Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana mimi kuniruhusu nichangie hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maji kwa mwaka 2022/2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza na mimi naunga mkono pongezi zinazotolewa na Wabunge wenzangu kwa Wizara hii kwa ndugu yangu/mdogo wangu, Jumaa Aweso na Naibu Waziri Maryprisca Mahundi kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara hii kwa kushirikiana na wenzao Mheshimiwa Katibu Mkuu Engineer Sanga na watumishi wengine wenye nidhamu nzuri sana katika Wizara hii hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi cha muda mfupi sana Wizara hii, Waziri huyu na wenzie wameokoa mamilioni ya fedha kutoka kwenye miradi iliyokuwa chechefu na hii haijapata kutokea kwa sababu miradi hii mingine imekaa miaka nenda rudi. Lakini pia nimehudhuria uzinduzi na Mheshimiwa Rais wa miradi mbalimbali kule Simanjiro Mugango, Kiabakari, Butiama na Misungwi. Miradi hii ilikuwa mikubwa sana na imepewa fedha na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na umeisimamia vizuri sana. Wizara hii haiwezi kupita bila hongera kubwa kutoka kwa Wabunge wote kwa sababu kila mahali Wizara hii imegusa tuwapongeze na hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze pia kwa kazi nzuri ya kuyavuta maji kutoka Ziwa Victoria na kuyapeleka kwa babu zao Wanyamwezi Tabora, Igunga, Nzega na Uyui; maji yenye thamani ya Shilingi Bilioni 615 na mradi ule umesimamiwa na unafanyakazi vizuri hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia sisi Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji tulitembelea miradi ya Kimbiji pamoja na Kisarawe II, ambayo ni miradi mikubwa imekaa muda mrefu sasa wameikwamua na inaendelea vizuri hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la upatikanaji wa fedha, ni lazima tuipongeze Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwapa fedha Wizara hii kwa kiwango cha asilimia 95 cha mahitaji yao ya fedha zilizokuwa zimepangwa. Hongera sana mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo changamoto katika Wizara hii ambazo hatuwezi kukaa kimya kwa sababu tunataka tuwasaidie na wao waweze kutusaidia. Kwanza, ukosefu wa mafundi, fundi mchundo na fundi sanifu. Miradi hii mikubwa ya maji ambayo tumeongelea hapa imefanikiwa kujengwa vizuri itahitaji matengenezo. Mimi ninashauri Wizara hii ifanyekazi karibu sana na Chuo chao cha Maji na wakiwezeshe, ili hatimaye wapate mafundi wa kutengeneza miradi hii itakapoharibika. Pia liko suala la kupungua kwa maji.

Wizara na Mamlaka zake zote za maji na RUWASA waanze sasa kufikiria jinsi ya kuhifadhi na kulinda vyanzo vya maji hasa Mito na ardhi oevu, kuvuna maji ya mvua, na ikiwezekana kuhifadhi maji hayo katika mabwawa makubwa badala ya kuacha yakapotea. Maji haya yanaweza kutokana na madaraja ya kwenye reli lakini pia na madaraja ya barabarani badala ya kuachwa yakafanye mafuriko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, suala la kumalizia miradi ambayo imeanzishwa mikubwa lakini bahati mbaya sana haikamiliki. Mfano mzuri, tulikuwa na mradi wa Ziwa Victoria kuleta maji Uyui, Tabora, Nzega na Igunga. Katika Jimbo langu la Tabora Kaskazini kulikuwa na vijiji kadhaa ambavyo vimeorodheshwa; na Wizara hii ilibakisha fedha (bakaa) Shilingi Bilioni 25 na miradi hii kwenye vijiji hivyo ninavyovitaja vijiji vya Ikongoro, Kanyenye, Kiwembe, Mbiti na Mogwe gharama ya miradi ile yote kwenye vijiji hivyo ni kama Shilingi Bilioni 5 hivi. Walikuwa na Shilingi Bilioni 25 lakini vijiji vile mpaka leo havijapata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina hakika hii hali ya kuacha miradi na fedha zipo inatuletea kasoro katika Wizara hii na mimi ninafikiri, Mheshimiwa Aweso na wenzake watarekebisha mara moja ili miradi itakayoanza na ambayo ina fedha ikamilike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo pia suala la makusanyo ya masurufu au fedha kwa ajili ya mamlaka zao za maji na RUWASA. Sasa hivi tunakusanya fedha hizi kwa kutumia dira au mita za maji, na kuna wasomaji. Sio vibaya ndugu yangu Mheshimiwa Waziri Aweso, Naibu Waziri na Katibu Mkuu mkaiga wenzenu wa TANESCO ambao waliiga mita za LUKU kutoka Afrika Kusini. Si vibaya na ninyi mkaiga hizi mita za LUKU; na tena niwapeni njia rahisi, mkaziita Lipia Maji Kadri unavyotumia (LUMAKU) na watu watakuwa tayari kulipia hayo maji kabla ya kuyatumia. Hii itaingiza mapato ya kutosha kwenye mamlaka za maji lakini pia RUWASA. Pia itaondoa gharama za udanganyifu wa watu wanaokwenda kusoma mita ambao ni chechefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mradi wa Miji 28, tumeusikia; mimi naunga mkono, kwamba Waziri amesema kabla ya bajeti hii kabla ya mwezi Juni, mradi huu utaanza na kwamba Mheshimiwa Rais ameunga mkono na ameridhia mradi huu uanze. Hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nautaja mradi huu kwa sababu nami utanipitia utakapopita kwenda Sikonge. Utakapokwenda Urambo vijiji vyangu kadhaa vitapata maji na kutimiza jumla ya vijiji 58 katika Jimbo langu. Ukipita kwenda Urambo Vijiji vya Kata za Ndono, Ufuluma, Makazi, Mabama, Lakasisi A, Kalola na Isila vitapata maji kwa sababu viko ndani ya ile kilometer 12 za bomba la maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, Mungu awatangulie na awape afya njema Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Jumaa Aweso, ndugu yangu Maryprisca Mahundi, Engineer Sanga na watumishi wote wa Wizara hii ya Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)