Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu nichangie hotuba hii ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na leo nina machache sana dakika tano zinanitosha. La kwanza, ni ombi, kumekuwa na maombi kwa wale wanaopenda kutumia lugha ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia lakini pia lugha ya kujifunzia. Serikali ianzishe shule ya mfano ambayo itafundisha Kiswahili darasa la kwanza mpaka Chuo Kikuu, ili kufuta kabisa wazo kwamba Kiswahili kinafaa au hakifai kufundishia. Suala hili litaonesha mfano mzuri, nimekuwa nikisema hivi watu wanaleta hoja yangu mimi binafsi badala ya kuchangia hoja, wanasema wewe wanao wamesoma Ulaya au wamesoma nje ya nchi, wanangu wamesoma hapa hapa Tanzania. Watu wachangie hoja na kama hawakufanya research, hawakufanya utafiti, basi hawana haja ya kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, liko suala la pili ambalo pia ni ombi, naomba Serikali ifanye utafiti mahususi je, lugha ya Kiswahili inafaa kufundishia au haifai kufundishia inafaa kujifunzia au haifai kujifunzia? Kumekuwa na tafiti kwa miaka 45 zote zinasema lugha ya Kiswahili ndio lugha mama kwa Tanzania inafaa kufundishia. Naomba Waziri Mheshimiwa Profesa Mkenda hebu, wafanye tena utafiti ili suala hili tulisahau kabisa, utafiti utoe jibu je, lugha ya Kiswahili inafaa kufundishia au haifai kufundishia? Watu waache kusema, watu wanaoomba Kiswahili sasa watoto wao walisoma nje ya nchi, watoto wetu wamesoma hapa hapa nchini na kwa kweli suala hili litakuwa la maana sana sana kama utafanyika utafiti leo ili kupata jibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba Watanzania wajiamini kwamba Kiswahili ndio lugha inayofaa kufundishia lakini pia kuwe na utashi, kinachokosekana hapa naona ni utashi. Watu hawana utashi wa kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia. Utashi wa kisiasa, nina imani iwapo kutakuwa na utashi wa kisiasa lakini uwepo utafiti wa kutosha kabisa kwamba Kiswahili hakifai au kinafaa. Utafiti wangu mimi mtu mmoja mmoja nimefanya, Kiswahili kinafaa kufundishia. Utafiti wa kina Profesa Mlama waliokuwa hapa jana, BAKITA, lakini pia TATAKI (Taasisi ya Taaluma za Kiswahili) pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wamefanya utafiti na kuthibitisha kabisa kwamba Kiswahili kinafaa kufundishia. Wameandaa vitabu, vyote vipo lakini hatuna utashi wa kisiasa wa kukipenda Kiswahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna uthibitisho wa kutosha kwamba duniani kote hakuna nchi iliyoendelea kisayansi kwa kutumia lugha ya mtu mwingine lugha ya kuazima. Kote tulikokwenda kusoma nje ya nchi tumejifunza kwanza lugha ya nchi ile ndipo ufundishwe masomo ambayo umeenda kusoma. Uchina, Ufaransa, Uingereza, Urusi, Denmark, Sweden kote waliokwenda kusoma nchi za nje, watu wamejifunza kwanza lugha ya nchi ile kabla ya kujifunza masomo yale yaliyompeleka mtu kwenda kusoma. Nina Imani, leo naonekana kama nasema peke yangu, lakini baada ya miaka mitano, sita, kumi mtakuja kuniunga mkono lakini tusiache suala hili likapita kienyeji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)