Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Mussa Ramadhani Sima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu. Pia na mimi niungane na Wabunge wengine kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakishukuru Chama changu Chama cha Mapinduzi kwa kuja na Ilani bora kabisa ambayo inatekelezeka. Nichukue fursa hii kumpongeza Waziri na timu yake yote. Kwa kweli wanafanya kazi nzuri na kazi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mchango wangu nianze kwa rejea ya Mwanafalsafa anaitwa Lord Macaulay ambaye pia alieleza kwa undani zaidi kuhusu mambo ya elimu alisema: ‘‘ukitaka kumtawala mtu ama jamii, haribu mfumo wake wa elimu na utamaduni wake’’. Haya aliyasema mwaka 1835. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitaka elimu yetu iwe bora au ukitaka maendeleo katika nchi maana yake uwekeze kwenye elimu, msingi wa maisha yetu ni elimu. Hili ni jambo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Wizara ya Elimu ndiyo inafanya kazi kubwa ya kuandaa Sera, ya kuandaa Mitaala, inaandaa Sheria lakini inawaandaa Walimu, inaandaa teaching and learning resources kwa maana ya vifaa vya kufundishia na kujifunzia, lakini inaandaa miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii ikishakamilisha kazi yake inakabidhi TAMISEMI kwenda kutekeleza haya ambayo wameyaandaa wao. Hapa ndipo tunakoenda kuwa na mkanganyiko wa utekelezaji wa malengo ambayo yamewekwa ya Wizara hii ya Elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mabadiliko haya yalifanyika wakati tumeingia kwenye ugatuaji wa D by D wa Wizara ya Elimu kukabidhi majukumu yake kwenye Wizara ya TAMISEMI kwenye utekelezaji. Changamoto ninayoiyona ni ongezeko la gharama katika uendeshaji kwenye eneo hili la elimu. Leo TAMISEMI yupo Naibu Waziri anayeshughulikia elimu, yupo Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia elimu lakini yupo Mkurugenzi anayeshughulikia elimu. Halkadhalika ukienda kwenye Wizara ya Elimu hivyo hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunahama sababu zilizotufanya tuhame Wizara ya Elimu iache kushughulika na Walimu moja kwa moja ama na elimu kuanzia chini mpaka mwisho, tuliangalia sababu mbalimbali. Sababu ambazo leo inawezekana haziko valid. Nataka kuiomba Serikali irudi tena ikatazame jambo hili kama bado lina tija kuwaachia Wizara ya TAMISEMI kusimamia suala la elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama haiwezekani tumewapa kazi hii Wadhibiti Ubora. Wadhibiti Ubora ni kama TCU kwenye level ya Vyuo Vikuu. Wao wako kwenye level hii ya chini. Wadhibiti Ubora hawa ni kama CAG lakini tumewaacha, Wadhibiti Ubora ukiwaangalia kazi wanayoifanya haiendani na kile ambacho kinatakiwa kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Elimu ilipaswa kuwekeza zaidi kwa hawa Wadhibiti Ubora ndiyo daraja, ndiyo injini yao. Sasa injini ambayo inawapa taarifa ya kwenda kusimamia utekelezaji kwamba TAMISEMI wamefanya nini? wao wawaletee taarifa, injini hii haifanyi kazi ipasavyo kwa sababu haijawezeshwa. Naiomba Serikali iende ikahakikishe inawawezesha Wadhibiti Ubora kufanya kazi yao vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo langu la pili ambalo ningependa pia nilichangie na pia napenda nifanye rejea ya Muingereza John Rusk ambaye ni Mwandishi nguli na Mwanafalsafa. Huyu alisema naomba ninukuu “quality is never an accident but a result of intelligent effort.” Kwa tafsiri isiyo rasmi, ubora hauji kama ajali bali ni matokeo ya fikra nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mtaala wetu unazungumzia competency-based education kwa maana ya ujuzi. Utekelezaji wake ni knowledge-based education. Hapa nataka niipongeze Serikali, Wizara ya Elimu hasa kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania, wanaandaa vitabu ambavyo vinazungumzia competency-based education (COBET). Lakini shida ninayoiyona anayekwenda kutumia vitabu hivi ni Mwalimu ambaye hajaandaliwa kwenye ujuzi. Changamoto hii itakuwa kubwa sana, wamefanya semina kwa Walimu wa Shule za Msingi semina ya muda mfupi lakini Sekondari bado. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama unaandaa vitabu ambavyo vinazungumzia ujuzi lakini elimu unayoenda kuitoa ni ya maarifa usitarajie utakuwa na elimu bora. Kwenye Bajeti hii ambayo imetengwa Serikali isiwekeze ziadi kwenye infrastructure tuende tuwekeze kwenye teaching and learning, tuwekeze kumwezesha Mwalimu, tumpe Mwalimu ujuzi, Mwalimu akasome kile kitabu. Kwa sababu ukizungumzia kitabu cha competency maana yake Mwalimu asome kitabu aelewe aweze ku-generate mawazo yake. Lakini sasa ukiacha hivi, Mwalimu ataenda kutafuta handout mtaani ambayo ina majibu tayari anarahisisha ufundishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mtu wa pili hapa ni mpimaji. Mpimaji hapa ni Baraza la Mitihani. Wabunge ni mashahidi, mtoto anaanza Darasa la Kwanza mpaka la Saba anaenda kupimwa kwa masaa hayo lakini hakuna continuous assessment kulikuwa na haja gani ya huyu kufanya annual examination kuanzia mwanzo mpaka mwisho lakini mwishoni tunaenda kuchukulia mtihani wa mwisho tunaacha continuous assessment? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtoto anamaliza Darasa la Saba anafanya hata hesabu kwa multiple choice, are we serious? Halafu unataka aende form one aende huyu akaanze sasa ku-generate mawazo, haiwezekani! Leo Baraza la Mitihani wamekuja na digital marking. Digital marking Mwalimu mwenyewe hayupo digital. Lakini digital marking hii inazingatia competency ambayo inaandaliwa na Taasisi ya Elimu ya Tanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa mnaiona discoordination kati ya mwandaaji wa vitabu lakini anayekwenda kufundisha vile vitabu na anayekwenda kupima kuna discoordination. Ninaliona anguko la elimu kesho kama hatujaenda kusimamia hii mifumo yetu vizuri ifanye kazi kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana nilichangia eneo la ujuzi na ufundi na nilitoa mfano mzuri sana. Tume ya Mipango ilitoa ripoti yake 2014 iliongozwa na Dkt. Mpango ambaye leo ni Makamu wa Rais. Katika ripoti yake ilisema elimu ya ujuzi inayotolewa haiendani na soko la ajira tulilonalo, kwa nini? Kwa sababu ya maandalizi ambayo tunayafanya kwa nini kwa sababu tumefuta FTCs. Leo ukienda huko kwenye FTCs wote wanatoa degree, tumeacha kuandaa wataalam tunaandaa wasimamizi (administrators, managers). Sasa hawa wataenda kumsimamia nani wakati hakuna mtu aliyeandaliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nitoe mfano mdogo, China mwaka 2014 walirudisha Vyuo Vikuu 600 kuwa vyuo vya kati, kwa sababu walitambua soko kubwa ambalo linatakiwa leo ni kuwaandaa watalaam badala ya kuandaa wasimamizi. Sisi leo hawa NACTE, NACTVET whatever wanavyoitwa na TCU hatutajua nani kati yao anasimamia vyuo vikuu, kwa sababu huku NACTE kuna vyuo vikuu na huku kuna vyuo vikuu. Nataka kuiomba Serikali, hatujachelewa, turudi kuimarisha vyuo vyetu vya kati ili kuweza kupata vijana wazuri ambao wameelimika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niipongeze Serikali, mwaka jana pia tulizungumza jambo jema sana hapa, juu ya vijana ambao wanamaliza kidato cha nne kuweza kupata fursa ya kuweza kupata elimu ya ufundi. Serikali imetoa fursa kwa miezi sita na inawalipia vijana hawa kwenda kwenye vyuo vyetu vya ufundi na sasa imetoa fursa nyingine, hili jambo jema sana, lakini je, kuna follow-up ya hawa vijana wetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo linatakiwa liwe continuous, liwe kwenye bajeti, lisiwe ni jambo ambalo Serikali inaweza ikaamka leo ikaamua, kesho wasiamue. Kama hawana fedha hawawezi kwenda huko. Motivation ni jambo la msingi sana. Msingi wa elimu Tanzania ndio msingi wa maisha ya Watanzania, haiwezekani elimu yetu ikawa tofauti na maisha tunayoishi sisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, anazungumza hapa Profesa Kishimba, anazungumza huwezi kupata majibu, ukimsikiliza vizuri anatuonyesha wapi tumeteleza na huko tulikoteleza maana yake sisi hatutaki kujikwamua, tunataka kuacha tufuate mawazo anayoyazungumza. Kwa mawazo yake hakuna sababu ya mtoto kumpeleka shule.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Serikali iwe inatoa majibu, kama anazungumza mtoto umempeleka shule anarudi nyumbani hawezi kuuza ng’ombe wengine ampeleke mwingine, maana yake hakuna sababu ya kumpeleka mtoto shule. Tutoe majibu na tuonyeshe umuhimu wa elimu. (Makofi)