Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

Hon. Catherine Valentine Magige

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii ya Afya inayoongozwa na mwanamke shupavu, jasiri ambaye halali usiku na mchana akihakikisha anamsaidia Mheshimiwa Rais kuboresha huduma za afya na si mwingine bali ni Mheshimiwa Ummy Mwalimu akisaidiana na kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mollel nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Rais Samia kwa kutoa fedha nyingi katika huduma ya afya ikiwemo afya ya wakinamama wajawazito na watoto. Vilevile tunaona hii Royal Tour pia fedha nyingi zitakazopatikana zitaenda katika huduma ya afya na kwenye kuboresha pia afya ya wamama wajawazito na watoto. Wanawake wa Arusha tunampongeza sana Mheshimiwa Rais Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais Samia kwa kutoa fedha kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa hospitali za rufaa za mikoa. Sisi wa Mkoa wa Arusha tunaomba hospitali yetu ya Mkoa ya Mount Meru iboreshwe ili iweze kuwatibu wananchi pamoja na watalii sambamba na uboreshaji wa hospitali hii tulikuwa tunaomba Madaktari Bingwa katika fani mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, nilitaka kufahamu ni kiasi gani cha pesa zimetengwa kwa ajili ya uboreshaji wa Hospitali ya Mount Meru ya Mkoa wa Arusha? Mkoa wa Arusha katika Jiji la Arusha tulikuwa tuna kiwanda cha dawa lakini kiwanda kile hakifanyi kazi muda mrefu sana. Kiwanda kile kilikuwa chanzo cha ajira kwa wananchi wa Arusha na mikoa iliyo jirani na Mkoa wetu wa Arusha. Vilevile kilikuwa kinaongeza mapato katika Jiji la Arusha. Tunaomba Serikali mliangalie hili, kiwanda hiki cha dawa cha Arusha kiweze kuanza mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampongeza Rais kwa kupeleka pesa nyingi katika ununuzi wa dawa na vifaatiba. Tumeona mwaka huu zimetolewa Shilingi bilioni 129 MSD, lakini cha kushangaza, kama Mheshimiwa Rais kaidhinisha Shilingi bilioni 129 kwenda MSD, ni kwa nini kuna upungufu wa dawa? Ina maana pale kuna tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kufanya mabadiliko MSD. Mabadiliko haya yatasaidia sana. Tumeona amemteua Mkurugenzi kijana ambaye tumeambiwa ana uzoefu katika masuala mazima ya dawa. Nina imani kabisa mabadiliko haya yataleta tija katika upatikanaji wa dawa na vifaatiba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile tumeona mjumbe wa bodi ni mwanamke. Jamani, tunaona mfano, alipo mwanamke haliharibiki neno. Mmeona mama Rais wetu ni mwanamke, mmeona wafanyakazi sasa hivi wanacheka, huyo ni Rais mwanamke. Kwa hiyo, Mwenyekiti wa Bodi kwa sababu ni mwanamke, waziri naye ni mwanamke, najua kabisa mambo yatakuwa mazuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri tunaomba sana mkajipange, Rais ameshatoa mwelekeao, miezi mitatu minne inawatosha kabisa kujipanga kuhakikisha wananchi wanapata dawa. Hatutaki tena kusikia sababu sababu, tunachotaka wananchi wapate dawa na vifaatiba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bado kuna upungufu wa madaktari. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais, katoa ajira, wameajiriwa katika Sekta ya Afya wafanyakazi wengi, lakini hawatoshi. Tunaomba atoe ajira zaidi kwa wauguzi na wakunga ili wananchi wasipate changamoto tena. Vilevile tumekuwa tukisikia changamoto katika Hospitali za Serikali juu ya huduma. Wizara ya Afya tunaomba mliangalie hili mhakikishe changamoto hizi zinafikia ukomo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais, vilevile tunashukuru Wizara nzima ya Afya, Katibu Mkuu, Mheshimiwa Ummy na Mheshimiwa Dkt. Mollel, mnafanya kazi kubwa sana. Tunaomba changamoto hizi ndogo ndogo tunajua haziwashindi. Afya ndiyo kila kitu, tunawaamini, tunaomba mfanye kazi mwendelee kuchapa kazi.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Ummy Rais amekuamini na hujawahi kumwaibisha Rais. Tunaomba dada yangu Mheshimiwa Ummy ufanye kazi kwa bidii, tuna imani kubwa na nyie, tuna imani kubwa na Naibu Waziri, Katibu Mkuu; Mkurugenzi mpya wa MSD, na wewe na Mwenyekiti wa Bodi. Hatutaki tena kusikia changamoto za dawa na vifaatiba.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru naunga mkono hoja. (Makofi)