Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Prof. Adolf Faustine Mkenda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rombo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa fursa hii. Naomba nianze kwanza kwa shukrani.

Kwanza naomba kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja yetu hii. Tumehesabu, tuna Wabunge 43 waliochangia na Wabunge kadhaa wameleta kwa maandishi. Tunaomba kuwahakikishia kwamba kila mchango uliotolewa hapa tutauzingatia sana tunavyosonga mbele na maoni mengi ambayo tumeyapata kwa kweli ni ya kufanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee kabisa, naomba niishukuru sana Kamati yetu inayotusimamia, Kamati ya Kudumu ya Bunge, maoni yao takribani yote tutayafanyia kazi. Wamekuwa wakitusimamia vizuri sana na kutuongoza. Hapa tulipofika kwa kweli, ni kwa sababu tumekuwa tukifanya kazi kwa pamoja. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge na ninaishukuru sana Kamati yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba vilevile nimshukuru Naibu Waziri, Mheshimiwa Kipanga. Nina bahati sana kupata Naibu Waziri mchapa kazi kama huyu, ananisaidia sana. Hii kazi ni teamwork ikiwa pamoja na Katibu Mkuu Prof. Sedoyeka pamoja na Manaibu Katibu Wakuu Prof. Mdoe na Prof. Nombo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee kabisa naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais. Mtakumbuka wakati anahutubia Bunge hapa mwezi wa nne mwaka 2021 katika vitu alivyovisema ilikuwa ni kutoa maelekezo kwamba, Serikali sasa ipitie mitaala ili iboreshe elimu na kuhakikisha kwamba elimu hii inaakisi mahitaji yetu na kweli inamwandaa mhitimu kuweza kuishi katika mazingira yetu na katika mazingira ya utandawazi. Amekuwa akirudia maelekezo hayo mara kadhaa na hata mimi aliponiteuwa kwenye Wizara hii alinipa maagizo kwamba kipaumbele chako ni kusimamia mageuzi makubwa kwenye sekta ya elimu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais aliliona hili mapema, Waheshimiwa Wabunge wameliona na takribani kila Mbunge aliyezungumza amegusia suala la mageuzi ya elimu. Sasa dunia nayo imeliona, dunia imetukuta tumeshaanza kazi kwa sababu Rais wetu tayari alikuwa ahead of the time. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, na kwa kweli, nashukuru sana vilevile kwa sekta yetu ya elimu kwa ujumla wake, kwetu sisi pamoja na wenzetu wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Kwa mfano, kwa upande wa mikopo ya elimu ya juu Mheshimiwa Rais alivyoingia ofisini alikuta tunatumia Shilingi bilioni 464 kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu, aliagiza iongezwe kufikia Shilingi bilioni 570 kwa mkupuo. Ndani ya mwaka mmoja tumeweza kuongeza vile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siyo hivyo tu, aliagiza tuondoe zile tozo; 6% ya kutunza fedha na 10% ya adhabu ili kumpunguzia mzigo mtu aliyenufaika na mkopo huu wakati wa kuweza kurudisha na vilevile fedha zile ambazo zilikuja kutoka IMF alizielekeza katika sekta ya elimu vile vile. Sisi kwetu tulipata takribani Shilingi bilioni 65, lakini kwa ujumla wake sekta nzima ya elimu ilipata takribani robo ya fedha hizi kwa ajili ya kusaidia elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi naona tunapoenda legacy ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wetu inawezekana itakuwa katika eneo la elimu. Namshukuru sana Makamu wa Rais vile vile na Waziri Mkuu wanamsaidia Rais vizuri sana kutusimamia sisi katika utendaji wetu wa kazi. Naomba nikushukuru sana nakupongeza tena wewe kwa kazi nzuri unayofanya kutusimamia kuendesha Bunge letu na Naibu Spika wetu na Wenyeviti wote wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe shukrani vile vile kwa wapiga kura wote watu wa Rombo kwa kunihakikishia kwamba naendelea kuwa hapa.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba nijibu hoja zile specific, na ni nyingi. Nyingine Waheshimiwa Wabunge wanaswma kwamba mimi nahitaji VETA, hapa tunahitaji High School; tumeziandika na tutaenda kuziangalia namna ya kutekeleza kwa sababu tutaangalia kwenye bajeti tumeweka kiasi gani. Kuna mahali pengine tunaambiwa twende; kwa mfano Mheshimiwa Maganga, kwenda kuona kule katika maeneo yake, hayo yote tutayafanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi sitaenda sana kwenye specific nitaenda katika masuala mapana ya kimkakati.

