Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia. Kwanza, namshukuru Waziri wa Elimu na wote wanaotumikia Wizara hiyo wanafanyakazi vizuri sana, kimsingi Profesa Mkenda tunakuamini sana katika mambo yote unayoyafanya na kwa uwezo wako kwa hiyo tunategemea utaitendea haki hii Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo mengi sana yamezungumzwa humu ndani, ombi langu la kwanza kwa Profesa ni kwamba Bunge hili katika suala la elimu wamezungumza mambo makubwa ya kutosha. Kiandikwe kitabu maalum ambacho sisi kabla ya bajeti itakayokuja, tuanze kukisoma tuliyosema humu ndani yametekelezwa yapi? Mambo yaliyozungumzwa humu ni makubwa sana na kila Mbunge aliyeongea humu, maneno yake yasomeke Hansard zote zisomwe hilo ndilo ombi langu la kwanza kwako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu la pili kwako Profesa ni VETA Bunda Vijijini. VETA ukiniambia kipaumbele cha kwanza VETA, kipaumbele cha Pili VETA, kipaumbele cha Tatu ni VETA, kipaumbele cha Sita VETA leo nimemaliza, kwa hiyo tutakutana huko kwenye VETA najua utaiwekea mpango maalum.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kulizungumza niongee kwa Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, kazi inayofanywa na Mama Samia siyo ya mchezo ni kazi kubwa sana, Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, popote anapozungumzwa Mama Samia mjue inazungumza CCM. Kwa hiyo, lazima tukae chonjo, kuangalia siasa za kwetu zinaendaje. Mama anafanya kazi ametuletea fedha tumejenga madarasa, anahangaika huku na huku kwa ajili ya matumizi ya nchi yetu. Kwa hiyo, lazima tumlinde Mama afanye kazi kwa muda wote anaoutaka yeye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine Mheshimiwa Profesa nakuomba ufanye tathmini ya elimu bure, tunatoa Shilingi Bilioni 24-point hivi kweli tumefuatilia kwamba, Shilingi Bilioni 24 hizo zimegawanywa? Kuna asilimia 30 kukarabati, asilimia 30 huduma za shule, asilimia 20 sijui michezo, zinafanyakazi au tunapeleka Shilingi Bilioni 24 ambazo pengine tungezibadili tukajenga nyumba za Walimu tunapeleka hazina kazi ya kufanya? Tufanye review tuna miaka Sita sasa, kwamba hii elimu bure Shilingi Bilioni 24 tunazopeleka karibu Shilingi Bilioni 25 zinakazi gani sasa hivi zinafanyakazi iliyokusudiwa au zinaliwa? Kwa hiyo na hilo tulifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ambacho mimi nimekiona baada ya kupitia hotuba yako ni suala la watahiniwa. Kwa mfano, Darasa la Nne mwaka 2021, waliotarajiwa kutahiniwa ni 1,678,209 waliokuja kutahiniwa ni 1,561,599 wanafunzi 116,610 hawakujitokeza wanakwenda wapi? Hawakuja, ni watoro wanakwenda wapi? Shule ya Msingi 2021, waliotarajiwa ni 1,132,084 waliokuja ni 1,108,023 ambao hawakufika ni 24,000 wamekwenda wapi, wanafanyakazi gani? Kidato cha Pili ni wanafunzi 652,611 waliotajariwa, waliokuja ni 602,955 wanafunzi 49,656 hawakuja, wamekwenda wapi, wanafanyakazi gani? Kidato cha Nne Wanafunzi 538,024 waliokuja ni 521,351 wanafunzi 16,673 hawakuja kufanya mtihani.

Mheshimiwa Naibu Spika, amekuja Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Bashungwa juzi tulikuwa naye Bunda ametuambia Halmashauri ya Bunda peke yake wanafunzi 7,000 hawakufanya mitihani kwa mujibu wa ripoti ya CAG, hawakufanya! Ndiyo maana nikipiga kelele humu ndani kwamba Bunda kunahitaji kujengwa sekondari kutokana na umbali wa wanafunzi mniunge mkono kwenye hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanafunzi 7,000 nchi nzima ni Bunda kwa umbali wa sekondari zilivyo, kwa hiyo hilo nalo utalifanyia kazi. Kwa hiyo, sekondari zile ambazo zinajengwa na wananchi mziunge mkono ili tupunguze hao wanafunzi ambao hawaendi kufanya mtihani.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nilikuwa nalizungumza hapa ni suala la kukopa, yaani mikopo ya wanafunzi wa Chuo Kikuu. Mimi naomba kama inawezekana kwa mwaka mmoja tu au kwa bajeti moja tu, tukubaliane kwamba wanafunzi wote wanaotaka kusoma tuwalipie karo, wote wenye kuhitaji kusoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiwalipia karo mahitaji mengine wanayofanya tutachangiana. Hebu mwaka mmoja bajeti moja tukubaliane, wanafunzi wote waliokwenda vyuo vikuu tuwalipie karo ili tuone kwamba itakuwaje, si kila kitu ni kujaribu tuone, kwa sababu shida kubwa ya wanafunzi ni karo, hata kama tunalipia karo kila mtoto atakuwa na uwezo wa kusoma. Hili nalo tuliangalie tuone linakwendaje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala langu la mwisho nililokuwa nataka kulizungumza leo ni elimu bure. Tumekubaliana Chama Cha Mapinduzi, Sera ya Chama Cha Mapinduzi tumekubaliana tunatoa elimu bure shule ya msingi mpaka sekondari lakini katikati hapo kuna kidato cha tano na sita; ukiangalia kidato cha tano na sita ni sekondari sasa kwa nini hatuwapi elimu bure? Umefika wakati sasa tuangalie kidato cha tano na sita tutoe elimu bure ili tukamilishe kile tunachosema elimu bure kwa shule ya msingi na sekondari. Kwa hiyo, tukubaliane kwamba mwaka ujao tupange mikakati ya kutoa elimu bure kwa kidato cha sita na sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)