Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

Hon. Husna Juma Sekiboko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa fursa leo tena kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu na kuchangia Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Mama yetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa maamuzi yake ya upendo sana kwa kuongeza kima cha chini cha mshahara mpaka asilimia 23.3. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri, dada yangu Ummy Ally Mwalimu kwa kazi kubwa anayochapa kwenye Wizara hii akiambatana na kaka yangu pale Mheshimiwa Dkt. Mollel. Kwa kweli katika Wizara ambazo sisi Wajumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii tunakuwa comfortable nazo ni pamoja na Wizara ya Afya. Tunawapongeza sana, tunawapongeza sana ongezeni hiyo spirit ya kuwajibika kwa ajili ya nchi yetu ili tuweze kutengeneza maisha bora kwa kila Mtanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesimama leo kwa ajili ya jambo moja tu, huduma ya mama na mtoto. Huduma ya mama na mtoto ukisoma Sera ya Afya, ukisoma miongozo yote ya afya inaeleza namna gani Serikali imepanga kuokoa vifo vya mama na mtoto hasa kwa kuondoa tozo na fedha zote ambazo mama mjamzito na mtoto mchanga wanaweza kugharamia kipindi hicho.

Mheshimiwa Spika, uhalisia ulivyo ni tofauti kabisa na miongozo yetu inavyotolewa. Nimshukuru sana mchangiaji aliyemaliza Mheshimiwa Munde ameligusia na ametoa msisitizo vizuri kwamba hali ilivyo ni tofauti kabisa na miongozo ambayo inawekwa mezani.

Mheshimiwa Spika, nitakupa mfano wa baadhi ya maeneo, Kilindi kuna Kata moja inaitwa Kwasunga ipo zaidi ya kilometa 100 kutoka kwenye Kituo cha Afya Mkata. Akina mama wa Kwasunga wanajifungua njiani kuelekea kwenye kituo cha afya. Lakini pamoja na kwamba wanajifungua njiani wakifika hospitalini kwenye Kituo cha Afya Mkata hawana fedha, hawapati huduma. Kama siyo fedha waende na ile package, gloves na nini kwa ajili ya kwenda kujifungulia. Lakini ukija kwenye utaratibu wa Sera na Miongozo inasema huduma ya mama na mtoto ni bure.

Mheshimiwa Spika, niliombe Bunge na niiombe Serikali kama kuna sehemu tunataka kufanya siasa siyo kwenye huduma ya mama na mtoto. Huduma ya mama na mtoto ni ustawi wa Taifa letu kwa ujumla, ni eneo ambalo ni nyeti na ndiyo inasababisha kwenye ustawi wa shughuli zetu za maendeleo kama tutakuwa na mama mwenye afya akajifungua mtoto mwenye afya bora. Sasa bila kusimamia kwa dhati kwa sababu Sera zipo, Miongozo ipo lakini utekelezaji umekuwa mgumu. Bila kusimamia eneo hili la utekelezaji sawasawa bado tutakuwa tunafanya siasa na kifo cha mama na mtoto nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pale Majengo–Korogwe Hospitali ya Wilaya yameshatokea haya akinamama wameenda kujifungua wameombwa fedha bila fedha na wanapiga simu. Mheshimwia Waziri nataka nikwambie moja ya eneo ambalo nimetangaza vita na watoa huduma ya afya kwenye Mkoa wa Tanga ni hili la afya ya mama na mtoto. Nimewapa namba zangu za simu wale akinamama wakishamuingiza kwenye kumi na nane mtoa huduma anayeoomba fedha, Mheshimiwa Waziri nitamsukumia kwako na ikitokea umechukua muda Mheshimiwa dada yangu Ummy Mwalimu nakupenda sana lakini kwenye eneo hili kama haitapatikana tiba ya dhati ya kuondoa kweli kwa dhati na kwenye utekelezaji ikaonekana kwamba mama na mtoto wanapata huduma bure. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sitaki kusema naweza kushika Shilingi ya Mheshimiwa Waziri. Lakini eneo hili ni gumu, eneo hili linatia uchungu akinamama wanapata shida, kipato chao ni kidogo hata hicho ambacho Serikali imeamua kukitengeneza kwa ajili yao na chenyewe hakipatikani. Namuomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya windup atoe maelekezo ya Serikali ni kwa namna gani wataenda kusimamia perpendicularly kwa dhati kabisa mama na mtoto apate huduma bora bila malipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)