Mheshimiwa Spika, la kwanza; hoja ilitolewa kwamba na ilitolewa na Mheshimiwa Sanga na nadhani kila mtu alipiga makofi kwa sababu kila mtu anaamini hivyo; kwamba katika sekta ya elimu tusiwe tunabahatisha na kukurupuka na kubadilisha. Kwamba, akija huyu twende kushoto akija huyu twende kulia akija huyu songa mbele akija huyu rudi nyuma. Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge, kwanza mimi binafsi kunieleza hivyo its like preaching to the Pope himself; kwa sababu hatuamini kwamba Wizara hii inahitaji kufanya maamuzi bila kutafakari vya kutosha na bila kushirikisha wadau vya kutosha. Hii si Wizara ya kubadilisha badilisha mambo bila kuwa na utafiti wa kina. Hii si Wizara ya kusema kuna la Mkenda la Ndalichako wala la Kawambwa. Hii ni Wizara ya Serikali ya Watanzania na jukumu letu ni kuhakikisha kwamba tunatumia mifumo yetu yote kwa ajili ya kufanyia maamuzi, na ndivyo tunavyokwenda; na ndiyo maana suala la mageuzi ya mitaala nimelikuta halikuanza na sisi lilikuwa limeanza na Mheshimiwa Ndalichako.

Mheshimiwa Spika, tunapitia Sera; hii ilipita wakati wa Mheshimiwa Kawambwa. Mambo mengi ambayo tunayafanya sasa hivi yako katika ripoti ya Jackson Makweta 1982. Kwamba tunarudi nyuma kuangalia ni nini ambacho hatukutekeleza? Lakini pamoja na yote hayo tunaendelea kushirikisha wadau. Waheshimiwa Wabunge tulikuwa na semina pamoja, tulikuwa na ya kutosha kueleza Wabunge, tukasema hatuji sisi kueleza tunakuja elezwa. Kwa hiyo tuliweka kila kitu kilichoko pembeni tukasikiliza maoni tumeahidi tutarudi tena, uturuhusu tukishakamilisha tutakuja sasa kueleza tumekusanya nini kabla kuingia kwenye mchakato wa kufanya maamuzi.

Mheshimiwa Spika, la pili labda niseme hili highlight moja kubwa, na ninaisema hii kwa sababu nataka kuhimiza wadau wengi watusaidie. Nimesema Mheshimiwa Rais ametusaidia kuongeza mkopo wa elimu ya juu, na ilikuwa ni big jam pamoja na kuondoa zile tozo ambazo zilikuwa zinasababisha kurudisha mkopo unakuwa kazi kubwa sana. Lakini vile vile Wizara imeamua kuongea na taasisi mbalimbali kuhakikisha kwamba tunaongeza fursa za mikopo kwa ajili ya elimu.

Mheshimiwa Spika, hapa nataka niitaje NMB, na nimtaje specifically mkuu wa NMB Ruth Zaipuna. Kwa sababu yeye baada ya mazungumzo amekubali kutenga bilioni 200 kwa ajili ya mikopo. Yapo masharti, tunaendelea ku- negotiate tuone unafuu utakuwa mkubwa kiasi gani. Fursa hii itatuwezesha sisi si kutoa tu mikopo kwa elimu ya juu itatoa fursa kwa wafanyakazi wanaotaka kwenda kujiendeleza kielimu na itatoa fursa kuhakikisha kwamba hata wazazi wanaweza kupeleka watoto wao kwenye elimu ya juu. Tumeshatoa maelekezo kwenye Bodi ya Mikopo kuhakikisha kwamba wanaangalia kwenye bajeti itakayokuja 2023/2024. Bajeti ambayo itafuata baada ya hii kukamilika tuwe tumeshajipanga kuhakikisha kwamba tunatoa scholarship kwenye vyuo vyetu vya ufundi na pengine VETA katika hali ya juu ili tuhakikishe kwamba yale maeneo ambayo mtu akipata mkopo anaweza akaajirika kirahisi na kurudisha fedha basi tunapeleka fedha kule. Kwa hiyo nawashukuru sana NMB, naomba benki nyingine zote tuendelee na mazungumzo, kwa sababu tunaendelea. Bado kuna fursa ya kuongeza wigo kwa kutoa mikopo kwa wanafunzi wetu.

Mheshimiwa Spika, tunaongea na Private Sector ambayo siyo banking. Na wakati nawasilisha hapa jana alikuwepo bwana mmoja anaitwa Rupin Rajani alikaa pale juu pale. Huyu tulizungumza, nikamwambia hebu jaribu kutengneneza aina fulani ya private foundation watu binafsi ambao wanaweza wakatafuta fedha kusaidia Watanzania kwenda kusoma nje kwenye Vyuo vya hali ya juu kama MIT Harvard na kadhalika. Alienda Marekani amerudi akaniona akanipa brief nzuri sana; na tutakuwa na mkutano tarehe 14 jioni nyumbani kwake Dar es Salaam. Amenieleza kuna matumaini makubwa sana watu binafsi wa ndani na nje kukaa chini na kuangalia uwezekano wa kuanzisha foundation ya kukusanya fedha kusaidia Watanzania wanaotaka kwenda kusoma nje hasa katika maeneo ya sayansi teknolojia na tiba.

