Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi asubuhi ya leo kuchangia kwenye Wizara hii ya Elimu.

Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri na kubwa aliyoifanya kwa muda mfupi. Ndani ya muda mfupi tumeona madarasa nchi nzima yamejengwa kwenye level ya sekondari. Kazi nzuri haijawahi kutokea, pongeza nyingi sana kwake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze pia Wizara ya Elimu kwa kuendelea kusimamia Wizara hii na mwendelezo wa sekta nzima ya elimu. Mimi binafsi nataka kuchangia kwenye masuala mazima ya mitaala yetu ambayo tunayo. Mitaala yetu imekuwa ni mzigo kwa vijana wetu maana katika mitaala hii wakati mwingine tunazalisha vijana ambao hawawezi kujiajiri wenyewe, tutengeneze mitaala ambayo itaweza kutusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mdogo mtoto wa darasa la kwanza mpaka darasa la saba, anakuwa na masomo mengi mpaka kumi na moja kumi na mbili. Madaftari yale yanakuwa nayo mengi sana, anasoma sayansi kilimo, sayansi kimu, uraia, historia, hisabati, a lot of things.

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo mengine anayoyasoma mtoto huyu tunamrundikia vitu vingi ambavyo havina ulazima kwa umri wake. Sasa tufike mahali mitaala yetu tuichambue na tuwape vijana masomo machache ikiwezekana masomo minimum yawe angalau matano au sita, hata manne tu inatosha. Hakuna ulazima wa kumbebesha mzigo mkubwa mtoto wetu mdogo, asome vitu vingi. Tufanye kuwe na option, lazima mtoto aanze kuchagua kusoma level ya chini.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazunguka duniani tunaona wenzetu, unakutana kule na watoto hata ukiwauliza Tanzania iko wapi hawaijui, ukimuuliza sijui wapi, hawaelewi vitu vingi, lakini mtoto wetu mdogo unamfundisha vitu vingi, ajue Marekani, ajue sijui China, South Africa, ajue tulitoka wapi, a lot of things tunawapa vijana wetu. Tupunguze hivi vitu kwa vijana wetu, tuwape vitu vichache ambavyo vinaweza kuwakomboa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naweza nikakupa mfano mdogo tu katika mitaala yetu. Leo tuna mitaala tunamfundisha mtoto wetu tulianza sisi kuwa masokwe, sokwe lile likabadilika baadaye likaja kuwa binadamu, hivi kweli kwa elimu ya sasa hivi sokwe huyu anabadilika anakuwa binadamu? Wanasayansi wetu watusaidie. Mbona hatuoni continuation ya masokwe kuwa binadamu Profesa atusaidie, wanasayansi watusaidie, continuation ya masokwe kuwa binadamu, mbona hatuioni, lakini bado tunamlazimisha mtoto asome kwamba tulikuwa sokwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, humu wote sisi tuna dini zetu, kuna Waislamu na Wakristo, kwenye vitabu vyetu hatuoni sehemu imeandikwa tumeanzia kuwa sokwe ndiyo tukawa binadamu au wenzetu tunaelewa vipi? Mimi sielewi! Tulianza kuwa sokwe, tumebadilika sokwe likawa baada ya mamilioni ya miaka, hivi hatuna sokwe leo waliofikisha miaka mamilioni wakabadilika kuwa binadamu? Kama tu kwa sababu tumefanana na sokwe basi tulikoanzia kuwa sokwe, kweli? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ni hivyo tuseme, muda mrefu simba alianza kutoka kuwa mbwa, maana yake mbwa anafanana na simba, hivyo hivyo, baada ya miaka mingi mbwa akabadilika kuwa simba, tuandike hivyo kwenye vitabu vyetu. Baada ya hivyo tuseme mbuzi baada ya miaka mingi anabadilika anakuwa ng’ombe, kwa sababu wanafanana.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Taarifa.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipa fursa hii naomba tu kumpa taarifa mzungumzaji kwamba ndio maana wanafunzi wetu au watoto wetu hawawezi kusoma somo la historia kwa sababu wanaamini moja kwa moja kwamba ni uongo. Wakifika Kanisani wanaambiwa wao wameumbwa na Mungu, lakini wakienda kwenye madarasa wanaambiwa kwamba mwanadamu anatokana na Sokwe, kwa hiyo hawawezi kusoma kwa sababu wanaona historia ni uongo. Ahsante sana. (Makofi)

