Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

Hon. Munde Abdallah Tambwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii na mimi naweza kuchangia Wizara ya Afya. Kwanza kabisa nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama ndani ya Bunge Lake Tukufu. Lakini nikushukuru wewe binafsi kwa kunipa fursa hii. Niwapongeze Wizara nzima ya Afya akiwepo Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, Naibu wake kaka yangu Mollel lakini Katibu Mkuu wa Wizara hii na watumishi wote kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu ameendelea kuipa fedha Wizara hii nyeti ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuchangia kwa sababu muda hautoshi kwamba 2021/2022 tulipewa fedha Shilingi Bilioni 129 kwa sababu ya dawa. Nikiongea harakaharaka pia tulipata Shilingi Bilioni 500 hela za UVIKO zilienda Wizara ya Afya. Lakini masikitiko makubwa kwenye hospitali zetu kulikuwa hakuna dawa. Hili ni jambo la kusikitika na ni lazima kama Wabunge tuseme. Nimuombe sana Mheshimiwa Waziri afuatilie fedha zinazotoka kwamba ziende zikafanye kazi iliyoambiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unashangaa Shilingi Bilioni 129 lakini hauoni mrejesho wa dawa ambazo ziko hospitali. Sijui MSD kuna tatizo gani au kuna tatizo gani, siwezi kujua lakini naiomba Wizara ifuatilie kwa nini dawa hazikwenda kwenye hospitali zetu. Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Rais alisema pia fumua MSD unasubiri nini? Unasubiri nini fumua MSD watu wa-deliver, watu wapate fedha zinazokwenda, wananchi wazione, wajue Rais wao anafanya kitu gani. Hauwezi ukapeleka Shilingi Bilioni 129 hospitali hakuna dawa. Nikuombe sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoe pongezi zangu za dhati kwa Mkurugenzi mpya wa MSD mpya aliyechaguliwa. Tumuombe akafanye kazi vizuri, yeye ni kijana, tunamjua ni mzooefu, alikuwa anafanya kazi USAID. Tunajua ana exposer kubwa. Tunakufahamu, tunakuona comment zako kwenye mitandao ya kijamii. Tunajua uwezo wako, nenda ukafanye kazi za watanzania. Uhakikishe dawa zinafika kwenye mahospitali. Kufanya kazi vizuri siyo kuweka program zako vizuri za kiofisi wakati tukienda hospitali hatukuti dawa, utakuwa haujafanya kazi vizuri. Hakikisha hospitali inapata dawa na safari hii Serikali imetenga Shilingi Bilioni 200 kwa ajili ya dawa peke yake. Shilingi Bilioni 200 kwa ajili ya dawa, tunaimani tutaona dawa kwenye hospitali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunakuomba sana usiogope, uende ukafanye kazi. Tunajua uweledi wako, tunajua una-exposer, tunakujua, tunakufahamu hata wewe kama hutufahamu sisi watu wa mtaani huko tunakujua. Kwa hiyo, nenda kafanye kazi wewe ni kijana, una kesho nyingi, ukiharibu hapo utakuwa umejiharibia mambo yako mengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, dawa zifike kwa wakati. Unakuta kuna cycle dawa zinatakiwa zifike tarehe 15 kwenye Mkoa wa Tabora, wanakuwa na dawa wanatumia mpaka tarehe 15. 15 inafika dawa hazijafika, zinafika tarehe 22. Watu wakienda pale wanalalamika kwamba hatujapata dawa, kumbe dawa ni uzembe tu wa kuzifikisha kwa wakati. Nimuombe sana Mkurugenzi wa MSD aende akafanye kazi yake kwa uweledi kwa kupanga mipango ya uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimwambie pia katika dawa atakazonunua ahakikishe anaweka package ya kujifungulia ya mama na mtoto. Hii imekuwa kero sana. Tunasema wakinamama wakijifungua, wakajifungue bure, wakifika pale package kama hamna inabidi akanunue, atajifungulia kitu gani haipo hospitali. Kwa hiyo, nimuombe kwenye bajeti zake aweke package ya kujifungulia ni kitu cha muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kupekea hii fedha nyingi kwenye hospitali zetu zote za Rufaa za mikoa yetu yote Tanzania nzima, tunampa hongera sana. Nimpongeze tena Rais kwa kuweza kujenga Hospitali ya Mama na Mtoto kwa mara ya kwanza katika Tanzania, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongee, sisi Tabora tumepata fedha nyingi sana, tumepata jengo la emergency la kisasa, mambo ya CT scan tumepata na kadhalika. Lakini tuna changamoto moja ndogo, nimuombe Mheshimiwa Waziri. Tulikuwa tumepangiwa kujengewa Hospitali ya Kanda kwenye Mkoa wa Tabora, tukaonesha na eneo, mpaka leo hamna Hospitali ya Kanda. Tatizo ni nini Mheshimiwa Waziri? Naomba ukija hapa utuambie kwa nini Hospitali ya Kanda haijaanza kujengwa kwenye Mkoa wa Tabora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hospitali yetu tuliyonayo ya Mkoa imejengwa 1906 ikiwa kama kituo cha kupokelea majeruhi wa kivita wa Mkoloni ndiyo hospitali tuliyonayo. Miundombinu imechakaa, kwa maana miundombinu ya maji na umeme imechakaa kwa kiwango kikubwa sana. Nimuombe sana Mheshimiwa Waziri tunaomba mtujengee Hospitali ya Kanda kama mlivyotuahidi siku zote kwenye Mkoa wa Tabora. Mheshimiwa Ummy akiwa Waziri kipindi kilichopita, ulikuja na ulituahidi Hospitali ya Kanda katika Mkoa wa Tabora itajengwa, tunaomba sana mtujengee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, upungufu wa Madaktari, tuna Madaktari Bingwa katika Hospitali yetu ya Rufaa ya Tabora watatu tu, yupo wa watoto na wanawake. Tunaomba tupate Daktari Bingwa hata wa upasuaji Mheshimiwa Ummy. Masuala ya upasuaji watu wanakufa, hatuna Daktari Bingwa. Hatuna Daktari Bingwa wa dawa za usingizi, mtu akiingia theater mara nyingi watu wamefariki, hatuna Madaktari Bingwa. Tunaomba Madaktari Bingwa wawepo hata ikitokea kufariki basi iwe ni bahati mbaya siyo kwa sababu hakuna Madaktari Bingwa. Hata mmoja akiwa wa upasuaji kwenye Mkoa mzima tukimpata itakuwa imewasaidia sana wananchi wa Mkoa wa Tabora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nirudie tena kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya. Ametoa ajira tunajua kwenye Wizara ya Afya ametoa ajira 10,000. Tunaamini hata Tabora na sisi tutapata watumishi wa Wizara kwa sababu kwa kweli watumishi ni wachache sana na inatokea kuleta malalamiko kwamba labda Wizara ya Afya haifanyi kazi vizuri. Tukienda hospitali Madaktari hawatuhudumii, Manesi lakini Manesi wanachoka.