Namshukuru sana ndugu yangu Rupin Rajan na alikuja hapa Dodoma nikamualika akarudi Dar es Salaam akaja asubuhi hapa kuja kusikiliza hotuba yetu ya bajeti naomba wadau wengine wote ambao tutakutana nao tushikane mkono kwa sabbu private sector ina nafasi kubwa sana ya kufanya hapa.

Mheshimiwa Spika, lakini si hivyo tu, vile vile sisi ndani ya Wizara tumetenga fedha kwa ajili ya scholarship, tuna bilioni tatu. Nyingi zitaenda kwa vijana wanaomaliza Form Six watakaofanya vizuri sana katika masomo ya sayansi watakaotaka kwenda kusoma elimu tiba, sayansi na teknolojia watapata 100% scholarship kutoka kwa Serikali kama zawadi ya kufanya vizuri darasani.

Kwa hiyo wakati matokeo ya Baraza la Mitihani yatakapotoka wale watakaofanya vizuri sana kwenye PCM, watakaofanya vizuri sana kwenye PCB, masomo ya sayansi wakaotoka kwa wazazi wajue haijalishi mzazi ni tajiri ni maskini tutawasomesha asilimia 100.

Mheshimiwa Spika, lakini tutatoa fursa vile vile, upendeleo maalum, scholarship kwa watu wenye ulemavu watakaomaliza form six na ambao watakuwa wamefanya vizuri vya kutosha kwenda kuendelea na masomo ya shule. Kwa hiyo hizi hela tunaamini zitatusaidia wenzetu kwa ajili ya kwenda kusoma.

Mheshimiwa Spika, tumetenga fedha vile vile kwa ajili ya scholarship kwa ujumla wake kwa Wahadhiri wa Vyuo Vikuu Watanzania; Vyuo Vikuu vyovyote, Private na Government; ambaye atapata nafasi ya kwenda kusoma nje ya nchi yetu katika masomo ya sayansi teknolojia na tiba. Kiasi hicho cha fedha, kati ya hizo bilioni tatu tulizotenga pamoja na fedha za mradi wa HEET ambao tunakaribia kuanza kuutumia, tutatoa scholarship kwa hawa watanzania kwenda kusoma nje kwa sababu itatusaidia sana kupunguza tatizo la ajira katika Vyuo vyetu Vikuu. Kwa hilo kubwa tunakwenda nalo.

Mheshimiwa Spika, yapo mambo saba tuliyoyazungumza kwenye bajeti yetu katika kuendeleza elimu, na Wabunge wengi wameongelea humo humo. Niyaseme haraka haraka halafu nitoe ufafanuzi katika maeneo kadhaa.

Mheshimiwa Spika, moja, tulisema lazima tupitie hii sera, nitaeleza kidogo, mbili sheria, tatu mitaala, nne idadi ya waalimu, wakufunzi na wahadhiri, tano ubora wa walimu wakufunzi na wahadhiri, sita miundombinu na saba ni vitendea kazi.

Mheshimiwa Spika, tukisema tunabadilisha mitaala ni jambo zuri sana, tukisema tunabadilisha sera ni jambo zuri sana suala la idadi ya walimu na ubora wao miundombinu vitendea kazi hatutopuuza; na hiyo nimesikia Wabunge wengi sana wamesema. Kwamba sasa tukienda huku hatuna walimu wa kutosha hapa na kandalika.

Mheshimiwa Spika, twende kidogo kwenye Sera. Sera yetu sasa hivi ukiondoa pre-school sasa hivi unaweza ukai- define kwa structure tu ya elimu ni 7, 4, 2, 3 plus. Maana yake ni kwamba, miaka saba ya lazima, miaka minne ya 0-level, miaka miwili high school, miaka mitatu plus ya Chuo Kikuu, minimum Chuo Kikuu ni miaka mitatu kwenda juu.

Mheshimiwa Spika, labda niliseme hili kwa sababu limezungumzwa sana. Kenya walikuwa na utaratibu wa 8, 4, 4. 8 elimu ya lazima, 4 Sekondari na 4 Chuo Kikuu. Na ile ilikuwa inawafanya washindwe kuingia vyuo vikuu kwetu sisi kwa sababu sisi nasi tuna viwango na wakenya wengi walikuwa wanapeleka watoto nchi nyingine hasa Uganda ili waweze kupata access kwenye vyuo vingine vya nchi nyingine kwa sababu wao ili uweze kwenda Chuo Kikuu lazima ukae Chuo Kikuu miaka minne; sisi Chuo Kikuu minimum miaka mitatu. Kwa hiyo huwezi kuchukua mtu aliyesoma kwa utaratibu huu Kenya halafu ukamlete Tanzania asome miaka mitatu ilhali elimu yake haijamuandaa kufanya miaka mitatu ya Chuo Kikuu.