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani tukawa na mitaala ya aina hii halafu ukataka watoto watoke wawe competence, haiwezekani! Hii ni mitaala ambayo inatakiwa tuiboreshe na hii hadithi ya kuwa tulitoka sokwe tukawa binadamu, tupeleke ile sehemu ya masomo hata vile vitabu vya hadithi, kama vile vitabu vya alfu lela ulela, vitabu vya abunuwasi, zikawemo na hizo hadithi kwamba tulianzia huko lakini sio kumfanya mtoto…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpa mchangiaji taarifa kwamba hawa masokwe ambao walikuwa wakibadilika kuwa watu kwa sasa tunaona hawabadiliki, sasa sijui kwa nini. (Makofi)

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, napokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli na tunaona sasa hivi binadamu tunazaliwa, tunakua, tunafariki; masokwe yanazaliwa, yanakua, yanakufa. Sasa mbona hayabadiliki haya kuja kuwa binadamu na tunawapa watoto wetu wasome wanakariri, wanapoteza muda mrefu kusoma hizi hadithi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunawapoteza vijana wetu kwa mifumo ya elimu ya aina hii tupunguze, tuweke vitu vya msingi kwenye elimu yetu, watoto wetu hata kama wana masomo matatu aanze kuanzia darasa la kwanza. Ikifika la nne anachagua vitu vya kusoma na masomo haya ya ujuzi mtoto aanze kusoma kuanzia darasa la nne anamaliza darasa la saba anajua kitu. Akienda form one mpaka form four amebobea kwenye ujuzi, lakini leo vijana wetu wanafika form six, hajui chochote, anaenda Chuo Kikuu anamaliza na miaka 27, haelewi, anasubiri kuajiriwa, wataajiriwa wangapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima tutengeneze vijana wa kujiajiri wenyewe ili waweze kujiajiri wenyewe lazima tuwape ujuzi wakiwa bado vijana wadogo darasa la nne, tano, sita, akimaliza darasa la saba amekomaa, akiingia form one anaendelea kukomaa zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vijana hawa wachague masomo yasiyopungua matatu, unamrundikia masomo asome historia, sayansi, hesabu, unapataje vijana competence, haiwezekani! Hata Walimu lazima tuwe na Walimu ambao wako competence, wakiwa wamebobea kwenye masomo hata moja tu, kuna ulazima gani Mwalimu lazima awe competence katika masomo matatu, haiwezekani! Ni lazima tutengeneze utaratibu wa kuwafanya vijana wetu wawe wabobezi, wabobee kwenye masomo wanayoyasoma, tutapata mafundi na tutapata Taifa la teknolojia.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi dunia imebadilika, mambo yote siku hizi kwenye mtandao, hizi hadithi hizi tulikuwa masokwe sijui nani, soma tu kwenye mtandao, soma kwenye simu, laptop, inatosha, lakini sio kumpotezea kijana wetu muda mrefu, anasoma vitu ambavyo haviji kumsaidia. Tumeona Profesa umekabidhiwa Wizara hii, tunataka tuone mabadiliko makubwa kwenye mitaala ya elimu, vijana wapate ujuzi wa kuja kuwasaidia wao ili kuweza kuboresha maisha yao kwa sababu tunasoma wote ili tupate hela.

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna anayesoma hapa aje akose hela na hata mzazi anapomsomesha mtoto wake, anaamini kesho atapata pesa, bila hicho kitu haieleweki, mtu asome miaka mpaka 27, halafu tena arudi nyumbani, ameuza ng’ombe, ameuza nini, amefilisika na mtoto naye akashiriki kumfilisi, halafu mwisho wa siku unaweza kusema ajira wataajiriwa, hiyo Serikali ya kuajiri wote hao ipo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)