Mheshimiwa Spika, niliwahi kulala na mgonjwa kwenye wodi moja ina vitanda 40. Kitanda kimoja watu wawili, watu 80 lakini yuko Nurse mmoja anahudumia usiku kucha. Heri ni wewe utamuonea huruma Nurse, huyu amemaliza dripu, huyu anatapika, huyu anataka kwenda kujisaidia, halafu wanasema wasilale na ndugu, yuko Nurse mmoja. Niliyepata bahati ya kuingia nilikuwa namwambia Nurse kamuwekee yule dripu acha nimfutie huyu matapishi, yaani unajisikia kuumia kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwaombe Wizara ya Afya pale mnapoona Ma-nurse ni wachache, ruhusuni ndugu wa mgonjwa walale hospitali. Tusifate tu kwamba Ulaya hawalali hospitali, wenzetu wana Ma-nurse wengi, wanaweza kumuhudumia mgonjwa kwa wakati unaoweza kustahili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Waziri Ummy Mwalimu. Waziri Ummy tunakujua, tunakufahamu, tumefanya kazi na wewe muda mrefu. Ni Waziri mahiri, ni mchapakazi, tunaomba uende MSD ukafanye kazi MSD. Uifumue MSD kama ulivyoambiwa na hatimaye tuone matunda kwa kupata dawa kwenye Hospitali zetu za rufaa, zahanati na vituo vya afya, tuombe sana. Lakini tumuombe mtu wa MSD, mmeagizwa mnunue dawa kwa owners ili dawa ziwe kwa bei rahisi. (Makofi/Vigelegele)

SPIKA: Sekunde 30 malizia.

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema kwamba niwaombe Waheshimiwa Wabunge twendeni tukaseme mambo mazuri yanayofanywa na Rais wetu Samia Suluhu Hassan. Tumeona kwenye Wizara fedha alizozitoa, haijawahi kutokea kupeleka Shilingi Bilioni 500 kwenye Wizara ya Afya. Twendeni tukahakikishe Watanzania hawajawahi kumpigia Rais mwanamke kura, 2025 apigiwe kura za heshimiwa kubwa sana kwa kazi nzuri anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)