Mheshimiwa Spika, lakini wenzetu wa Kenya na wenyewe wamebadilika sasa hivi wanaenda six elimu ya msingi, three jumla miaka tisa elimu ya lazima three Sekondari na three Chuo Kikuu kwa hiyo wana six three three sasa hivi wamebadilisha na naamini kwa utaratibu huo itakuwa ni rahisi kuwapata wanafunzi kutoka Kenya.

Mheshimiwa Spika, sasa turudi kwa upande wetu sisi. Kwa upande wetu Sera yetu ya Elimu na Mafunzo ya 2014 inasema nchi yetu itatoa elimu ya lazima (compulsory education) miaka 10; na ndicho tulichosaini kwenye Sustainable Development Goal duniani, wakuu wa nchi wote walisaini. Na structure yake ni kwamba, tutakuwa six basic education, four secondary education. Kwa hiyo six plus four ni lazima kila mtoto asome pale. Halafu two high school three plus Chuo Kikuu, ndivyo Sera ilivyo, haijabadilishwa, ndiyo Sera iliyoko sasa hivi, haijabadilishwa. Tunachotekeleza sasa hivi, ni seven, four, two, three plus. Tunaposema tunafanya mapitio ya Sera, pamoja na mambo mengine tunataka kujiuliza, ile Sera ilivyokuwa tuitekeleze ilivyo? Kuna sababu ya kubadilisha? Economic necessity zake ni zipi, budgetary implication zake. Kwa hiyo kwenye timu inayofanya ile kazi kuna wachumi sasa hivi wanaangalia miundombinu yetu yote, human resource zetu zote tulizonazo na mfumo ambao tunataka kwenda nao kwa ajili ya kuangalia Sera yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Sera ipo ni six, four, two, three plus utekelezaji tofauti, ni seven four two three plus. Lazima tufanye maamuzi, hatuwezi kuwa na Sera hapa na utekelezaji hapa sera yetu lazima tufanye maamuzi na baadhi ya mambo mengine ambayo wameyazungumza hapa.

Mheshimiwa Spika, kwa uapnde wa Sera, hii ya structure ya elimu kama tukienda kwa sera ya elimu na mafunzo 2014, dhana yake, kama tukienda nasema maana maamuzi lazima yatafanyika, kama tukienda dhana yake basic education miaka sita, compulsory education miaka 10, basic education miaka sita punguza idadi ya masomo focus kwenye masomo ambayo wanafunzi wataeleza build strong foundation. Ukitoka pale wanafunzi kutakuwa na michepuo miwili wanaopenda vitabu sana na kusoma sana pengine asilimia 20 au wachache wataendelea huku watasoma trigonometrically complex number na kadhalika, na masomo mengi. Majority wataenda kwenye elimu ujuzi kwa miaka minne. Na watakapofanya mitihani masomo labda mawili, matatu manne, itakavyoamuliwa ndiyo watafanya chini ya NECTA; masomo mengine ni on the spot. Umejifunza ufundi magari, wiring, ya nyumba, uashi, useremala pengine, namna ya ku-repair ma-fridge na kadhalika utafanyiwa mtihani pale na mafundi wengine on the spot. Kwa hiyo utakapomaliza cheti chako cha miaka 10 kama ni kilimo unajua kilimo, kama ni kufuga wale nini aliosema Mheshimiwa pale wale wanaoliwa na kuku wale utafunzwa huko kama ni kufuga samaki na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hiyo ndiyo dhana iliyo kwenye elimu ya mafunzo ya 2014 ambayo kwa kiasi kikubwa imechukua mfumo wa Ujerumani wenzetu wa Zambia wanatekeleza something along those lines, kwa hiyo sisi lazima sasa tufanye maamuzi hatuwezi kuwa na Sera ikakaa kapuni halafu tukaenda kana kwamba hatukutunga Sera sisi wenyewe na Sera hii ilikuwa shirikishi sana lakini kama ambavyo nimesema sisi ni waumini wa utulivu kwa hiyo pamoja na kwamba kulikuwa na consultation tumeanza tena consultation na tunataka tuzimalize mwisho wa mwaka huu.

