Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Robert Chacha Maboto

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kupata nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia Wizara hii ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Lakini mimi ninayechangia sina elimu ya juu, nina elimu ya chini, kwa maana ya elimu ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Juzi alikuwa anazindua suala la utalii kwenye nchi yetu, ambapo ukija ukiangalia kwenye Mkoa wa Mara, Mbuga ya Serengeti kwa sehemu kubwa iko upande wetu; kwa hiyo tunampongeza kwa kazi kubwa hiyo anayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Wizara hii ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia, mimi nilitaka kuzungumza jambo moja tu kuhusiana na suala la vyuo vya ufundi. Kwamba, vyuo vya ufundi vikiboreshwa aidha vikaongezeka vikawa vyakutosha kwenye maeneo yetu, ikiwezekana kila Wilaya au Jimbo kutokana na wingi wa vijana wetu vitatusaidia kuwafanya wao wafundishwe vitu ambavyo wanaviishi kwenye maeneo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimekuja kupata shida hapa kwenye nafasi hizi zilizotolewa za ualimu. Kwamba shule moja inahitaji mwalimu mmoja, lakini waliyotuma maombi pale kwenye nafasi hiyo ya mwalimu mmoja ni walimu zaidi ya 800; halafu anachukuliwa Mwalimu mmoja, wale 790 wanabaki. Halafu kila wanapobaki muda wao wa kustaafu unazidi kuwasogelea. Najiuliza muda wao utakapoisha hawa watu watakuwa wanafanya nini? Lakini pia najiuliza hawa watu wakifundishwa kwenye vyuo vya ufundi kwa mfano Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kisangwa kile kilichopo pale Bunda, kikaboreshwa vizuri na Serikali kikaweza kuchukua vijana wetu wengi, wale waliomaliza Darasa la Saba hata wengine waliomaliza Kidato cha Nne ambao hawakupata nafasi ya kuendelea; wakaenda pale wakafundishwa shughuli zao za mikono ambazo wao kwenye maeneo yao wanayoishi hazitawafanya zitawafanya waweze kumudu maisha? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sasa ukija ukiangalia walimu wamepata elimu yao ya ualimu lakini nafasi zinazotoka ni kidogo na hawawezi kuitumia nafasi hiyo. Kwa hiyo, mimi nikawa napenda kuishauri Wizara hii ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kwamba kwenye Mpango wake mkubwa ni vizuri ikaboresha vyuo vya ufundi. Ili kwamba tukiwa na wimbi kubwa la watu ambao wamekaa hawawezi kufanya kazi, lazima tuwe tunajiuliza mara mbili mbili matokeo yake ni nini? Lakini hata wale wanaosoma sasa leo lazima waone wale wenzao waliotangulia wanachokifanya ni kitu gani au ninafasi gani wanayoipata na kama wanaona nafasi ni kidogo lazima watafute njia ya pili ya kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia mimi sidhani kama ingewezekana Taifa zima hili la Tanzania watu wote tukawa tuna degree; atakayeweza kumbebea mwenzake mzigo atakuwa nani? Haiwezekani. Kwa hiyo mimi ninaishauri Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu kuboresha vyuo vya ufundi tena kwa speed kubwa kwa sababu vijana wetu wakipata utaalam wao pale utawawezesha wao kuishi mitaani kwa kufanya shughuli zao wao wenyewe na kwa kujiajiri wao wenyewe. Na kujiajiri kwao wao wenyewe kutawafanya shughuli yao wao wanayoifanya wachange kwenye mfuko wa Serikali kwa kulipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu vijana wetu wa bodaboda, kwa mfano leo hii tusingekuwa na mpango huu wa bodaboda kwamba vijana wamejiajiri kwenye bodaboda, wale wote wangekuwa wako mitaani wamekaa wanasubiri kuomba ajira Serikalini ilhali nafasi zenyewe zinazotoka za ajira ndiyo hizo; kwamba kati ya watu 800 anatakiwa kuchukuliwa mtu mmoja na wale wangeongezeka ingekuwaje? Kwa hiyo wimbi la watu ambao hawana kazi lingekuwa ni kubwa kuliko uhalisia wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana mimi nilikuwa nashauri kwamba ni vizuri Wizara hii ikaboresha vyuo vya ufundi na kuviongezea upana wake ili iweze kuchukua wanafunzi wengi zaidi ili hawa vijana wetu watakapomaliza kujifunza utaalam wao watajiajiri wao wenyewe kama vile ambavyo vijana wetu wa bodaboda walivyojiajiri wao wenyewe. Tofauti na hapo kwa kweli itakuwa hata hawa ambao wamepata elimu zao wanafika sehemu wanataka kuchukia kile alichokisomea.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine najiuliza, mtu wakati mwingine anakuja ana degree yake, amemaliza shule ana degree; lakini hata ukimuuliza ile namna ya kujieleza baadhi yao hata kujieleza tu hawezi. Sasa unajiuliza wewe hata kama umesoma ni kweli una degree, degree hii hata huwezi kwenda kuiishi mitaani au kwa mazingira yako unayoyaishi wewe huweizi kuitumia inakuwa inakusaidiaje? Ndiyo maana nasema, watu wakifundishwa katika uhalisia wao wa maisha yao utawaondolea umasikini kwa sehemu kubwa. Lakini pia itawafanya wao wajiajiri wao wenyewe, vilevile wao pia watakuwa fundisho kwa wenzao. Kwamba nikiona njia hii ya ajira imebana nitakwenda njia nyingine ya pili ambayo itanifanya na mimi niishi kama fulani anavyoishi yeye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukisema watu wote wafanye kazi aina moja naamini kwamba nafasi hizo pia hazitaweza kupatikana. Mwisho watu watakaa kubaki kulalamika Serikali kwamba Serikali haitoi ajira lakini Serikali itatoa ajira baada ya kuwa ina income ya kuweza kuwalipa watu Mishahara. Na Serikali kupata mishahara ya kulipa watu ni lazima watu wawe wanafanya kazi, wanapata pato, wanalipa kodi na Serikali inapata fedha ya kuwalipa watu mishahara. Kwa sababu Serikali haiwezi kulipa watu mishahara kwa kupitia fedha ya kukopa, haiwezekani; ni lazima watu wafanye kazi, wazalishe wapate fedha kwao wao wenyewe na fedha zao zitumike kuwalipa mishahara wananchi wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi niliona kwenye suala hili la Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia nitoe mchango wangu huo ili kwamba Wizara hii ikituboreshea chuo chetu kile cha Maendeleo ya Wananchi pale Bunda, ikakipanua, itaweszesha vijana wetu wengi waende kupata mafunzo yao pale na mafunzo yale yatawawezesha kuishi vizuri kwenye eneo lao baada ya kuwa wanafanya shughuli zao ndogondogo za mikono na zitakazowezesha kuendesha maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mara baada ya kusema hayo, nakushuruku kwa kupata nafasi hii, ahsante. (Makofi)