Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Issa Jumanne Mtemvu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi nichangie kwenye wizara hii. Kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Ndugu yangu Jumaa Aweso Mbunge na Naibu Waziri dada yangu Mahundi na watendaji wao wote wa wizara hii ya Maji, Fungu 49.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ukweli kazi wanayoifanya ni kazi kubwa ni kazi ya kizalendo nchi yetu ni kubwa. Miradi inayohitajika ni mingi na maji hayana Subira. Mwananchi uweze kumwambia usubiri maji kesho au kesho kutwa hali ya maji ni muhimu kupatikana kwa wananchi wetu kwa haraka na kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, Nampongeza kwa niaba ya Wananchi wa Jimbo la Kibamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya Mwaka 2021/2022 nilizungumza hapa, nikalia kwa muda sana na nikasema kwenye maswali yangu ya msingi naya nyongeza mliyonipa nafasi ya kuuliza, juu ya tanki ya mradi mkubwa pale mshikamano ambao utakuja kuwa majibu ya sehemu kubwa ya Jimbo la Kibamba. Mheshimiwa Rais alisikia kupitia mwamvuli wake Mheshimiwa Waziri, alifika jimboni mwezi wa nane mwishoni mwaka jana na kusaini mkataba ule hadharani mbele ya wananchi wa Jimbo la Kibamba na tayari kazi ile kubwa inafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na nimshukuru sana, kwamba fedha zilizokopwa za tirioni 1.3 za UVIKO zilipelekwa zaidi ya bilioni 139 za maendeleo katika Wizara ya Maji fungu 49, na bilioni 2.5 zilitolewa kwenda Kibamba kwa ajili ya mradi huu wa mshikamano. Nikushukuru sana Mheshimiwa Rais na kwa usikivu wa waziri wako kwenye eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli, panakuwepo na mazuri mengi lakini vile vile na changamoto huwa zipo. Nifurahi tu, nifurahi kwa maana kimbilio la ukosefu wa fedha linaweza likatamkwa katika njia nyingine kama UVIKO ilienda kuongezea 139, lakini kila mwaka tunawapangia au tunawapitishia almost bilioni 680 katika Wizara hii. Lakini za maendeleo ni takribani bilioni 646 lakini walivyoongezewa na hizo 139 zikafika takriban bilioni 785, bajeti ya mwaka 2021/ 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kupanga na kupata ni vitu viwili tofauti hawa wanabahati sana wamepanga wamewekewa hizo lakini wamepokea takribani bilioni 743 ambapo taarifa ya Waziri inasema ni asilimia 95. Hii ni pongezi kubwa sana kwa Mheshimiwa Rais pia sana, sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama tunapata kile tulichokipanga kwa nini sasa miradi haitekelezeki kwa wakati? Kwanini miradi haitekelezeki kwa wakati? Wananchi wa Jimbo la Kibamba wanaendelea kulia na mimi huwa nalia hapa mwakilishiwao. Kibamba ndiyo imelisha Ubungo yote Jimbo la Ubungo kaka yangu Profesa Kitila Alexander Mkumbo yupo hapa. Lakini Kibamba ndiyo inalisha Pugu, kila siku nasema, I mean Kisarawe hadi na huko Pugu; mradi mkubwa umeenda Kibamba – Kirasawe, asilimia 95 wananachi wa kule kwa kaka yangu Jafo wanakunywa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hawana maji Jimbo la Kibamba. Tunaambiwa hapa asilimia 86 katika miji, nafurahi hiyo ni takwimu ya jumla na uwiano au average. Lakini ukienda specific Kibamba natamka tu maeneo machache na Mijini, na Waheshimiwa Wabunge hapa zaidi ya 50 wanaishi kwenye Jimbo la Kibamba na Mawaziri zaidi ya 15 wako. Ipo siku nitawataja kwa majina ili muweze kuona umuhimu wa Jimbo lile. Mimi nasema ni Dar es Salaam Vijijini, mkubali ni Dar es Salaam Vijijini kwa sababu wanahitaji attention kubwa ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme, maeneo ambayo ni maarufu na wananchi wanayajua na humu wote wanajua. Nasema Mpiji Magohe, Msumi, Msakuzi yote Kaskazini na Kusini hakuna maji kabisa. Vilevile, maeneo machache ya Kwembe, King’azi A nimezungumza watu wanakunywa maji machafu ya visima, machafu ya rangi na Mheshimiwa Waziri anajua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme, leo nilisema sitosema sana. Kazi mpaka sasa inafanyika. Sisemi kwamba hafanyi. Ipo miradi mitatu nimesema ukiondoa Mshikamano wa Mheshimiwa Rais, mradi wa Kitaifa. Nimesema mradi wa Kitopeni upo kwenye taarifa zao. Tuliahidiwa na Mheshimiwa Waziri tangu mwezi wa nane kwamba mwezi wa 12 tungepata hii miradi mitatu, ambayo ni Kitopeni, Mradi wa Mabwepande kule kwa Askofu Gwajima namuibia maji kwenye Tanki la Malolo kuja kilometa 8.2 hadi Mpiji Center kujazia pale Kidesa mpaka leo miezi sita imeongezeka. Christmas tutaenda na Waziri kunywa pale maji, hakuna miezi sita imeongezeka. Tenki pale kutokea Kwembe Kati kuelekea King’azi AB na Kilimahewa tumewaambiwa wananchi pale, tumeenda na Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Mbunge. Leo hawa viongozi ninaowataja hawawezi kwenda watapigwa mawe. Hawawezi kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri tumeahidiwa mimi na wewe, kwa nini tunadanganywa? Mpango mzuri ulionao ni kuongeza uwezo na kutoa mafunzo mazuri kwa Watendaji wako wa ndani kwa ajili ya kazi za extension na distribution zifanyike kwa wakati. Kama bado uwezo mdogo, muone jinsi na mikakati ya dharula kuiokoa Dar es Salaam maeneo ya pembezoni. Mimi nimekusifia kazi unaifanya vizuri kama kijana mwenzangu lakini kama unaangushwa, sisemi unaangushwa na Ruemeja; anafanya kazi mpaka mnamuongezea na Tanga, Korogwe, Same na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mimi niaombe sana, leo siwezi kumaliza kusema, jicho la Serikali lijielekeze Kibamba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante…

MHE. ISSA J. MTEMVU: …vinginevyo mtamuondoa Mheshimiwa Mtemvu Kibamba na siasa itaendelea kuwa ngumu sana katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.