Mheshimiwa Spika, pengine tuna kitu cha kutosha kwenda kwenye maamuzi lakini tunadhani haitatusaidia sana. Tuendelee na consultation; na naomba Wabunge waendelee kutoa maoni pamoja na ile semina ambayo tulikuwa tumeifanya, lakini tutakapoyafanya haya kwa kweli nawaambia yatakuwa ni mageuzi makubwa katika historia ya nchi yetu katika elimu ni mageuzi ambayo yataitikia wito na maelekezo ya Rais. Kwamba elimu yetu iongeze ujuzi. Ni mageuzi ambayo yatakidhi kiu ya Wabunge wetu; kwamba elimu yetu iongeze ujuzi. Ni mageuzi ambayo hayatatuondoa kwenye utandawazi; kwamba wanaotaka kwenda kuwa marubani wa ndege au wanaotaka kuwa madaktari bado kutakuwa na mrengo wa kwenda kufanya masomo hayo na kuyasoma vizuri sana ili kuweza ku-compete katika dunia. Kwa hiyo hatutapoteza chochote tutakachofanya ni kwamba wanafunzi wote watakapomaliza kusoma; kwanza watamaliza wakiwa miaka 15, 16, 17 ni umri ambao unaweza ukaanza kutafuta ajira sasa hivi wanamaliza miaka 13, 12, 14 ni umri hata kwa sheria za ILO huwezi kutarajia huyu mtoto aende akaajiriwe.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hili la kwanza, la Sera. La pili ni kuhusu Sheria. Huku kwenye Sheria bado tutakuja kujadiliana nanyi. Lakini mojawapo lazima tufunge, kuhakikisha kwamba utaratibu wa kubadilisha mambo usiwe wa ghafla ghafla katika sekta ya elimu kama ambavyo imesemwa hapa.

Mheshimiwa Spika, la tatu ni suala la mitaala. Kazi ya mitaala imeshafanyika na imeenda mbali sana. Na juzi wakati wa semina ya Wabunge, nawahakikishia takribani asilimia 98 ya maoni ya Wabunge tulishayapata, tulikuwa nayo. Na ndiyo nikashukuru kwamba niliwaambia wenzangu wataalam tusiende sisi na kueleza kwamba tuna nini tuweke chini tuwasikilize Waheshimiwa Wabunge tukawasikiliza tukawa tunafurahi tukasema inaonekana tuko on the right track; haiwezekani haya mambo tumeshayakusanya watu zaidi ya 100,000 wametoa maoni na Wabunge wakati fulani kulikuwa na semina ya kukusanya maoni hayo hayo; kwa hiyo tunayasikia hata baada ya one year down the road we have the same views. Kwa hiyo kwa kweli it seems we have a stable system ya kwenda kubadilisha mitaala.

