kuwa kubwa na kila familia itaendelea na simanzi kwa sababu ya athari ya magonjwa yasiyoambukiza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)