Mheshimiwa Spika, lakini tunaendelea kukusanya maoni; na Waheshimiwa Wabunge tunaomba tuendelee; ukiwa na maoni njooni tuendelee kuangalia. Ikifika Desemba tunataka tuwe na tuna rasimu zetu za mitaala na tuna rasimu ya Sera. Januari mwakani tunataka tuanze kuingia kwenye maamuzi ili tuhakikishe kwamba baadhi ya haya mambo yanatekelezwa mapema 2024 kuelekea 2025. Na mitaala hiyo inaangalia sana suala la ujuzi. Kuna mambo mengi tunajiuliza, nasema lakini siyo maamuzi, tunajiuliza tuna shule shikizi sasa hivi kwani miaka minne mwanafunzi hawezi kuwekwa kwenye kituo shikizi? Kama kuna eneo lenye shughuli kubwa ya ufundi wakajifunza darasani kidogo wakafanya on the field wakapelekwa kwenye field for four years akitoka pale anakuwa amekamilika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunapozungumza kwenda kwenye michepuo mchepuo mwingine kwenye kilimo. Kwa nini tusitumie maeneo yetu na vyuo vyetu vya kilimo; akienda kukaa pale mtoto akajifunza kilimo, akajifunza uvuvi, akajifunza mifugo biology kidogo na kadhalika akitoka pale ameshakamilika? Lakini hatutoacha kufundisha yale mengine physics, chemistry, biology, additional mathematics, advance mathematics kwa wale wachache ambao wana attitude na ambao tunawahitaji kwa sababu nchi hii inahitaji engineer vile vile; kwa hiyo kwenda huko hatuta-compromise kwenye quality ila itatoa fursa kwa kila mtu kuchagua mrengo anaotaka kwenda unaoona unamnufaisha. Watakaoenda kwenye ujuzi lazima tuwape path way ya kwenda Chuo Kikuu. Kutakuwa wana masomo machache ambayo ukiyasoma na ukiamua kwamba unataka kuendelea basi chukua hayo hayo nenda high school au tumia utaratibu ambao umeelezwa hapa; nadhani Mheshimiwa Mbunge mmoja alikuwa anasema lazima tuwe na utaratibu wa kuandaa foundation course. Tumtengenezee mtu foundation course akitaka kwenda kuchukua degree aende kwa sababu bila ya hivyo baadhi ya wazazi watasema mtoto wangu lazima aende kwenye ma-physics na chemistry na biology na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, la nne ni idadi ya walimu, wakufunzi na Wahadhiri ambao limezungumzwa sana hapa hilo nalo muhimu hata ukiwa na mitaala mizuri hata ukiwa na sera nzuri usipokuwa na walimu wa kutosha na kadhalika. Humu ndani kuna suala la distribution. Ukichukua - Basic Education Statistic of Tanzania (BEST) ipo available, kaangalie tu pupil per teacher ratio, mwalimu mmoja na wanafunzi Kasulu 104, Kinondoni takriban 31, wote wanafanya mtihani ule ule. Uyui 74, sawa, ukienda Arusha 31, wote wanafanya mtihani huo huo na nchi hii ni moja na wote wana haki. Kwahiyo distribution ya walimu lazima itumike kwanza kwa kupunguza makali haya. Lakini na mengine kwa sababu ajira zinaendelea tunaamini tutaenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, la tano ni ubora. Unakuwa na mwalimu wanakuwa na Mhadhiri wanakuwa na Mkufunzi. wanahitajika ku-update knowledge wanahitajika kuwa na fursa ya ku-exchange wanahitajika kukutana pamoja kuongeza ubora na huko mbele kuangalia tunapo-recruit walimu tuna-recruit vipi. Kwa sasa hivi kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu sana tumetumia 2.1 bilioni kufanya semina katika maeneo maalum ya walimu. Tumefanya Tanga, Bagamoyo na Morogoro nchi nzima; na Morogoro nimeenda kufungua mafunzo hayo kwa walimu wa kilimo na sayansi kimu. Wanakusanywa tena, wanakaa kama darasani wanabadilishana idea na kuongeza ujuzi. Tumeweka tena kiasi hicho cha bajeti naomba Waheshimiwa Wabunge mpitishe bajeti hii kwa sasa tutakuwa tunaendelea na mfumo huu huu.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa kushirikiana na TAMISEMI tunaimarisha sasa Teachers Resources Centers sehemu za walimu kwenda kukaa pamoja walimu wa hesabu wakae pamoja wapate na mtaalam wakae wa-update uwezo wao. Walimu wa kiingereza wakae wazungumze kiingereza kizungumzike maana yake kinafundishwa shuleni kwa hiyo tunaposema wanafunzi wana challenge ya kiingereza wakati tunafundisha maana yake ufundishaji wenyewe ndiyo challenge yenyewe, changamoto. Kwa hiyo huko tunakwenda lakini hata vyuo vikuu.

Mheshimiwa Spika, kwa kuanzia tu kwa vyuo vikuu sasa hivi tutaanza na ubora wa walimu. Tumesema tuwapeleke nje kwenda kusoma. Vyuo vikuu vyote duniani vinajaribu kupeleka watu mbali kwenda kusoma. Kachukue elimu hata China leta nchini mwako, hilo tunalifanya. Lakini lingine, tumesema, sasa hivi watu wanapanda vyeo kwa ku- publish kwenye journals ambazo hazitambuliki na haziko juu sana katika impact factor, hazikubaliki sana. Kwa hiyo tumesema kwa upande wa sayansi na tiba mwalimu wa Chuo Kikuu uki-publish kwenye journal top five zile kubwa ambazo zinafahamika ambazo mhadhiri wa pale aki-publish chuo kinapandishwa rank; wewe mwalimu ukiweza kufanya vile una milioni 50 cash una ondoka nazo na utazitumia unavyotaka.

Mheshimiwa Spika, tumetenga bilioni moja, na nina- challenge wahadhiri, hela hizo hapo bilioni moja tusije tukarudi nazo Bungeni mwakani. Tunataka tuone publication za Watanzania kwenye nature, kwenye landset, kwa sababu kule uta-publish kitu ambacho umekifanyia utafiti vizuri na kinaanza kuleta matokeo. Tumezungumza hapa, Mheshimiwa Abbas Tarimba umezungumza; tulikuwa na covid hapa, sasa tunataka hawa wafanyiwe research sasa hatutaki unafanya research unakimbilia kwenda kuangalia unafuga kuku halafu una daladala yako huwezi ku-concetrate. Unafanya research kwenye medicine ukifanya vizuri breakthrough milioni 50 cash mfukoni tumia unavyotaka. Tutaona inavyofanya ikifanya vizuri tutasonga mbele zaidi. Lakini tunaanzia hapa; South Africa uki-publish popote kwenye journal za juu unawekewa fedha kwenye akaunti yako kwa ajili ya kufanya research ku-recruit assistance na kusafiri sisi tunakupa cash tumia unavyotaka milioni 50.

Mheshimiwa Spika, lingine ni miundombinu. Ni kweli lakini Mheshimiwa Kipanga ameelezea kwamba tunahitaji kuendelea kuboresha miundombinu ya vyuo pamoja na shule zetu. Namshukuru tena Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwakweli maamuzi yake ya kusema kwamba fedha hizi zimekuja kwa ajili ya kupambana na UVIKO-19 na alisema Mbunge mmoja hapa tunaweza tukaondoa barakoa zote tukanunua na chanjo na kadhalika, tukasema tumefanya hivyo, na zipo nchi zimefanya hivyo, lakini alisema sisi tunataka kuondoa msongamano wa watu, kama tunataka kuondoa msongamano wa watu tuanzie shuleni, tujenge madarasa na wenye fedha zao wakaona kweli ni hoja nzuri, lakini dhana ya Rais wetu ilikuwa kwamba hizi fedha tutakapoziweka ziwe na impact long term zibaki. Kwa hiyo, hata COVID ikiisha tutabaki na madarasa yetu hiyo imetupeleka mbali sana.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tuna miradi kadhaa katika Wizara yetu ya kuendeleza ujenzi na napenda kusema tu kwamba na maelekezo hayo mradi wa HEET ambao unajenga miundombinu kadhaa katika vyuo mbalimbali hapa nchini, Vyuo Vikuu mbalimbali 14 sasa tumetenga katika kila fedha, tutakuwa tunatenga kiasi fulani kijenge Kampasi katika Mkoa ambao sasa hivi hauna Chuo Kikuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kampasi hiyo tunataka itumike for technical education isimamiwe na chuo for technical education, kwa sababu kilio chetu sasa hivi ni elimu ya ufundi tutaongea na ma-Vice Chancellor kwamba sawa hata kama ipo chini ya chuo chako basi itoe Diploma, au kitu kidogo pale ili watu wakitoka pale wameimarika vizuri wanaajirika. Kwa hiyo fedha hizo mazungumzo yamekubalika tunasonga mbele.

Mheshimiwa Spika, tutakuwa na Mikoa mingi sana sasa hivi ambayo haijaonja level hiyo ya elimu nadhani naweza nikataja Rukwa hapa, nadhani Kigoma mingi tu Mheshimiwa Sanga, kwa hiyo huko tunapokwenda tutakwenda vizuri kwenye miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika yale mambo saba kuna vitendeakazi, Walimu wanaandaliwaje kwa ajili ya kwenda kufundisha. Dhana iliyokuwepo na Mheshimiwa Ndalichako mimi nakushukuru sana umeniacha pazuri, dhana iliyopo ni kuhakikisha sasa tunaenda na tablets kwa Walimu huko tunapokwenda, kwa sababu kila mmoja anazungumza TEHAMA hapa, tunazungumza mitaala maoni ni vilevile tufundishe vijana wetu coding. Tunasikia Kenya wame-adopt lakini humu tumeshaipata tayari na kama tunaenda vile ina maana lazima tuwe tumejiandaa na vitendeakazi, huwezi kumfundisha mtu mambo ya computer kwenye ubao wa chaki, uanze kumwambia hii ndiyo nini, kwa hiyo huko tunakwenda na nina matumaini huenda mambo hayo yakatekelezeka haraka sana kwasababu maelekezo hayo yamekubaliwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mambo hayo saba lazima ni muhimu tuende nayo yote bila kupuuza hata moja. Nimesema la kwanza sera, sera nimetaja kitu kimoja tu kuna mengine hapa yamezungumzwa lugha nini na kadhalika na hayo yote tutaenda kwa kushirikiana na watu halafu tuende tuamue.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili tunazungumzia sheria. Sheria hii pamoja na kubadilisha Sheria ya mwaka 1978 ni pamoja na kukazia baadhi ya maeneo tusiwe tunabadilisha kiurahisi sana, yaani tuwe na utaratibu mzuri wa kubadilisha mambo ili wakati wa kubadilisha tuwe kweli tuna improve mabadiliko lazima yatakuja mbele ya safari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimezungumza tatu ni mitaala, kazi ambayo imeshaanza takribani mwaka mzima, halafu nimesema tunahitaji idadi ya Walimu, ubora wa Walimu, miundombinu na vitendea kazi.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie baadhi ya vitu vingine haraka haraka, liliulizwa swali moja hapa labda ningependa nilielezee na Mheshimiwa Abbas Tarimba, aliuliza vyuo vikuu kazi yao ni kufanya research, na vyuo vikuu siyo High School, hatuwezi kufanya Wahadhiri wa vyuo vikuu kazi yao ni kufudisha tu haiwi tena Chuo Kikuu.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu kazi ya Vyuo Vikuu ni production of knowledge and dissemination of knowledge, siyo dissemination of knowledge ivumbuliwe kwingine wewe kazi yako hapa ni kuwapa wanafunzi.

Mheshimiwa Spika, Mhadhiri wa Chuo Kikuu, Mhadhiri wa Chuo Kikuu lazima afanye research, push to the front of knowledge. Kuna baadhi ya maeneo tulipowekeza kwenye research matokeo yake yamekuwa mazuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nimetoka kilimo juzi hapa, tuna mbegu nyingi zilifanyiwa utafiti na TARI na ukienda Kongwa pale kulikuwa na mashamba, hata Mtama wa mbegu za kawaida hapa Mtama wa mbegu za masia, zimefanyiwa research na watalam wetu unaziona zinavyobeba tofauti kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunajua juzi hapa kwenye bajeti tulimwalika Researcher mmoja kutoka Zanzibar, alifanya research kuhusu mbegu bora za mpunga duniani anatambulika, alikuwa hapa amekaa na sisi, kwa hiyo kuwekeza kwenye research kunalipa.

Mheshimiwa Spika, tunayo chanjo ya kideri ni matokeo ya research na sasa hivi tunaweza tukaangalia katika tafiti kwa sababu sasa hivi wanakusanya zaidi za COSTECH lakini lazima twende beyond that, tuna miradi 145 ya tafiti ya kuangalia utafiti umeenda tumepata nini.

Mheshimiwa Spika, kinachohitajika huko tunapoenda lazima kwenye bajeti tuangalie Wahadhiri kuna bajeti ya research, Waheshimiwa Wabunge mmezungumza vizuri sana, kwamba sisi tusipoweka bajeti wafadhili ndio wataweka bajeti. Kulikuwa na mradi mkubwa sana wa research Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nakumbuka ulikuwa unaangalia dawa itokanayo na mitishamba, ulifadhiliwa na nchi moja ya Ulaya, matokeo yake yote yalikuwa yanachukuliwa kwenda Ulaya. Aliyekupa fedha ndiye mwenye haki miliki, walifanya research wapo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wenye taarifa zote wapo nje ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, sisi lazima tutoe fedha, ndiyo maana nimesema leo nawaombeni sana, Waheshimiwa Wabunge mtupitishie bajeti yetu, hizo fedha kidogo za research ambazo tunawapa hawa ni stimulus package tutaomba na watu wengine watoe fedha kwenye research zitatusaidia Wahadhiri wakiwa Chuo Kikuu wasiwe na mambo mengi kichwani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haiwezekani wewe umeajiriwa kufanya research kwenye medicine ili baadaye likija janga lingine kama UVIKO uweze kututafutia dawa lakini huna fedha ya kutosha kazi yako ni kutafuta shamba Kiteto na kwenda kufuga ng’ombe, huku unakwenda kuwa na daladala na kuangalia miradi halafu hujui ukistaafu unakwendaje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unakuta wako Maprofesa, tupo maprofesa publication zetu ukizitafuta uki-google huziona katika ma-journal ya hali ya juu lazima tubadilike! Kwa hiyo, naomba hiki kwa mfano Shilingi 50,000,000 kwa kila research ni hela ndogo, wenzangu walisema zitaisha Bilioni Moja, zinaweza zikabaki kwa sababu tumeshaanza na trend mbaya, naomba sana mtusaidie kupitisha hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, labda jingine kwa muda uliobaki, maoni mengine kwa mfano Vyuo Vikuu tunaajiri vipi, una mwajiri mtu Chuo Kikuu vipi? Tunalipokea. Mimi niliajiriwa baada ya muda fulani kwenye Idara yangu unafanya mtihani matokeo yanatoka unaambiwa wewe tunakubakisha hapa unaendelea kufundisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wapo watu wengi Waafrika, Wachina, Wahindi wanakwenda kusoma Marekani na kadhalika, wanaonekana wanafanya vizuri sana ndiyo unaambiwa wewe tunakutaka ubaki hapa usiondoke, sasa na sisi lazima tujiulize maswali tunataka tuajiri vipi, kwa mkupuo, kutangaza tunachukua cohort moja, Wahadhiri nimepata fursa ya ajira niliambiwa nikasema kwa Vyuo Vikuu punguza idadi tunataka tuajiri taratibu kwa performance na hatutaki kuajiri cohort ambayo yote inakuja kustaafu wakati mmoja.

Mheshimiwa Spika, hivyo niliongea na Mheshimiwa Mhagama nikasema hivyo vingine sasa Vyuo Vikuu napenda yule aliyefanya vizuri wa 4.6 tumwajiri kipindi hichi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuwekeeni akiba mwakani ikija akifanya vizuri mwingine tumchukue na tusipomchukua akiondoka anaenda huko anapata kazi nyingine matokeo yake kumrudisha haiwezekani siku unapoajiri you don’t get the best, kwa hiyo hizi hoja tutazibeba tutazifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba Waheshimiwa Wabunge mpitishe bajeti yetu na naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naafiki.